Waziri wa Madini Anthony Mavunde akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kiwanda cha Geofields kilichonzishwa na wazawa kwa ajili ya huduma migodini ya Wire Mesh.
Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Geofields Tanzania Limited, Denis Dillip akitoa maelezo kuhusiana kiwanda hicho kinachomilikiwa na watanzania kwa asilimia 100 kuwa sera za nchi zimewezesha wazawa kuwa sehemu ya kutoa huduma katika sekta ya madini.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo akizungumza kuhusiana na umhimu wa kiwanda Geofields katika kunufaika na ajira kwa kwa watanzania wakiwemo wananchi wa Bagamoyo.Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Masoko was Chama cha Watoa Huduma Migodini (TAMISA) Dkt Sebastian Ndege akitoa maelezo kuhusiana matokeo ya wazawa kuanzisha kiwanda cha kutoa huduma migodini.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde akizungumza katika uzinduzi wa Kiwanda cha Geofields kilichonzishwa na wazawa kwa ajili ya huduma migodini ya Wire Mesh.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TAMISA Japhet Mussa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na fursa ya watanzania kuwa na nguvu ya kutoa huduma migodini.
*Geofields yazindua kiwanda cha Wire Mesh mgodini
Na Mwandishi Wetu Pwani
WAZIRI wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amefungua rasmi kiwanda cha Geofields Tanzania Limited cha kuzalisha bidhaa za Wire Mesh zinazotumika katika shughuli za uchimbaji madini, kilichopo Kerege, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, chenye uwezo wa kuzalisha vipande zaidi ya 100,000 kwa mwaka.
Uzinduzi wa kiwanda hicho uliofanyika Oktoba 17, 2026, unaashiria hatua muhimu katika kukuza uzalishaji wa ndani wa vifaa vinavyotumika migodini, kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi na kuongeza ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
Kiwanda hicho kinaendeshwa na Geofields Tanzania Limited kupitia kitengo chake cha Geofields Underground Support (GUS), kinachojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa vifaa vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji chini ya ardhi migodini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Geofields Tanzania Limited, Denis Dillip, amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kukidhi mahitaji ya migodi nchini, huku kampuni ikiendelea kuweka mikakati ya kupanua uzalishaji na kuongeza ushindani katika masoko ya Afrika Mashariki na kimataifa.
Dillip amesema kampuni hiyo tayari imefungua tawi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hatua inayolenga kupanua wigo wa biashara na kuongeza nafasi ya kampuni katika soko la kikanda.
Ameeleza kuwa kampuni imewekeza katika teknolojia na utaalamu ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango vya kimataifana na hasa katika kulinda usalama na maisha ya wafanyakazi chini ya migodi. Aidha, amesema uwepo wa wataalamu wenye mafunzo kutoka Australia na China unalenga kuimarisha ujuzi, teknolojia na uwezo wa juu wa uzalishaji wa kampuni.
Aidha, Dillip ameishukuru Serikali, hususani Wizara na Tume ya Madini kwa kuweka sera nzuri za maudhui ya ndani (Local Content), akieleza kuwa sera hizo zimekuwa chachu ya uwekezaji na kuimarisha ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
Amesema hatua hiyo muhimu pia imechangiwa na ushirikiano kati ya Geofields Tanzania Limited na kampuni yake mbia ya African Underground Mining Services (AUMS), pamoja na washirika wake wa Australia, kampuni za Perenti na Barminco. Aidha, ameishukuru Geita Gold Mine (GGM) kuwa miongoni mwa wadau wakubwa watumiaji wa bidhaa zetu na kushirikiana nasi kuhakisha kuwa tunafikia dhumuni la serikali la sera ya maudhui ya ndani na ushirikiswaji wa watanzania katika shughuli za migodi.
Ameeleza kuwa ushirikiano huo una mchango muhimu katika kuendeleza uzalishaji wa ndani, kuhamisha teknolojia na utaalamu, pamoja na kuhakikisha utekelezaji wa sera ya maudhui ya ndani unazingatia viwango vya kimataifa.
Katika suala la ajira, Geofields Tanzania Limited ina jumla ya wafanyakazi 105 ina mpango wa kuongeza nafasi zaidi za ajira kwa Watanzania kadri shughuli za uzalishaji zitakavyoendelea kupanuka. Hatua hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta ya viwanda, kukuza ujuzi wa kitaalamu na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia fursa zinazotokana na uwekezaji huo.
Akizindua kiwanda hicho, Waziri wa Madini Mh, Mavunde amepongeza uwekezaji huo na kueleza dhamira ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na utengenezaji wa vifaa vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji madini barani Afrika.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani ili kuongeza uwezo wa kampuni za Kitanzania kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya migodi nchini na katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono na maelekezo yaliyochangia kuimarisha sekta ya madini na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.
Pia, Waziri Mavunde amewahimiza Watanzania kuunganisha mitaji na nguvu za kibiashara ili kutumia fursa zinazopatikana katika mnyororo wa manunuzi wa sekta ya madini. Amebainisha kuwa takribani shilingi trilioni 5.1 zinahusishwa na mnyororo huo, huku sehemu kubwa ya shughuli hizo ikitajwa kujikita katika kampuni zisizozidi sita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanislaus Nyongo, amesema mkoa huo una viwanda vikubwa na vidogo 1,768, akieleza kuwa uwekezaji wa Geofields unaongeza mchango wa mkoa katika kukuza sekta ya viwanda nchini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amesisitiza umuhimu wa kampuni hiyo kutoa kipaumbele kwa wakazi wa Kerege katika fursa za ajira zitakazotokana na uwekezaji huo.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janeth Reuben Lekashingo, amesema mafanikio ya sekta ya madini yanapaswa kupimwa pia kwa ukuaji wa kampuni za Kitanzania, ajira zinazozalishwa, viwanda vinavyoanzishwa, uhamishaji wa teknolojia na ongezeko la uzalishaji wa ndani.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...