Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema tuzo lilizopata katika Tuzo za Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) zinatarajiwa kuongeza uwazi, uwajibikaji na uaminifu wa wananchi kwa shirika hilo, kupitia usimamizi bora wa fedha kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
TPDC imesema tuzo hizo pia ni chachu kwa shirika kuendelea kuboresha usimamizi wa fedha na utekelezaji wa majukumu yake katika sekta ya mafuta na gesi nchini.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo zilizotolewa Novemba 25, 2026, katika eneo la APC, Mbweni, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC Balozi, Ombeni Sefue amesema kutambuliwa huko ni faraja kwa bodi kwa kuwa kunathibitisha juhudi za kuhakikisha shirika linaendeshwa kwa kuzingatia misingi bora ya utawala na usimamizi wa fedha.
Amesema TPDC ni Shirika la Taifa la Mafuta (National Oil Company), lenye majukumu makubwa katika sekta ya mafuta na gesi, hivyo ni muhimu kuhakikisha taarifa zake za kifedha zinaandaliwa kwa viwango vinavyokubalika kimataifa, hususan kutokana na ushirikiano wake na kampuni mbalimbali za kimataifa.
Ameeleza kuwa taarifa za fedha ni sehemu muhimu ya taswira ya shirika, kwani zinaonesha namna linavyosimamia rasilimali zake na kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sera na miongozo ya Serikali.
Aidha, amesema tuzo za NBAA zina mchango mkubwa katika kuhamasisha ushindani chanya miongoni mwa taasisi kwa kutambua zinazofanya vizuri katika maandalizi ya taarifa za fedha, hali inayochochea mashirika mengine kuboresha mifumo yao ya usimamizi na uendeshaji.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa TPDC, Francis Upokela, amesema tuzo hizo zimewapa wafanyakazi wa shirika hilo morali ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia misingi bora ya usimamizi wa fedha.
Amesema kutambuliwa kwa TPDC katika tuzo hizo ni ishara kuwa shirika limekuwa likizingatia taratibu na miongozo mbalimbali katika usimamizi wa fedha na utekelezaji wa majukumu yake.
Upokela amesema mafanikio hayo yanaimarisha pia uaminifu wa wananchi kwa TPDC, kwa kuwa ni shirika la umma linalotekeleza majukumu yake kwa kutumia rasilimali za umma, ikiwemo fedha zinazotokana na kodi na tozo mbalimbali.


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...