Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

VIJANA nchini wametakiwa kutumia fursa zinazopatikana katika sekta za elimu, fedha, uwekezaji, biashara na utamaduni, huku wakitumia teknolojia ya kisasa kujiletea maendeleo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Wito huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wafanyabiashara Wanawake Afrika Mashariki (EAWiBP), Janice Benson Kimaro, wakati wa uzinduzi wa TAWEN Youth Dar es Salaam, tawi la vijana la Mtandao wa Uwezeshaji Wanawake Tanzania (TAWEN), uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Janice amesema uzinduzi huo unaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inayosisitiza upatikanaji wa fursa sawa kwa wote, akibainisha kuwa vijana wanapaswa kuwa washiriki hai wa maendeleo kupitia ubunifu, uongozi na utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

“Tunaposema fursa sawa kwa vijana wetu, tunamaanisha kujenga mazingira ambayo kila kijana anapata nafasi ya kujifunza, kukuza kipaji chake, kuanzisha biashara na kupata ujuzi,” amesema.

Amewataka vijana kutambua na kuendeleza vipaji vyao badala ya kutegemea elimu ya darasani pekee, huku akiwahimiza kujifunza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ili kufahamu fursa zilizopo na namna ya kuzitumia.

Aidha, amesema ukuaji wa teknolojia, ikiwemo Akili Unde (AI), umefungua fursa nyingi kwa vijana, hivyo wanapaswa kutumia ujuzi wao wa teknolojia kupata taarifa sahihi, kutafuta fursa na kuunganishwa na watu na taasisi zinazoweza kuwasaidia kufikia malengo yao.

“Vijana mko vizuri sana katika mambo ya teknolojia. Tumieni elimu hiyo kutazama maudhui muhimu na kutambua mitandao inayowaunganisha na fursa. TAWEN Youth itoe semina kwa vijana ili kuwaonesha fursa muhimu zilizopo,” amesema.

Amesisitiza kuwa uzinduzi wa TAWEN Youth unapaswa kuwa mwanzo wa utekelezaji wa mipango yenye matokeo yanayopimika, badala ya kuishia katika kuandika malengo bila kuyafanyia kazi.

Amesema ni muhimu kwa viongozi wa jukwaa hilo kuweka utaratibu wa kutathmini utekelezaji wa mipango yao baada ya muda maalumu ili kubaini mafanikio na maeneo yanayohitaji maboresho.

Kuhusu soko la Afrika Mashariki na Soko Huru la Afrika, Janice amewataka vijana kujifunza kwa kina kuhusu fursa za masoko hayo ili waweze kuzitumia kukuza biashara, uwekezaji na shughuli nyingine za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAWEN Taifa, Balozi Amina Salum Ally, amesema TAWEN Youth itakuwa jukwaa muhimu la kuendeleza falsafa ya vijana na kuwahamasisha kujitolea kushiriki katika shughuli za maendeleo ya taifa.

Naye Mwenyekiti wa TAWEN Youth Dar es Salaam, Tarik Ninga, amesema jukwaa hilo limeanzishwa kwa lengo la kuwawezesha vijana katika uongozi, stadi za maisha na ujasiriamali.

Amesema pia litawaunganisha vijana na fursa za elimu, ajira, uwekezaji, masoko na mitandao ya kibiashara, huku likihamasisha ubunifu katika matumizi ya teknolojia kama nyenzo ya maendeleo na upatikanaji wa ajira.

Malengo mengine ya jukwaa hilo ni kuimarisha ushiriki wa vijana katika uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati jadidifu, kukuza mchango wao katika utafiti, pamoja na kuandaa mijadala, midahalo na mafunzo ya mara kwa mara.

Ninga amesema TAWEN Youth pia inalenga kuwaunganisha vijana na taasisi zinazoweza kuwapatia fursa, mitaji na ushauri utakaowawezesha kutekeleza mawazo yao na kujenga msingi imara wa kujitegemea kiuchumi.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...