Na Farida Saidi Mangube, Morogoro

WAKATI wengine walipoona mwisho wa safari, Eva John aliona mwanzo wa maisha mapya.

Mwaka 2015, baada ya kuhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kiwangwa, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Eva alitamani kuendelea na masomo, lakini changamoto za maisha zilimlazimisha kusitisha safari yake ya elimu.

Badala ya kufungua ukurasa mpya wa masomo, maisha yake yaliingia katika kipindi kigumu kilichoambatana na shinikizo la kuolewa akiwa katika umri mdogo.

Akiwa bado na ndoto za kujijenga, Eva alilazimishwa kuingia katika ndoa mara tatu na wanaume tofauti. Baadhi yao walikuwa tayari na wake wengine, huku wengine wakimtaka awe mke wa nyumbani asiyehusika katika shughuli za kiuchumi.

Hata hivyo, Eva hakukubali hali hiyo iwe hatima ya maisha yake.

Mwaka 2017, aliamua kuanza kujenga maisha yake kwa kujikita katika shughuli za kilimo. Alianza kwa kuomba ardhi kwa ndugu zake na kutafuta namna ya kujipatia kipato kupitia kilimo ili aweze kujikimu.

Mwaka 2018 alianza rasmi kujitegemea baada ya kununua shamba lenye ukubwa wa ekari moja, hatua iliyokuwa mwanzo wa safari iliyombadilisha kutoka mwanamke aliyekuwa akitegemea maamuzi ya wengine hadi kuwa mkulima, mjasiriamali na mwajiri.

Tatizo la mazao likawa fursa

Mwaka 2018, Eva alianza kilimo cha nanasi akiwa na ekari moja.

Kama ilivyo kwa wakulima wengi wanaotegemea kilimo kama chanzo cha kipato, changamoto hazikuwa chache. Uzalishaji ulikuwa mdogo, ujuzi ulikuwa bado unaendelea kujengwa na masoko hayakuwa ya uhakika.

Wakati mwingine mazao yalibaki shambani na kuharibika kutokana na kukosa wanunuzi.

Badala ya kukiona kilimo kama shughuli ya kuzalisha na kuuza mazao ghafi pekee, Eva alianza kutafuta namna ya kuongeza thamani ya mazao na kupunguza upotevu baada ya mavuno.

Hapo ndipo safari yake kutoka mkulima mdogo hadi mjasiriamali wa kilimo ilipoanza kuchukua mwelekeo mpya.

Leo, shughuli zake kupitia MJASI Enterprises zinahusisha uzalishaji na usindikaji wa mazao mbalimbali, yakiwemo mananasi, nyanya na mbogamboga.

Sh milioni 44.5 zafungua ukurasa mpya

Mabadiliko makubwa katika biashara yake yalikuja baada ya kupata mkopo wa Sh milioni 44.5 usio na riba kutoka shirika la CAMFED, kupitia mpango wa kuwawezesha wasichana na wanawake wanachama wa CAMA kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi.

Kwa Eva, fedha hizo hazikuwa tu mtaji wa biashara, bali zilikuwa fursa ya kubadili ukubwa na mwelekeo wa shughuli zake.

Alizielekeza katika kuongeza uwezo wa uzalishaji, ikiwemo kununua mashine za kukausha mazao na kupanua shughuli zake za kilimo.

Mashine hizo zimemwezesha kwenda hatua zaidi ya kuuza mazao ghafi kwa kuyaongezea thamani na kuyafanya yaweze kuhifadhiwa kwa muda mrefu zaidi.

Uwekezaji huo pia umemsaidia kupanua wigo wa uzalishaji.

Kutoka kutegemea zaidi mananasi, sasa ameanza kulima dragon fruit, huku akilenga kuongeza aina ya mazao, fursa za biashara na uzalishaji shambani.

Kwa sasa, anamiliki takribani ekari 10, kutoka ekari moja aliyokuwa nayo mwaka 2018.

Shamba lililogeuka kuwa chanzo cha ajira

Mafanikio ya Eva hayaishii katika ukubwa wa shamba.

Kupitia MJASI Enterprises, ameajiri wafanyakazi wanne, wakiwemo mwanamke mmoja na wanaume watatu, wanaomsaidia katika shughuli mbalimbali za shamba.

