Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Nahodha Mussa Mandia, ametoa wito kwa sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika shughuli za usafirishaji na uhifadhi wa shehena kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma hizo, kufuatia ukuaji wa shehena katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mandia ametoa wito huo wakati wa ziara ya Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC iliyotembelea Bandari Kavu za Bravoo na Mainland Logistics jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujionea shughuli za uwekezaji na utoaji wa huduma katika sekta ya usafirishaji.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki katika uwekezaji, hivyo kuwataka Watanzania kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika sekta hiyo.
Ameeleza kuwa Bandari ya Dar es Salaam inapokea shehena kubwa zinazohitaji kuondolewa bandarini na kuhifadhiwa katika maeneo maalumu kabla ya kusafirishwa kwenda kwa watumiaji, hali inayoongeza umuhimu wa uwepo wa kampuni zinazotoa huduma za bandari kavu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Bravoo, Anjelina Ngalula, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefungua milango kwa wazawa kuwekeza katika sekta ya usafirishaji kupitia reli kuondosha Shehena Bandarini na barabara.
Amesema usikivu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sekta binafsi umechangia kuwepo kwa mazingira rafiki ya uwekezaji, ikiwamo fursa ya wadau kujadili changamoto zinazokabili shughuli zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha, amewahimiza Watanzania wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya usafirishaji na uhifadhi wa shehena kutembelea Kampuni ya Bravoo ili kujifunza namna shughuli hizo zinavyofanyika na kutumia fursa zilizopo.
Amesema uwekezaji zaidi katika eneo hilo utasaidia kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...