Na Oscar Assenga, TANGA

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tanga unatarajia kufanya ukarabati wa madaraja ya Hale na Maguzoni yaliyopo katika barabara kuu ya Tanga–Segera, kwa lengo la kuimarisha usalama na kulinda miundombinu hiyo dhidi ya athari za mvua kubwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya wataalamu wa TANROADS kufanya ukaguzi wa barabara na madaraja mkoani humo kufuatia taarifa za uwepo wa mvua nyingi za El Niño nchini, ambapo walibaini changamoto zinazohitaji kushughulikiwa katika madaraja hayo.

Akizungumzia hatua hiyo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama K Msama alisema ukarabati huo utahusisha maeneo ya chini ya madaraja yanayopitisha maji pamoja na vyuma vilivyopo katika sehemu za juu za madaraja ambavyo vimeathiriwa na kutu.

Alisema wamebaini kuwa maji ya mvua yanapita katika baadhi ya maeneo ya madaraja na kusababisha vyuma kupata kutu na kuharibika, hali inayohitaji hatua za haraka ili kuzuia uharibifu zaidi na kuhakikisha madaraja yanaendelea kutekeleza majukumu yake.



Alisema ukarabati huo unalenga kuimarisha uimara wa madaraja hayo na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara, wakiwemo wasafiri na wasafirishaji wanaotumia njia hiyo muhimu.

Alifafanua kuwa ili kuruhusu kazi hiyo kufanyika kwa ufanisi na kwa muda uliopangwa, barabara ya Tanga–Segera itafungwa kwa muda wa saa nne, kuanzia asubuhi hadi saa sita mchana, Jumanne, Oktoba 20.

Alisema TANROADS imejipanga kuhakikisha mitambo na vifaa vinavyohitajika vinafika eneo la kazi ili ukarabati ukamilike ndani ya muda uliopangwa na kuruhusu magari kuendelea na safari zake.


Meneja huyo aliwataka wasafiri na wasafirishaji kupanga safari zao mapema kwa kuzingatia muda wa kufungwa kwa barabara hiyo ili kupunguza usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa kazi hizo.

Barabara ya Tanga–Segera ni kiunganishi muhimu cha usafiri na usafirishaji, inayohudumia magari yanayotoka Dar es Salaam kupitia Chalinze kuelekea Segera na kuendelea Tanga, pamoja na magari yanayotoka mikoa ya Singida, Arusha na Kilimanjaro.


Aidha, barabara hiyo hutumiwa na magari yanayohudumia shughuli za Bandari ya Tanga pamoja na usafirishaji unaotoka eneo la Horohoro mpakani mwa Tanzania na Kenya.

Kosani alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha madaraja na barabara vinaendelea kuwa salama kwa matumizi ya wananchi na wadau wa usafirishaji.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...