Aidha, zaidi ya watu 10 hupata ajira zisizo rasmi kulingana na msimu, hususan katika shughuli za kilimo na uzalishaji.

Hivyo, kile kilichoanza kama juhudi ya mwanamke mmoja kutafuta maisha, sasa kimeanza kuwa chanzo cha kipato kwa watu wengine.

Hapo ndipo maana pana ya uwezeshaji wa kiuchumi inapojitokeza, kwani mwananchi anapopata fursa ya kukuza shughuli yake, matokeo yanaweza kuvuka mipaka ya kaya yake na kuwafikia watu wengine katika jamii.

Kutoka kukatisha masomo hadi kusaidia watoto wengine

Pengine sehemu inayogusa zaidi katika simulizi ya Eva si ukubwa wa shamba lake wala thamani ya mkopo alioupata, bali kile anachofanya baada ya kufikia mafanikio hayo.

Kwa sasa, Eva anawasaidia wanafunzi 13 katika eneo analoishi kwa kuwapatia mahitaji ya shule ili waendelee na masomo.

Yeye mwenyewe alifikia kidato cha nne lakini hakupata nafasi ya kuendelea na elimu kutokana na changamoto za maisha.

Changamoto hiyo, ambayo wakati mmoja ilikuwa chanzo cha maumivu na dharau kutoka kwa baadhi ya watu, sasa imekuwa msukumo wa kuwasaidia watoto wengine wasikatize safari yao ya elimu.

Safari ya Eva inaingia katika mjadala mpana wa kitaifa kuhusu namna ya kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na kujenga uwezo wa kiuchumi.

NEEC: Uwezeshaji si kutoa fedha pekee

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bengil Issa, anasema uwezeshaji wa wananchi haupaswi kuangaliwa kwa mtazamo wa kutoa fedha pekee.

Kwa mujibu wa Bengil, Mkakati wa Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi unahitaji wananchi kuunganishwa na fursa zinazowawezesha kuzalisha, kukuza biashara na kuongeza kipato.

“Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi unahitaji kuangalia mnyororo mzima wa thamani. Mwananchi anapopata mtaji, anahitaji pia kuwa na ujuzi, teknolojia, taarifa, masoko na huduma zinazomwezesha kutumia fursa hiyo kwa tija,” anasema.

Anaeleza kuwa kilimo ni miongoni mwa maeneo yenye nafasi kubwa ya kuzalisha ajira na kipato pale kinapounganishwa na usindikaji, teknolojia na masoko.

“Tunataka kuona wananchi wakitoka kwenye uzalishaji wa kawaida kwenda kwenye shughuli zinazoongeza thamani. Hii inasaidia kuongeza kipato cha mzalishaji, kupunguza upotevu wa mazao na pia kufungua fursa nyingine katika mnyororo wa thamani,” anasema.

CAMFED na daraja kutoka elimu hadi kujitegemea

Kwa upande wa CAMFED, safari ya Eva ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wasichana na wanawake kupitia elimu, ujuzi na fursa za kiuchumi.

Akizungumza katika maadhimisho ya mafanikio ya mwaka 2025 ya mtandao wa CAMA, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa CAMFED, Anna Sawaki, alisema ushirikiano kati ya CAMFED, Serikali na wadau mbalimbali umesaidia kuwaandaa wasichana kupata elimu, ujuzi wa ufundi, mikopo na fursa za kujitegemea.

“Lengo letu ni kumfanya mtoto wa kike aweze kujitegemea yeye mwenyewe, kuisaidia familia yake na hatimaye kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa ujumla,” alisema Sawaki.

Kwa mujibu wa CAMFED, zaidi ya wasichana 100,000 kutoka mikoa 10 ya Tanzania wamefikiwa kupitia mipango ya elimu na uwezeshaji, huku zaidi ya wasichana 34,000 wakinufaika mwaka 2025 pekee.

Mwenyekiti wa mtandao huo, Shamsa Mkuruno, amesema wanachama 511 wamepata mikopo isiyo na riba kutoka CAMFED, huku wengine wakijikita katika kilimo, ushonaji, useremala, ufundi wa chuma na shughuli za kuongeza thamani ya bidhaa na mazao.

Mafanikio yanayovuka mipaka ya kaya

Kisa cha Eva kinaonyesha kwamba thamani ya uwezeshaji haiishii katika kiasi cha fedha anachopokea mwananchi.

