Na Byera Deus, Bukoba

Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Abel Nyamahanga, amezindua kampeni ya PikaSmart awamu ya pili mkoani Kagera kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Yahya Ramadhani Kido, inayolenga kuhamasisha wananchi kutumia umeme kama nishati safi, salama na nafuu ya kupikia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliohudhuriwa na mamia ya wananchi, Dkt. Nyamahanga alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ajenda ya kitaifa inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuzingatia umuhimu wake katika kulinda afya za wananchi, kupunguza gharama za kaya, kuhifadhi mazingira na kuokoa muda wa familia.

Alisema Mkoa wa Kagera unaendelea kutekeleza ajenda hiyo kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kaya na taasisi zinazohudumia idadi kubwa ya watu.

Alieleza kuwa kuunganishwa kwa umeme katika vijiji vyote vya mkoa huo kupitia juhudi za Serikali na Wizara ya Nishati kumeweka mazingira wezeshi kwa wananchi kutumia umeme katika shughuli za kupikia.

“Tangu kuanza kwa juhudi za Serikali na wadau mbalimbali kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, taasisi zaidi ya 80 zinazohudumia watu wengi zimeanza kutumia nishati hiyo, na hivyo kupunguza matumizi ya kuni na mkaa,” alisema Dkt. Nyamahanga.

Aliongeza kuwa kampeni ya PikaSmart inatarajiwa kuongeza uelewa na matumizi ya umeme katika kupikia, sambamba na azma ya Serikali ya kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Dkt. Nyamahanga alisema Serikali inapohamasisha matumizi ya umeme katika kupikia, inalenga kuhakikisha wananchi wanatumia ipasavyo miundombinu ya umeme ambayo tayari imewekezwa kwa ajili yao.

Aliwataka wananchi wa Kagera kutumia umeme si kwa ajili ya mwanga pekee, bali pia kupikia, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza moshi majumbani na kulinda afya za wanawake na watoto dhidi ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji. Aidha, alisema matumizi hayo yanaweza kupunguza gharama zinazotumika kununua mkaa na kuni.

Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, aliwaagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na viongozi wengine kuhakikisha elimu kuhusu matumizi ya umeme kupikia inawafikia wananchi hadi ngazi ya vijiji, huku wakitoa mwongozo kuhusu matumizi bora na salama ya majiko ya umeme.

Kwa upande wake, balozi wa kampeni hiyo kutoka Tanzania House of Talent (THT), Mrisho Mpoto, alisema kampeni ya PikaSmart inatekelezwa kwa kuungwa mkono na Serikali na kufadhiliwa na mradi wa Modern Energy Cooking Services (MECS) kupitia Chuo Kikuu cha Loughborough nchini Uingereza.

Alisema kampeni hiyo inatekelezwa na THT Innovation Limited kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Kwa mujibu wa Mpoto, kampeni hiyo itafanyika katika mikoa saba nchini na itahusisha mikutano ya uhamasishaji pamoja na maonesho ya vifaa vya kupikia kwa umeme. Pia, wananchi watapata fursa ya kufahamu na kupata majiko ya umeme kwa gharama nafuu kupitia mifumo inayowezesha malipo ya awamu.

Naye Afisa Uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Kagera, Liian Mungai, alisema shirika hilo linaunga mkono kampeni ya PikaSmart kupitia mpango wa On-Bill Financing, unaomwezesha mteja kupata jiko la umeme na kulipia gharama yake kidogo kidogo kupitia manunuzi ya umeme wa LUKU hadi deni litakapokamilika.

“Gharama za awali zimekuwa mojawapo ya vikwazo vikubwa vya matumizi ya umeme kupikia. Kupitia mpango wa On-Bill Financing, mteja anaweza kuchukua jiko la umeme na kulilipia kidogo kidogo kila anaponunua LUKU,” alisema Mungai.

Aliwahimiza wananchi wa Kagera kutembelea ofisi za TANESCO kwa maelekezo zaidi na kujiunga na mpango huo, akieleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yatasaidia kupunguza ukataji wa miti, kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...