Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ameitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kujitathmini na kuongeza kasi ya kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ya uwekezaji wa viwanda, akisisitiza kuwa kipaumbele kisielekezwe katika barabara za vijijini pekee.
Nyongo ametoa agizo hilo Oktoba 22, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kongani ya Viwanda ya King Lion, iliyopo Kibaha, kwa lengo la kufuatilia maendeleo ya uwekezaji na kusikiliza changamoto zinazowakabili wawekezaji.
Amesema Mkoa umelichukua suala la ubovu wa barabara yenye urefu wa kilomita mbili inayoelekea katika kongani hiyo, ambayo imekuwa kero kwa muda mrefu, akieleza kuwa barabara zinazoelekea kwenye maeneo ya viwanda zinapaswa kupewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake katika shughuli za uzalishaji na usafirishaji.
“Barabara hizi zinazoelekea kwenye viwanda ni maalumu, lazima zitazamwe kwa jicho la kipekee, TARURA mnapaswa kujitathmini na kuchukua hatua kukabiliana na changamoto za barabara katika maeneo haya,” amesema Nyongo.
Kuhusu changamoto ya umeme, Nyongo amesema Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lipo katika hatua za kukamilisha juhudi za kutatua changamoto ya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya uwekezaji.
Awali, Meneja Mkuu wa Uendeshaji wa kinglion, Jerry Chow, amesema ubovu wa miundombinu ya barabara na ukosefu wa umeme wa uhakika ni miongoni mwa changamoto kuu zinazoathiri mazingira ya uwekezaji katika eneo hilo.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...