Thamani yake inaonekana katika kile kinachotokea baada ya fursa hiyo kupatikana.

Kwa Eva, Sh milioni 44.5 zimegeuka kuwa mashine za usindikaji, uzalishaji mkubwa, upanuzi wa mashamba, zao jipya, ajira na vyanzo vipya vya mapato.

Kwa familia yake, mafanikio hayo yameambatana na kujenga nyumba, kuwasaidia wazazi na kuongeza uwezo wa kukidhi mahitaji ya kila siku.

Kwa jamii, yamezalisha ajira na shughuli za kiuchumi.

Na kwa watoto 13 anaowasaidia, mafanikio hayo yamekuwa sehemu ya jitihada za kuhakikisha changamoto za kiuchumi hazikatizi ndoto zao za elimu.

Safari yake inaacha ujumbe mpana: uwezeshaji wa kiuchumi unapounganisha mtaji na maarifa, teknolojia, masoko na mazingira wezeshi, unaweza kuwa kichocheo cha mabadiliko yanayofika mbali zaidi ya mfukoni mwa mwananchi mmoja.









Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa CAMFED Anna Sawaki Akizungumza na wanahabari katika maadhimisho ya mafanikio ya mwaka 2025 ya mtandao wa CAMA yaliyofanyika Mjini Morogoro


Na. Mwandishi Wetu, Tabora
WATENDAJI wa uchaguzi wamesisitizwa kuheshimu viapo vyao na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele leo tarehe 29 Septemba, 2026 mkoani Tabora wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge kwenye Jimbo la Chamwino Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma na Kata 11 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 04 Novemba, 2026.

“Ninawasisitiza kuheshimu viapo vyenu kwa nafasi mlizoteuliwa, tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, kanuni za maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele.

Amewaelekeza watendaji hao kuhakikisha kuwa wakati wote wa mchakato wa uchaguzi huo, wanavishirikisha kwa karibu vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yao kuhusu masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa.

Ameongeza kuwa watendaji hao wanapaswa kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha kupanga mawakala.

“Ni muhimu kwenu pia, kuhakikisha mnayatambua na kuyajua vyema maeneo ambayo uchaguzi utaendeshwa ikiwemo miundombinu ya kufika katika vituo vya kupigia kura,” amesema Jaji Mwambegele.

Amewaasa watendaji hao kuhakikisha kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yao wanao katika uendeshaji wa uchaguzi, wanaepuka kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa kila uchaguzi unatofautiana na uchaguzi mwingine.

Jaji Mwambegele amewasisitiza watendaji hao kuhakikisha wanaajiri watendaji wa vituo wenye sifa, weledi, wanaojitambua na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.

“Mhakiki vifaa vya uchaguzi mnavyopokea kutoka Tume na kuhakikisha kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema na kuhakikisha siku ya uchaguzi mnaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 asubuhi,” amesema.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanawajumuisha waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata, maafisa uchaguzi, maafisa ununuzi na wahasibu.

Kata 11 za Tanzania Bara zitakazofanya uchaguzi wa Udiwani ni Nonde iliyopo Halmashauri ya Jiji la Mbeya; Lugenge, Halmashauri ya Mji Njombe; Bargish, Halmashauri ya Mji Mbulu; Makole, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza; Mwera, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Oldonyosambu, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Nyingine ni Igalula iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui; Shelui, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba; Mvumi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Nyarero, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ilolangulu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele akizungumza leo tarehe 29 Septemba 2026 mkoani Tabora wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na Kata 11 za Tanzania bara.(Picha na INEC).

Sehemu ya washiriki ambao ni watendaji wa Uchaguzi kutoka katika Jimbo la Chamwino Mkoani Dodoma na Kata 11za Tanzania Bara wakifuatilia hotuba ya ufunguzi. (Picha na INEC).

-Kamishna Jenerali Lyimo atoa angalizo kwa familia, wamiliki wa mabasi


Na Mwandishi Wetu


FAMILIA zinazokodi mabasi madogo (hiace/coaster) kusafirisha waombolezaji au miili ya marehemu kwenda mikoani zimetakiwa kuwa waangalifu, baada ya kubainika baadhi ya gari hizo zinatumika kusafirisha Dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ni kwamba kuna magari yanayotumika kubeba miili ya marehemu yamekuwq yanabeba Dawa za kulevya wakati wa kwenda au kurudi.

