
Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) inatarajia kuwakutanisha Wahasibu, Wakaguzi na wadau mbalimbali wa Taaluma ya Uhasibu katika Mkutano Mkuu wa 39 wa Wahasibu 2026 utakaofanyika Novemba 24 hadi 27, 2026, jijini Dar es Salaam, kujadili mchango wa Taaluma ya Uhasibu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Sylvia Temu amesema mkutano huo utajumuisha shughuli za kijamii na kitaaluma, ambapo Novemba 24, Bodi hiyo itakabidhi vifaa tiba kwa Hospitali ya Mwananyamala na Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Watoto ya CCBRT jijini Dar es Salaam.
Amesema vifaa hivyo vimenunuliwa kupitia michango ya wahasibu mbalimbali waliojitokeza kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya nchini, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mchango wa wataalamu hao katika kusaidia jamii.
Amesema mkutano rasmi utaanza Novemba 25 na kufunguliwa na Waziri wa Fedha, Balozi Hamisi Mussa Omar, huku mada kuu ikijikita katika mchango wa Wahasibu na Wakaguzi wa hesabu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ameeleza kuwa dira hiyo inalenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja za Marekani ifikapo mwaka 2050, huku pato la mtu mmoja mmoja likitarajiwa kufikia angalau dola 7,000. Pia inalenga kuimarisha elimu na uelewa wa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kuongeza uwezo wa wananchi kutumia na kuendeleza teknolojia katika shughuli za maendeleo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, siku ya pili ya mkutano, Novemba 26, itajadili masuala mbalimbali ya kitaaluma pamoja na afya ya mwili na akili, uwiano kati ya kazi na maisha binafsi na umuhimu wa wataalamu kutenga muda kwa ajili ya familia zao. Washiriki pia watapata fursa ya kushiriki michezo mbalimbali na kupata elimu ya afya kutoka kwa wataalamu.
Pia jioni ya tarehe 26 Novemba kutakuwa na hafla ya utoaji Tuzo kwa Taasisi za Umma, kampuni binafsi na Taasisi zisizo za kiserikali zilizofanya vizuri katika kuandaa taarifa bora za hesabu. Hafla hiyo itafanyika katika ukumbi wa mkutano wa APC Bunju jijini Dar es Salaam.
Amesema mchakato wa kupata washindi wa Tuzo hizo una ushindani mkubwa na unazingatia usiri, huku tathmini ikifanywa na wataalamu huru wenye ujuzi na uzoefu katika Taaluma ya Uhasibu na uandaaji wa taarifa za hesabu.
Ameongeza kuwa majina ya washindi yataendelea kuwa siri hadi wakati wa kutangazwa, akizihimiza Taasisi zote zilizoshiriki kuhudhuria hafla hiyo ili kushuhudia kutangazwa kwa washindi.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa la kujadili mustakabali wa Taaluma ya Uhasibu nchini, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mchango wa Wahasibu na Wakaguzi wa hesabu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NBAA CPA Prof. Sylvia Temu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano mkuu wa 39 wa mwaka wa Wahasibu 2026 utakaofanyika katika ukumbi wa mkutano wa APC Bunju jijini Dar es Salaam.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...