BALOZI wa Tanzania nchini Zimbabwe, Kamishna wa Polisi (CP) Suzan Kaganda, ameongoza harambee ya kuchangia ukarabati wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Magharibi Kati, Jimbo la Mashariki, Usharika wa Ndala, wilayani Nzega, mkoani Tabora, huku akisisitiza umuhimu wa malezi bora kwa watoto na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Harambee hiyo imefanyika Oktoba 26, 2026, katika kanisa hilo lililopo Kata ya Ndala, ikiwa na lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa kanisa, ikiwemo uwekaji wa paa jipya na kuboresha mazingira ya ndani na nje ya nyumba hiyo ya ibada.
Akizungumza katika harambee hiyo, CP Kaganda amesisitiza kuwa jamii ina wajibu wa kuwalea watoto katika misingi bora ya dini na maadili, pamoja na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili, hususan ukatili wa kijinsia, ili kujenga jamii yenye maadili mema na inayoheshimu haki za kila mmoja.
Aidha, ameitaka jamii kumrudia Mungu, kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa hekima na uadilifu katika kuwaletea wananchi maendeleo na ustawi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ambaye pia ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tabora, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Peter Magayane, amewataka wazazi na walezi kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za haraka kwa mamlaka husika kuhusu matukio ya ukatili wa kijinsia ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Katika harambee hiyo, CP Kaganda amechangia kiasi cha fedha kilichosaidia kufikisha zaidi ya shilingi milioni 70 zilizochangwa kwa ajili ya shughuli hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Askofu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Magharibi Kati, Mchungaji Patrick Katembo ametoa shukrani kwa CP Kaganda na washiriki wote wa harambee hiyo kwa mchango wao, huku akiahidi kuwa kanisa litaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani, kuzuia uhalifu na kujenga jamii yenye maadili mema.












Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...