Akizungumza leo Septemba 29,2026 jijini Dar es Salaam amesema Mamlaka imebainika kuna magari yanayotumika kusafirisha miili ya marehemu na wanafamilia yanatumika kusafirisha dawa za kulevya, hivyo mamlaka itachukua hatua kali kwa mujibu wa sheria.

“Iwapo tutabaini gari inayosafirisha maiti imebeba dawa za kulevya hatutasita kuchukua hatua, tutakama gari,familia na kuzuia maiti.Wanaotumia magari hayo wengine wanasafirisha dawa wakati wanaenda mkoani au wanarudi. Magari hayo mengi ni yale yanayokwenda kanda ya Kaskazini Tanga, Kilimanjaro na Arusha.”

Pia amesema kuongezeka kwa matumizi ya magari ya abiria katika usafirishaji wa dawa za kulevya ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa, huku wasafirishaji wakitumia huduma za kawaida za usafiri kusafirisha dawa hizo kati ya mkoa na mkoa.

Amewataka wamiliki na waendeshaji wa mabasi madogo, mabasi makubwa na magari binafsi kuimarisha udhibiti wa mizigo inayobeba katika magari yao, akionya kuwa gari lolote litakalobainika kutumika kusafirisha dawa za kulevya litatafishwa.

"Hatua hii inaweza kuwaacha wamiliki wa magari wasio na hatia wakipata hasara za kifedha, hasa pale ambapo wameshindwa kusimamia ipasavyo jinsi magari yao yanavyotumiwa," amesema Kamishina Jenerali Lyimo.

Ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuwa waangalifu wanapokodi magari, hasa kwa ajili ya shughuli za msiba na shughuli nyingine za kijamii, na kuweka makubaliano ya wazi na waendeshaji kuhusu mizigo na vifurushi vingine.

Wakati huo huo DCEA imeendelea kufanya operesheni maalum katika mikoa 14 kati ya Julai na Septemba MWAKA huu na kufanikiwa kukamata dawa za kulevya kilo 18,078.41.

Mikoa iliyohusika katika operesheni hizo ni Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dodoma, Mbeya, Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Kati ya dawa zilizokamatwa, kilo 11,504.76 zilikuwa ni bangi, kilo 6,529.5 mirungi, kilo 44.45 bangi aina ya skanka na gramu 41.25 za heroin huku jumla ya watuhumiwa 289 walikamatwa, ambapo 169 kati yao wamefikishwa mahakamani.Wengine taratibu za kisheria dhidi ya wengine zikiendelea.

Operesheni hizo pia zilifanikisha ukamataji wa magari mepesi manane, bajaji moja na pikipiki 40 zilizohusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya kilogramu 18,078.41 za dawa za kulevya, katika operesheni zilizofanyika katika mikoa 14 nchini katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2026.

Operesheni hizo zilifanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dodoma, Mbeya, Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Akizungumza leo Septemba 29,2026 jijini Dar es Salaam Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema Kati ya kiasi hicho kilichokamatwa kilo 11,504.76 zilikuwa bangi, kilogramu 6,529.5 mirungi, kilogramu 44.45 bangi aina ya skanka na gramu 41.25 heroin.

Pia Katika operesheni hizo, jumla ya watuhumiwa 289 walikamatwa, ambapo 169 wamefikishwa mahakamani, huku taratibu za kisheria zikiendelea dhidi ya watuhumiwa wengine.

Ameongeza operesheni hizo zimewezesha kukamatwa kwa magari nane, bajaji moja na pikipiki 40, ambazo zilitumika katika shughuli zinazohusiana na usafirishaji wa dawa za kulevya.

“Kufuatia operesheni hizo, bangi imeendelea kuongoza kwa kiwango cha uzalishaji na ukamataji, hususan katika mikoa ya Morogoro na Tabora. Mkoani Morogoro, jumla ya kilogramu 6,299.24 za bangi pamoja na kilogramu 226 za mbegu za bangi zilikamatwa, huku mkoani Tabora kilogramu 4,650.86 za bangi pamoja na kilogramu 203 za mbegu za bangi zilikamatwa.

