Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, akifafanua kitabu kilichozinduliwa jijini Dar es Salaam Novemba 15, 2026 kwaajili ya kuwasaidia wanawake Watakaojifungua watoto njiti.

Na Avila Kakingo, Michuzi
NAIBU Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, ikiwemo kuongeza miundombinu maalum, muda wa mama kumhudumia mtoto baada ya kujifungua na kuhakikisha wazazi wanashirikishwa katika malezi ya watoto hao tangu siku ya kwanza.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Watoto Wanaozaliwa Kabla ya Wakati, Dkt. Samizi amesema Serikali imeendelea kuongeza idadi ya vituo vinavyotoa huduma kwa watoto hao kutoka vituo 14 mwaka 2018 hadi zaidi ya 400 nchini, huku ikiendelea kujenga miundombinu yenye viwango katika hospitali za mikoa, wilaya na vituo vya afya vinavyohudumia idadi kubwa ya wajawazito.

Amesema hatua hiyo imeanza kuleta matokeo, kwani baadhi ya vituo vimepunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto wachanga na mahitaji ya kuwapeleka watoto katika hospitali za rufaa, huku Serikali ikilenga kuongeza zaidi vituo vyenye huduma maalum kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ili kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 50.

Dkt. Samizi amesema Serikali pia imefanyia kazi changamoto ya muda ambao mama anaruhusiwa kukaa na mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati, ambapo sasa mama anaweza kupewa muda wa ziada wa kumhudumia mtoto hadi kufikia umri unaolingana na muda ambao angekuwa amezaliwa iwapo ujauzito ungefikia wiki 40.

Aidha, amesema Serikali imeweka msisitizo katika kuwashirikisha baba katika huduma na malezi ya watoto hao, akieleza kuwa uwepo wa mzazi katika kipindi hicho ni muhimu kwa afya ya mtoto na utulivu wa mama. Amesema huduma hizo zinapaswa kutolewa kwa kuzingatia utu, staha na heshima kwa mama na familia yake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume, amesema Serikali imepokea changamoto zilizotolewa na wazazi na wadau kuhusu gharama za matibabu, miundombinu, rufaa na elimu kwa jamii, na itaendelea kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau.

Amesema takribani watoto 250,000 huzaliwa kabla ya wakati nchini kwa mujibu wa takwimu zilizopo, huku akisisitiza kuwa idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na changamoto za upatikanaji na urekodi wa taarifa. Ameongeza kuwa elimu kwa jamii kuhusu huduma kwa watoto hao ni muhimu ili kupunguza hofu, msongo wa mawazo na vitendo vya baadhi ya wazazi kukata tamaa.

Akitoa ushuhuda, Joseph Simon maarufu DJ Jose amesema mtoto wake Ethan alizaliwa njiti akiwa na ujauzito wa takribani miezi saba, hali iliyomkabili na changamoto kubwa za gharama za matibabu na kutoweza kukaa na mtoto hospitalini kwa muda wote kutokana na kutafuta fedha. Amesema uzoefu huo umemfundisha kuwa kila mtoto ni baraka na amewataka wazazi, hususan vijana, kutokata tamaa wala kusikiliza maneno yanayoweza kuwafanya waachane na watoto wao.

Naye Mary Marwa ameeleza kuwa alijifungua mtoto akiwa na ujauzito wa wiki 22 baada ya kukumbwa na changamoto ya kiafya iliyosababisha presha kupanda, akisema mtoto alizaliwa akiwa mdogo sana na madaktari walikuwa na mashaka kuhusu uwezekano wake wa kuishi. Amesema msaada wa wataalamu wa afya na kutiwa moyo na mama mwingine aliyekuwa hospitalini ulimsaidia kuendelea kuwa na matumaini, huku mtoto huyo akiendelea kukua na sasa akiwa na miaka kadhaa, jambo alilolitaja kuwa ushahidi kuwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wanaweza kuishi wanapopata huduma na uangalizi unaostahili.

Licha ya hayo, Doris Mollel Foundation (DMF) imezindua vitabu vitatu vinavyolenga kuwasaidia wazazi, wahudumu wa afya na wadau wanaojenga huduma kwa watoto wachanga nchini Tanzania. Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam Jumapili, Novemba 15, 2026, sambamba na maadhimisho ya Siku ya Watoto Njiti Duniani.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...