
MBIO za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zimezindua rasmi msimu wake wa 25 (Silver Jubilee) katika hafla iliyojaa hamasa kubwa iliyofanyika katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, ikiweka msingi wa wikendi ya kihistoria ya mbio mjini Moshi mnamo Februari7, 2027.
Akizungumza KAtika hafla hiyo, Waziri Mkuu mstaafu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, alipongeza mbio hizo kwa kufikia hatua hiyo kubwa ya robo karne ya ubora na mchango wake mkubwa katika kuhamasisha utamaduni wa michezo na utalii wa michezo.
"Kufikisha miaka 25 ni mafanikio ya kipekee yanayoonyesha udhibiti, maono, na ushirikiano bora na Serikali ya Tanzania," alisema Mhe. Majaliwa.
Alibainisha kuwa Kilimanjaro Marathon mara zote imekuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya wanasayansi na wanariadha wa ndani.
Pia alizipa changamoto mbio nyingine nchini kote kuiga mfano huu wa kipekee, kwani lengo linapaswa kuwa kukuza mabingwa wengi zaidi wa Kitanzania katika miaka 25 ijayo.
Mhe. Majaliwa alisisitiza kuwa mbio hizi zina faida kubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania huku akiongeza kuwa ndio tukio kuu la michezo la kimataifa nchini Tanzania.
"Inapokusanya zaidi ya washiriki 13,200 na idadi sawa ya watazamaji kutoka zaidi ya nchi 60, mbio hizi zinakuwa chachu kubwa kwa sekta ya ukarimu, usafirishaji, na biashara ndogondogo mjini Moshi na maeneo ya jirani," alisema.
Aliwahimiza washiriki na wageni watakaohudhuria msimu huu wa miaka 25 kutumia fursa hiyo kutembelea vivutio vikuu vya utalii vya Tanzania, ikiwa ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Bonde la Ngorongoro na Zanzibar.
Mhe. Majaliwa pia alitoa shukrani za dhati kwa wadhamini wote: mdhamini mkuu Kilimanjaro Premium Lager (Mbio za Km 42), YAS (Mbio za Nusu Marathon Km 21), na CRDB Bank (Mbio za kujifurahisha za Km 5); wadhamini rasmi wasaidizi: Coral Paints, Kilimanjaro Natural Mineral Water, na TPC Sugar; washirika rasmi GardaWorld Security, Toyota Tanzania, Columbia Sportswear, Simba Cement, ALAF Limited, Salinero Hotel - Kilimanjaro, na Harleys Deep Heat and Deep Freeze; pamoja na wasambazaji rasmi Kibo Palace Hotel Arusha na Keys Hotel Moshi.
Mwakilishi wa Kilimanjaro Premium Lager) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania, Bi. Khensani Mkhombo, alieleza kujivunia kwa kampuni hiyo kushirikiana na mbio hizo kwa miaka 25—moja ya udhamini mrefu na wenye mafanikio makubwa zaidi wa michezo wa makampuni nchini Tanzania.
"Kwa miaka 25 ya ajabu, Kilimanjaro Premium Lager imesimama bega kwa bega na tukio hili la kiwango cha kimataifa kusherehekea utamaduni wa Kitanzania, michezo, na roho ya jamii iliyo hai," alisema.
"Ili kusherehekea hatua hii ya robo karne, wanariadha na wageni watarajie wikendi isiyosahaulika iliyojaa matukio ya kusisimua, huduma za ukarimu, na sherehe mjini Moshi.
Tunawasihi washiriki kujisajili mapema kupitia www.kilimanjaromarathon.com au Mixx BY YAS pindi lango la usajili litakapofunguliwa, kwani nafasi za ushiriki ni chache."
Mwakilishi wa Kampuni ya YAS, Woinde Shisael, alithibitisha tena azma ya YAS ya kuendelea kuwezesha mbio hizo na kuwasihi watu wengi zaidi kujiunga na mbio za mwaka huu.
"Kwa miaka 25, Kilimanjaro Marathon imeunganisha wanariadha, familia, jamii, na dunia kupitia Tanzania. Kama Mdhamini Rasmi wa Nusu Marathon, tunajivunia kuwezesha viunganishi hivi kupitia Mtandao wetu wa 4G na 5G Ya Viwango, tukisaidia watu wengi zaidi kushiriki katika uzoefu huu wa kipekee huku tukisaidia jamii zenye afya bora, kuwezesha vijana, na kuhamasisha nia inayoisukuma Tanzania mbele.
"Tunawaalika washiriki wote kutoka nnadi na nje ya mipaka ya Tanzania kujiunga nasi mjini Moshi kwa sherehe za kihistoria za miaka 25."
Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam wa CRDB Bank, Bw. Muhumuliza Buberwa, alisema CRDB Bank inajivunia kuendeleza ushirikiano wake na tukio hili kama mdhamini rasmi wa Mbio za kujifurahisha za Km 5 (Fun Run).
“Mbio za Km 5 zinahusisha watu mbalimbali – familia, vijana, na wakimbiaji wa mara ya kwanza – kuwa sehemu ya hadithi hii ya kipekee ya Kitanzania.
" Tunawapongeza Kilimanjaro Premium Lager na washirika wote kwa hatua hii kubwa.”
Waandaaji, Kilimanjaro Marathon Company Limited, wamethibitisha kuwa usajili katika kategoria zote za mbio utafuata mfumo wa atayeanza kufika ndiye atakayehudumiwa kwanza (first-come, first-served).
Mara tu idadi inayotakiwa itakapofikiwa, usajili utafungwa mara moja.
Wanariadha wanahimizwa kujisajili mapema ili kujihakikishia nafasi na kuepuka kutoridhika.
Mbio za 25 za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon, zikiwa na kaulimbiu ya “Mbio ya Watu”, zitafanyika Jumapili, 7 Februari 2027, zikianzia katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).
Tukio hili limeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited, huku usafiri wa wageni wa kimataifa na masoko ya kimataifa yakiendelea kuratibiwa na Wild Frontiers Events.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...