“Kwa upande wa mirungi, operesheni zimebaini matumizi ya pikipiki na mabasi ya abiria katika usafirishaji wa dawa hiyo, hususan katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Dodoma, ambapo jumla ya kilogramu 6,412.89 za mirungi zilikamatwa,amesema.

Kamishina Jenerali Lyimo amesema katika moja ya matukio hayo, watuhumiwa watatu walikamatwa wakisafirisha bunda 238 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 125.33 kwa kutumia basi la kampuni ya RATCO, lenye namba za usajili T.443 EMG, ililokuwa likifanya safari kati ya Tanga na Dar es Salaam.

Aidha, mkoani Tabora, Wilaya ya Uyui, kilogramu 21.95 za bangi zilikamatwa katika gari aina ya TATA lenye namba za usajili T.381 DWU, lililokuwa likifanya safari kati ya Uyui mkoani Tabora na Kahama. Watuhumiwa watano walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wagonjwa na watumishi wa hospitali hiyo.

Mara baada ya kuwasili hospitalini hapo, Makamu wa Rais amepokelewa na viongozi pamoja na watumishi wa hospitali, ambapo taarifa fupi ilitolewa kuhusu maendeleo, utendaji na huduma zinazotolewa, kabla ya kutembelea wodi mbalimbali na kuzungumza na wananchi wanaopata huduma hospitalini hapo.

Akizungumza na wananchi waliolazwa hospitalini hapo, Mhe. Ndejembi aliwapa pole kutokana na maradhi yanayowakabili na kuwafikishia salamu za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akiwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuipa sekta ya afya kipaumbele na kuboresha huduma zinazotolewa katika vituo vya afya nchini.

Akiwa katika Wodi ya wazazi, Makamu wa Rais alieleza kufurahishwa kuwaona akina mama waliojifungua salama pamoja na watoto wao wakiwa na afya nzuri, akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi pamoja na vifo vya watoto.

Alisema jitihada hizo zinaendana na dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha huduma bora na salama za afya ya uzazi zinawafikia wanawake na watoto katika maeneo mbalimbali nchini, sambamba na nafasi yake katika kusukuma mbele ajenda ya kupunguza vifo vya mama na mtoto barani Afrika.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais pia alipata fursa ya kuzungumza ana kwa ana na baadhi ya wagonjwa kuhusu huduma zinazotolewa hospitalini hapo.

Wagonjwa hao walieleza kuridhishwa na huduma wanazopatiwa, huku baadhi yao wakitaja kushindwa kulipa gharama za matibabu. Kufuatia changamoto hiyo, Makamu wa Rais aliwezesha kulipwa kwa gharama za matibabu za baadhi ya wagonjwa waliokuwa wamekwama kutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipa, hatua iliyowapa unafuu wagonjwa hao pamoja na familia zao.

Ziara hiyo imempa Makamu wa Rais nafasi ya kujionea moja kwa moja huduma zinazotolewa katika Hospitali ya Mount Meru, kusikiliza wananchi wanaozitumia na kufahamu changamoto zinazowakabili, huku akisisitiza kuendelea na hatua za kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za afya nchini.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais alitembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha, kuwasalimu wananchi na kujionea hali ya mazingira mkoani humo.






SAME.

WANANCHI wa Jimbo la Same Mashariki, wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari na kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Nino zinazotarajiwa kuanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu.

Huku wataalamu wakitoa tahadhari juu ya uwezekano wa kutokea kwa mafuriko, mmomonyoko wa udongo na changamoto nyingine zinazoweza kuhatarisha maisha na mali za wananchi.

Rai hiyo ilitolewa katika semina maalumu iyofanyika jana kata ya Ndungu iliyolenga kutoa elimu kuhusu El Nino, namna inavyoweza kuathiri jamii pamoja na hatua muhimu za kuchukua kabla na wakati na baada ya mvua hizo, iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, na kuwakutanisha Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Madiwani pamoja na wataalamu kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Akizungumza mara baada ya semina hiyo, Mbunge Jimbo hilo, Anne Kilango aliishukuru GST kwa kutoa elimu hiyo, akisema atahakikisha elimu na taarifa za tahadhari zinazohusiana na El Nino zinawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo kwa wakati, ili kuwawezesha kuchukua hatua za kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, Mjiolojia Mwandamizi kutoka GST, Gabriel Mbogoni, alisema maeneo mbalimbali waliyoyatembelea katika Wilaya ya Same yanakabiliwa na changamoto zinazofanana.

