Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imewezesha kuokolewa na kurejeshwa kwa Dola za Marekani milioni 3.3, sawa na Sh bilioni 8.86, katika fungu la ugawanaji wa mapato kupitia ukaguzi wa gharama na mapato ya kampuni zinazojihusisha na shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Akizungumza jana wakati akiwasilisha taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya PURA kwa mwaka wa fedha 2025/26, katika kikao na wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Charles Sangweni, alisema jumla ya Dola za Marekani 3,306,678, sawa na Sh8,861,897,040, ziliokolewa kupitia ukaguzi huo.

Alisema PURA ilikamilisha ukaguzi wa gharama na mapato katika Kitalu cha Songo Songo kwa miaka ya 2023 na 2024, Vitalu Na. 1 na 4 kwa miaka ya 2023 na 2024, pamoja na Kitalu cha Ruvuma kwa mwaka 2024.

Aidha, alisema mamlaka hiyo ilianza ukaguzi katika Kitalu cha Songo Songo kwa mwaka 2025 na Kitalu Na. 2 kwa mwaka 2023.

Katika kuimarisha usimamizi wa taarifa za kifedha, Sangweni alisema PURA imekamilisha uandaaji wa mfumo wa kuhifadhi kumbukumbu za hesabu za gharama na mapato ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini, unaojulikana kama PURA Cost Recovery Management System (CRMS).

Alisema mfumo huo umerahisisha uwasilishaji na uhifadhi wa taarifa za mapato na gharama kutoka kwa kampuni zinazojihusisha na shughuli za mkondo wa juu wa petroli nchini.

Katika hatua nyingine, alisema thamani ya bidhaa na huduma zilizotolewa na kampuni za ndani katika miradi ya mkondo wa juu wa petroli mwaka 2026 ilikuwa zaidi ya Dola za Marekani milioni 30, ikilinganishwa na Dola milioni 14 mwaka 2025.

Aidha, PURA iliendelea kusimamia na kuhakikisha kampuni zinazofanya shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini zinatekeleza programu na miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR), ikiwemo ujenzi wa Shule ya Msingi Likong’o katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, ujenzi wa majiko ya kisasa ya kupikia kwa kutumia nishati ya LPG katika shule nne zilizopo Kata ya Msimbati, Mtwara, na ufadhili wa vijana kusoma masuala ya ufundi katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mkoani Lindi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...