Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ametoa kipindi cha mwezi mmoja kwa mkandarasi anayetekeleza miradi mitano ya maendeleo chini ya Programu ya TACTIC yenye thamani ya Sh bilioni 19.83, kukamilisha angalau mradi mmoja na kuutaka kuongeza kasi ya kazi ili kukamilisha miradi yote kwa wakati.

Nyongo amemtaka mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa kuzingatia masharti ya mkataba yanayotaka kazi hizo kukamilika Februari 2027.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika Manispaa ya Kibaha, Nyongo amesema Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha kazi wakati vifaa vya ujenzi vinapatikana.

Amesema ifikapo Novemba 22, mwaka huu, atarejea kukagua maendeleo ya utekelezaji na kujiridhisha iwapo mkandarasi ametekeleza agizo la kukamilisha angalau mradi mmoja ndani ya mwezi mmoja.

“Jumla ya utekelezaji wa miradi hadi sasa nimeambiwa ni asilimia 45, serikali imeshafanya sehemu yake, vifaa vipo, mnachelewa kwa sababu gani, mkandarasi? Wakati mwingine mnabana fedha,tengenezeni mpango kazi, msifanye ubahili unaochelewesha kazi,” amesisitiza Nyongo.

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi huo, Mhandisi Shaban Kaswaka, ameahidi kukamilisha angalau mradi mmoja ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kama alivyoelekezwa na Mkuu wa Mkoa.

Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa Soko la Kisasa la Mnarani (Loliondo), barabara ya Picha ya Ndege–Hospitali ya Lulanzi–NDC yenye urefu wa kilomita 3.7 kwa kiwango cha lami, barabara ya TUGHE–Anglican kwa kiwango cha lami, bustani ya burudani na mapumziko, pamoja na jengo la usimamizi na uratibu wa mradi.

Katika ziara hiyo, Nyongo pia alikagua mradi wa maji unaohusisha ujenzi wa kituo cha pampu na tanki katika Kata ya Sofu, wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 8.

Amesema Mkoa utaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika na kusaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya Pangani, Lulanzi na Muheza.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...