Mbogoni alisema baadhi ya shughuli za kilimo zinazofanyika katika maeneo hatarishi zinaweza kuchangia mmomonyoko wa udongo na kupasuka kwa ardhi, hali ambayo inaweza kuongeza madhara wakati wa mvua kubwa hasa kipindi hiki cha mvua za El Nino.







Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Asha-Rose Migiro, amefungua semina elekezi kwa Kaimu Makatibu wa CCM Mikoa 32, leo Septemba 29, 2026, jijini Dodoma.

Semina hiyo ya siku mbili inalenga kuwajengea uwezo viongozi hao kuhusu majukumu yao ya kiuongozi, uendeshaji wa shughuli za chama pamoja na utekelezaji wa mipango na maelekezo ya Chama Cha Mapinduzi.

Akifungua semina hiyo, Ndugu Migiro amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na kuzingatia misingi, kanuni na taratibu za chama.








Uchunguzi uliofanywa katika sekta ya usafiri wa mtandao nchini Tanzania umeibua wasiwasi kwamba kutokuwapo kwa usawa katika utekelezaji wa masharti ya udhibiti kunahatarisha usalama wa abiria, huku kukiziweka katika mazingira magumu kampuni zinazowekeza fedha nyingi kutimiza matakwa ya kisheria. 

Waandishi wa habari waliojaribu taratibu za usajili walibaini kuwa baadhi ya makampuni yaliwaruhusu madereva wanaotaka kujiunga kuendelea na mchakato bila kuwasilisha kikamilifu nyaraka muhimu, ikiwemo picha, leseni sahihi ya udereva, kadi ya usajili wa chombo, leseni ya LATRA na nyaraka za bima. 

Majaribio ya usajili yaliyofanywa kwa kificho yalibaini tofauti kubwa katika masharti ya kuwapokea na kuwahakiki madereva kati ya kampuni moja na jingine. Hali hiyo imeongeza wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wadau kwamba waendeshaji wanaokabiliwa na uangalizi mdogo wa udhibiti wanalegeza masharti ya uhakiki ili kuongeza idadi ya madereva kwa kasi. 

Mbinu hiyo inaweza kuharakisha uongezekaji wa madereva kwenye aplikesheni, lakini pia inatengeneza mazingira yasiyo sawa kibiashara. Kampuni zinazolipia leseni, uhakiki wa madereva, bima, mifumo ya uzingatiaji wa kanuni na kodi hubeba gharama ambazo washindani wasiotimiza masharti kikamilifu huziepuka. 

Matokeo yake ni kuwapo kwa faida isiyo ya haki katika gharama za uendeshaji, hali inayoweza kuvuruga ushindani wa nauli na kukatisha tamaa uwekezaji wa muda mrefu katika sekta hiyo. 

Athari zake kwa usalama nazo ni kubwa. Baadhi ya abiria waliohojiwa walisema wamekutana na akaunti zisizo na picha za madereva, majina yanayoonekana kuwa ya utani badala ya utambulisho unaoweza kuthibitishwa, pamoja na magari yanayofika yakiwa na taarifa tofauti na zile zilizooneshwa kwenye programu. 

Kanuni za LATRA zinataka magari ya kukodi kuwa na leseni halali, huku waendeshaji wa makampuni ya taxi mtandao wakitakiwa kuhakikisha madereva na magari yanayosajiliwa yanakidhi viwango vilivyowekwa. Matokeo ya uchunguzi huo yanaimarisha hoja ya kuitaka LATRA kusimamia masharti ya uzingatiaji wa sheria kwa usawa katika makampuni ya taxi mtandao yote. 

Ushindani wa haki hauwezi kuwepo ikiwa baadhi ya waendeshaji wanabeba gharama kamili za udhibiti huku wengine wakikua kwa kukwepa masharti hayo. Utekelezaji wenye usawa ni muhimu katika kulinda abiria, kuhifadhi imani ya wawekezaji na kujenga sekta endelevu ya usafiri wa kidijitali nchini Tanzania.






