MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewataka viongozi wa vijiji vinavyozunguka mradi wa umeme wa upepo katika Kijiji cha Usokami, Wilaya ya Mufindi, kuhamasisha wananchi kushiriki katika kulinda miundombinu ya mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 3.9, huku akiwahimiza kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme kuimarisha shughuli za kiuchumi na kujikwamua kimaisha
Akizungumza wakati wa kutembelea mradi huo katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano ya kutembelea viwanda mkoani Iringa, James amesema uwekezaji huo una manufaa makubwa kwa jamii, ikizingatiwa kuwa unawanufaisha wananchi zaidi ya 9,000 kutoka vijiji 32 katika kata sita za Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi. Amesema ni muhimu wananchi kuutunza mradi huo ili uendelee kutoa huduma ya umeme na kuchochea shughuli za uzalishaji, biashara na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya Mwenge Hydro Power Ltd, Deogratius Massawe, amesema kampuni hiyo inayotekeleza mradi huo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme ya uhakika na kwa gharama nafuu, ili kuongeza fursa za kiuchumi, kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara, pamoja na kuchochea maendeleo ya jamii zinazozunguka mradi huo.
Naye Michael Mahenge, akizungumza kwa niaba ya wananchi wanufaika, amesema mradi huo umeleta mabadiliko chanya katika maisha yao kwa kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo hapo awali zilikuwa ngumu kutekelezwa kutokana na changamoto ya upatikanaji wa umeme.
Amesema uwepo wa umeme huo umewawezesha wananchi kuanza kufanya shughuli ndogo ndogo za uzalishaji ndani ya kijiji hicho, ikiwemo kusaga mahindi, hali inayorahisisha upatikanaji wa huduma, kupunguza usumbufu na kufungua fursa za kuongeza kipato kwa wananchi.
Uwekezaji huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 50 unaonesha umuhimu wa mazingira bora na wezeshi yaliyowekwa na Serikali katika kuvutia uwekezaji, kukuza sekta ya nishati na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Mradi huo unatarajiwa kuendelea kuwa kichocheo cha maendeleo kwa wananchi wa Mufindi kupitia upatikanaji wa nishati ya umeme na kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...