MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Deogratius Ndejembi, amesema Bahari ya Hindi ya Magharibi ina thamani ya zaidi ya dola bilioni 300 na kuzalisha takribani dola bilioni 20.8 kwa mwaka.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutumia fursa hizo kuchochea uchumi na ajira huku ukilinda mazingira ya bahari na pwani.
Dkt. Ndejembi amesema hayo leo, Oktoba 8, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12).
Amesema huduma za mifumo ya ikolojia ya bahari hiyo zina thamani ya takribani dola bilioni 25 kwa mwaka, huku utalii ukichangia zaidi ya asilimia 70 ya bidhaa hiyo ya kiuchumi.
Amesema zaidi ya watu milioni 65 katika ukanda wa Bahari ya Hindi ya Magharibi wanategemea moja kwa moja bahari kwa chakula na maisha, akisisitiza kuwa afya ya mifumo ya ikolojia ni msingi wa ustawi wa kiuchumi wa jamii hizo.
Kwa mujibu wa Dkt. Ndejembi, ukanda huo una zaidi ya asilimia 30 ya miamba muhimu ya matumbawe, mikoko na nyasi bahari duniani, huku Tanzania ikiwa na zaidi ya hekta 158,000 za mikoko zinazosaidia kuzalisha mazalia ya samaki, kulinda maeneo ya pwani na kuchuja uchafuzi.
Amesema Tanzania imekuwa ikichukua hatua za kuhifadhi rasilimali hizo, ikiwemo kurejesha zaidi ya hekta 3,000 za mikoko katika kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya Mkataba wa Nairobi.
Ameonya kuwa fursa hizo ziko hatarini kutokana na mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi, uvuvi haramu na usio endelevu, upotevu wa makazi ya viumbe na maendeleo yasiyopangwa, hali inayohitaji ushirikiano wa nchi za ukanda huo.
Amesema Tanzania itaendelea kusimamia uwiano kati ya uhifadhi na maendeleo kupitia mipango kama upangaji wa matumizi ya maeneo ya bahari, maeneo tengefu ya baharini, uvuvi endelevu, biashara ya kaboni, ufugaji wa viumbe vya baharini, utalii na usafiri wa majini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sekretarieti ya Mkataba wa Nairobi, Dkt. Jared Bosire, amesema Tanzania pia imeandaa Jukwaa la Biashara, Tukio la Vijana, matukio ya pembeni zaidi ya 50 pamoja na maonyesho, huku kukiwa na tukio la wanawake katika uchumi wa buluu na Majadiliano ya Kiwaziri.
Alisema kiwango hicho cha maandalizi kimeifanya Tanzania kufanya COP12 kwa ukubwa na ubora wa hali ya juu, hali ambayo imeweka changamoto kwa nchi itakayokuwa mwenyeji wa Mkutano wa 13 wa Nchi Wanachama wa Mkataba huo.
“Tanzania imefanya kweli, imefanya kwa ukubwa na kwa ubora wa hali ya juu, na kuweka rekodi ambazo zitakuwa changamoto kwa COPs zote zijazo. Rais ajaye wa Kamati ya Mkataba atakayeandaa COP ya 13 atakuwa na kazi kubwa sana ya kufanya,” alisema Bosire.




.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...