Na MWANDISHI WETU - ARUSHA

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuimarisha nafasi yake katika kuwezesha shughuli za Serikali kidijitali kwa kutoa huduma ya intaneti yenye uhakika na kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano inayosaidia utekelezaji wa shughuli za Serikali, taasisi na mashirika ya umma nchini.

TTCL imetoa huduma hiyo katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (Chairpersons and CEOs Forum), kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), ambapo huduma ya intaneti imewawezesha washiriki kupata na kubadilishana taarifa kwa wakati, kufanya mawasiliano ya kidijitali na kutumia mifumo mbalimbali katika shughuli za kikao.

Kikao hicho cha siku tatu kimefunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndenjembi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kinawakutanisha Wenyeviti wa Bodi, Wakuu wa Taasisi pamoja na viongozi mbalimbali kujadili masuala ya kimkakati yanayohusu uongozi, uwajibikaji, utawala bora na uboreshaji wa utendaji wa taasisi na mashirika ya umma.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kufunguliwa kwa kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa, amesema Shirika hilo litaendelea kuwezesha uchumi wa kidijitali kupitia uwekezaji na usimamizi wa miundombinu ya mawasiliano, huduma za kifedha za kidijitali na teknolojia zinazochochea maendeleo ya taifa.

Bw. Marwa amesema miundombinu ya mawasiliano ina nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kukuza uchumi wa kidijitali na kuwawezesha wananchi, wafanyabiashara na taasisi kupata huduma kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Ameeleza kuwa TTCL inaendelea kuwekeza na kusimamia miundombinu ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, minara ya mawasiliano na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (National ICT Data Centre), ambayo inawezesha upatikanaji wa mawasiliano, uhifadhi wa taarifa na matumizi ya huduma mbalimbali za kidijitali.

Kwa mujibu wa Bw. Marwa, jukumu la TTCL ni kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kujengwa, kuimarishwa na kusimamiwa kwa ufanisi ili huduma za mawasiliano zipatikane kwa uhakika na kusaidia shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, amesema TTCL inachangia kuwezesha miamala ya kifedha ya kidijitali kupitia huduma zake, huku ikiendelea kuunga mkono juhudi za kukuza ajira kwa vijana kupitia programu za mafunzo kwa vitendo na kuwashirikisha katika shughuli za mawasiliano ya simu pamoja na usambazaji wa huduma za intaneti kwa teknolojia ya faiba kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Akizungumzia matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), Bw. Marwa amesema teknolojia hiyo inahitaji miundombinu imara ya mawasiliano pamoja na uwezo wa kutosha wa kuhifadhi na kuchakata data.

Amesema TTCL inaendelea kuboresha na kupanua uwezo wa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za kidijitali na teknolojia mpya.

Utoaji wa huduma ya intaneti katika kikao hicho unaakisi dhamira ya TTCL ya kuendelea kuwa mhimili wa mawasiliano nchini kwa kuiwezesha Serikali, taasisi na mashirika ya umma kupata miundombinu na huduma za mawasiliano zinazochochea ufanisi katika utendaji, ushirikiano na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kupitia uwekezaji katika miundombinu na uboreshaji wa huduma za mawasiliano, TTCL inaendelea kuchangia utekelezaji wa ajenda ya Mageuzi ya Kidijitali Tanzania kwa kuhakikisha teknolojia inatumika kuongeza tija, uwajibikaji na ufanisi katika shughuli za Serikali na uchumi kwa ujumla.









Na; Mwandishi Wetu – Morogoro.

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu, Idara ya Usimamizi wa Maafa Dkt. Salim Manyata ametoa Salaam za Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Kamati za Maafa za Mkoa wa Morogoro pamoja na Timu ya Mkoa ya Kukabiliana na Dharura wakati wa kikao kazi kitakachoambata na ziara ya kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwa Mikoa kuhusu kujiandaa na kukabiliana na athari za El Nino tarehe 28 Septemba 2026.

Mawasilisho mbalimbali yamewasilishwa katika kikao kazi hicho ikiwa ni pamoja na Taarifa ya Utayari kwa kila sekta na wadau ya kujiandaa na kukabiliana na athari za El Nino, ambapo sekta zilizohusika ni pamoja na TANROADS, TARURA, Sekta ya Afya,TANESCO, kilimo, Maji yaani maji safi na maji taka na Mamlaka zote za Bonde, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Shirika la Reli nchini (TRC), Maliasili, REDCROSS na SKAUTI.


