Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo MWASHITA SACCOS kimefanya uchaguzi wa viongozi wapya wa bodi katika Mkutano Mkuu wa 29 uliofanyika jijini Dodoma, huku uongozi mpya ukilenga kuongeza idadi ya wanachama, hususan vijana, ili kuimarisha maendeleo ya chama hicho.
Makamu Mwenyekiti mpya wa MWASHITA SACCOS, Paul Mwanga, amesema kuongeza wanachama vijana ni miongoni mwa vipaumbele vya uongozi mpya, akieleza kuwa vijana wana nafasi muhimu katika kuendeleza shughuli za ushirika na kuwa viongozi wa baadaye.
Mwanga amesema uongozi mpya utaendeleza juhudi zilizofanywa na bodi iliyopita, ambazo kwa kushirikiana na wafanyakazi zimechangia kutatua baadhi ya changamoto za muda mrefu za chama hicho, ikiwemo changamoto ya hasara.
Amesema MWASHITA SACCOS imepata faida kwa mara ya pili, hatua ambayo inaonesha maendeleo yaliyofikiwa na juhudi zilizofanywa na uongozi uliopita, ameahidi kuwa bodi mpya itaendeleza mafanikio hayo kwa kushirikiana na menejimenti pamoja na wanachama.
Mwanga ameongeza kuwa uongozi mpya utazingatia misingi ya demokrasia kwa kusikiliza maoni na mahitaji ya wanachama, huku ukitekeleza mpango mkakati mpya uliopitishwa katika mkutano huo kwa lengo la kufikia malengo ya chama.
Kwa upande wake, Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dodoma, Joseph Chitinka, amewahimiza vijana kujiunga na vyama vya ushirika vya akiba na mikopo, akieleza kuwa ni fursa ya kupata mitaji ya kuanzisha biashara, kuweka akiba na kuwekeza kwa ajili ya maendeleo yao ya kiuchumi.
Chitinka amesema elimu ya ushirika inapaswa kuimarishwa kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuoni ili kuwajengea vijana uelewa kuhusu umuhimu wa kuweka akiba, kununua hisa na kutumia mikopo kwa malengo yenye tija. Amesema Mkoa wa Dodoma umeanzisha klabu za ushirika kwenye baadhi ya shule tangu mwaka uliopita.
Aidha, Chitinka amesema MWASHITA SACCOS imeendelea na mipango ya uwekezaji, ikiwemo ujenzi wa jengo la zaidi ya ghorofa tano litakalokuwa sehemu ya uwekezaji wa chama hicho. Ameeleza kuwa wanachama wamechangia mpango huo kupitia ununuzi wa hisa, ambapo ushiriki wao ni muhimu katika kuimarisha mtaji wa chama.
Naye Kaimu Meneja wa MWASHITA SACCOS, Yasinta Justine Semwenda, amesema menejimenti itaendelea kushirikiana na viongozi wapya wa bodi katika kutekeleza maamuzi ya mkutano mkuu na mipango ya chama, huku ikiendelea kutimiza majukumu yake kwa kushirikiana na wanachama ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo MWASHITA SACCOS kimepitisha bajeti ya shilingi milioni 425.378 kwa mwaka ujao wa fedha, ikilinganishwa na bajeti ya shilingi milioni 335.445 ya mwaka uliopita, hatua inayoonesha ongezeko la mipango ya kifedha ya chama hicho.
Aidha, katika uchaguzi huo Eustard Athanas Ngatale ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya Mwashita SACCOS, Paul Mwanga, Makamu Mwenyekiti,Spacioza Joseph, Peter shirima, Anna Mulugu,Joseph Mashenene na Daniel kitua, wamechaguliwa kuwa wajumbe wa Bodi ya MWASHITA SACCOS.




.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...