*Ni kiwanda cha vinywaji baridi kilichopo Kibaha mkoa wa Pwani;
*Asifu uwekezaji mkubwa bilioni 28 wa kiwanda hicho, ajira kwa wazawa asilimia 90
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Pwani
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga ameipongeza kampuni ya Simba Beverages Limited kwa uwekezaji wa takribani Sh.bilioni 28 katika sekta ya viwanda na uwekezajo huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uchumi kupitia uzalishaji wa bidhaa nchini.
Ametoa pongezi hizo alipokuwa akizindua kiwanda hicho kilichopo katika eneo la viwanda la Zegereni wilayani Kibaha mkoani Pwani ambapo ameeleza pia Serikali inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kufungua viwanda vipya nchini na kuvutia uwekezaji wa viwanda vipya ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.
“Sekta ya vinywaji baridi ni miongoni mwa sekta muhimu katika kukuza uchumi wa viwanda kutokana na mchango wake katika uzalishaji, ajira na uwekezaji, pamoja na kuunganisha shughuli nyingine za kiuchumi zikiwemo kilimo, usindikaji na usambazaji wa bidhaa.”
Waziri Kapinga amesema maendeleo ya sekta hiyo yanapaswa kwenda sambamba na matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini ili kuongeza thamani ya rasilimali za ndani na kunufaisha wazalishaji wa Kitanzania.
Pia amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, huku akiwataka wawekezaji kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinazingatia sheria, kanuni na viwango vya ubora na usalama.
Awali Ofisa Mkuu wa Fedha Surya Murthy, Afisa Mkuu wa Fedha (CFO) wa Simba Beverages Limited, ametoa Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na viongozi wa Mkoa wa Pwani kwa ushirikiano wao katika kuwezesha uwekezaji huo.
“Uzinduzi wa kiwanda hiki ni hatua muhimu katika kuendeleza shughuli za uzalishaji nchini, kuongeza thamani ya bidhaa na kuimarisha minyororo ya ugavi, huku kampuni ikiendelea kutekeleza dhamira yake kupitia kaulimbiu ya “Imezaliwa Tanzania, Inatumikia Afrika.”
Amefafanua pia Simba Beverages Limited imewekeza katika uzalishaji wa vinywaji baridi vyenye gesi pamoja na vifungashio vya plastiki. Mitambo ya kiwanda hicho ina uwezo wa kuzalisha chupa 12,000 za vinywaji baridi kwa saa.Kampuni inatarajia kuzalisha ajira za moja kwa moja 100 na ajira nyingine 200 zisizo za moja kwa moja kadri shughuli zake zitakavyopanuka.
Aidha zaidi ya asilimia 90 ya malighafi zinazotumika katika kutengeneza bidhaa katika kampuni hiyo zinazopatikana nchini hatua inayochangia kuimarisha mnyororo wa thamani wa uzalishaji wa ndani.
“Kampuni pia inalenga kuongeza mauzo yake hadi Sh bilioni 15.4 ifikapo mwaka 2027 na Sh bilioni 33 ifikapo mwaka 2030, kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa katika uzinduzi huo.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Fadhili Nkurlu, amesema idadi ya viwanda katika Mkoa wa Pwani imeongezeka kutoka viwanda 387 katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi kufikia viwanda 768 kufikia Septemba 2026. Alieleza kuwa viwanda hivyo vinajumuisha viwanda vikubwa 33, vya kati 33, vidogo 248 na vidogo zaidi 454.
Ameongeza viwanda vikubwa na vya kati 38 vilikuwa katika hatua za ujenzi ila sasa vimekamilika, vikiwemo viwanda vikubwa 27 na vya kati 11, huku viwanda vingine 99 vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi na maandalizi.
Pia amesema viwanda 35 vilivyopo katika maeneo ya uwekezaji mkoani humo vimechangia kuzalisha ajira za moja kwa moja 2,357 na ajira nyingine zisizo rasmi 6,062 zinazotokana na shughuli za kiuchumi zinazohusiana na viwanda hivyo.
“Mkoa wa Pwani unaendelea kuweka kipaumbele katika kuvutia uwekezaji wa viwanda vipya, kuongeza ajira kwa vijana, kuhamasisha matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini na kusimamia ubora na usalama wa bidhaa zinazozalishwa.”
Pia amesema kwa mujibu wa takwimu ya mwaka 2021 hadi 2022 viwanda 1387 vimejengwa na kufikia Septemba 2026 vimejengwa viwanda 1768.Viwanda 99 vingine vinajengwa na kwamba Mkoa wa Pwani lenye ukubwa wa Hekta 148000 likiwa na kongani 35.
Wakati huo huo Mkurugenzi wa TanTrade, Ephraim Mafuru amesema uwekezaji uliofanywa na Simba Beverages ni mchango mkubwa wa Pato la Taifa huku akitoa mwito kwa wawekezaji ili waweze kutambulika watumie nembo ya uzalishaji ya Tanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera, Utafiti na utetezi wa TPSF Mwanahamis Hussein alipongeza hatua hiyo ya uwekezaji kwa sababu imeongeza soko la ajira na kuleta ushindani wa kiuchumi.Pia ameupongeza Mkoa wa Pwani kwa kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.



.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...