Awali, akizungumza katika kikao hicho kilichohusisha pia kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa kabla ya kuanza Ziara Maalum Mkoani hapo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Masauni (Mb), alisema ni muhimu kuchukua tahadhari na hatua mahsusi kuhusiana na tishio la El Nino na kuweka nguvu zaidi katika kuzuia na kujiandaa ili hata madhara yatakapotokea yasiwe makubwa zaidi.


“Tutumie vizuri Rasilimali zilizopo ili kuweza kukabiliana na jambo hili, sambamba na kuzingatia suala zima la usafi wa mazingira katika maeneo yetu Alisisitiza Waziri Masauni.’

Imeelezwa kuwa Mkoa wa Morogoro ni Miongoni mwa Mikoa ambayo imekuwa akiathirika mara nyingi na mvua za misimu tofauti, hivyo ni vyema kuangaliwa kwa namna ya kipekee hasa katika kipindi hiki cha Mvua za El Nino, zilizotabiriwa na Mamlaka ya hali ya hewa Nchini kunyesha mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2026


" Usimamizi wa Maafa ni jukumu la kila mtu, kila mmoja anatakiwa kushiriki sasa na kuchukua hatua katika eneo lake ili kuokoa maisha, mali, miundombinu na mazingira."





Na Chalila Kibuda , Bagamoyo
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), limefanya zoezi la majaribio ya Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini Tanzania Bara kwa mwaka 2026 katika maeneo ya Pwani ya Bagamoyo.

Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Sensa hiyo, kwa lengo la kupima uelewa na uwezo wa washiriki katika kutekeleza mafunzo waliyopatiwa, pamoja na kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa ukusanyaji wa taarifa.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu Wanaoratibu Sensa hiyo, Nahodha Alex Katama, amesema zoezi la majaribio limekwenda vizuri na washiriki wameweza kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maelekezo na mafunzo waliyopatiwa.

Amesema Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini inatarajiwa kuanza Oktoba Mosi na kukamilika Oktoba 25, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katama, zoezi la majaribio limewapa washiriki wanaohusika na ukusanyaji wa taarifa fursa ya kufanya kazi kwa vitendo, hatua iliyowasaidia kujenga uelewa na uzoefu wa namna ya kukusanya taarifa sahihi kutoka kwa wadau wa sekta ya usafiri majini.

“Kwa ujumla, zoezi limekwenda vizuri. Washiriki wanaokwenda kukusanya taarifa wameweza kufanya majaribio kama walivyofundishwa, jambo ambalo linatupa imani kuwa watakuwa tayari kutekeleza zoezi la Sensa kwa ufanisi,” amesema Katama.

Kwa upande wao, wavuvi pamoja na wajenzi wa vyombo vya usafiri majini, wameeleza utayari wao wa kutoa ushirikiano katika zoezi hilo kwa kutoa taarifa zinazohitajika ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi na zenye ubora kuhusu sekta ya usafiri majini nchini.

Mtengenezaji wa vyombo vya majini, Said Doto, amesema watatoa ushirikiano wakati zoezi hilo litakapoanza ili kuiwezesha Serikali kupata taarifa zitakazosaidia katika kupanga na kuendeleza shughuli za karakana za ujenzi wa vyombo vya majini.

“Tutatoa ushirikiano ili Serikali iweze kupata taarifa sahihi na kupanga mipango mizuri kwa upande wa karakana za vyombo vya majini,” amesema Doto.

Naye Mtakwimu wa TASAC, Ally Njama, amesema zoezi la majaribio limefanikiwa na kutoa uzoefu muhimu kwa washiriki kabla ya kuanza kwa zoezi rasmi.

Amesema ushirikiano wa wadau wakati wa Sensa hiyo utasaidia kuhakikisha taarifa zitakazokusanywa zinakuwa sahihi na kuwezesha zoezi kufanyika kwa ufanisi.

Sensa hiyo inalenga kupata taarifa muhimu kuhusu idadi na aina ya vyombo vya usafiri majini, pamoja na shughuli za ujenzi wa meli na vyombo vingine vya majini Tanzania Bara.

TASAC na NBS zimeendelea kuhamasisha wadau wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati, ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu zitakazosaidia katika kupanga, kusimamia na kuendeleza sekta ya usafiri majini nchini.