Na Mwandishi Wetu
ATLAS Schools inatarajia kushirikisha zaidi ya wakimbiaji 3,000 katika mbio za Atlas Schools Half Marathon, msimu wa nane, zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 14, mwaka huu, katika viwanja vya shule hiyo, Madale, Dar es Salaam, kwa lengo la kuhamasisha afya bora, michezo na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mbio hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Atlas Day, Wakili Didas Kanyambo, amesema tukio hilo linatarajiwa kuvutia zaidi ya watu 10,000 watakaoshiriki kwa namna mbalimbali, likiwa na kaulimbiu isemayo “Run for Nature, Run for Kids” inayosisitiza umuhimu wa kutunza mazingira kwa manufaa ya watoto na vizazi vijavyo.

Amesema mbio hizo zitakuwa na makundi matatu, yakiwamo kilomita 21 kwa wanariadha wa mbio ndefu, kilomita 10 kwa kampuni na taasisi, pamoja na kilomita tano kwa washiriki wanaotaka kushiriki kwa burudani na kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi. Ameeleza kuwa njia za mbio zimeandaliwa kwa kuzingatia umbali na usalama wa washiriki.

Kanyambo amesema kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuhamasisha jamii kutambua kuwa afya na maendeleo ya watoto yanategemea pia mazingira wanamoishi, yakiwamo upatikanaji wa hewa safi, maji salama, miti na maeneo safi. Ameongeza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja, kuanzia familia, shule na taasisi hadi Serikali na sekta binafsi.

Amesema Oktoba 14 pia itakuwa siku ya mahafali ya 20 ya Atlas Schools, yatakayowakutanisha wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la saba na kidato cha nne. Amesema kuunganisha mbio hizo na mahafali ni sehemu ya utamaduni wa shule hiyo wa kuenzi Siku ya Mwalimu Julius Nyerere kwa kuhimiza elimu, nidhamu, uzalendo na malezi bora kwa watoto.

Kwa mujibu wa Kanyambo, Atlas Schools inaamini kuwa elimu bora haipaswi kuishia katika ufaulu wa mitihani pekee, bali inapaswa kumjenga mwanafunzi katika nyanja mbalimbali, zikiwamo michezo, afya, uongozi na utunzaji wa mazingira. Amesema shule hiyo inasisitiza ufaulu wa kiwango cha Single Digit huku ikiweka mazingira yanayowezesha wanafunzi kukuza vipaji na kujiandaa kwa maisha ya baadaye.

Katika mbio hizo, washindi watano wa kwanza katika kila kundi watapata zawadi za fedha kwa wanaume na wanawake. Mshindi wa kwanza wa kilomita 21 atazawadiwa Shilingi 300,000, kilomita 10 Shilingi 200,000 na kilomita tano Shilingi 150,000, huku zawadi nyingine zikitolewa kulingana na nafasi za washindi. Jumla ya fedha zilizotengwa kwa zawadi ni Shilingi 3,010,000.

Amesema ada ya ushiriki ni Shilingi 40,000, ambapo kila mshiriki atapata vifaa rasmi vya kukimbilia (Official Running Kit) pamoja na medali baada ya kumaliza mbio. Usajili na malipo yatafanyika kupitia MIXX by YAS Paybill namba 5927380, kwa jina la Atlas Schools, huku washiriki wenye changamoto wakitakiwa kuwasiliana na uongozi kupitia namba 0787 651 656 au 0715 651 656.

Aidha, amewashukuru wadhamini na washirika wa mbio hizo, wakiwamo Kilimanjaro Natural Mineral Water, SGA Security, ASAS Maziwa, Kuambiana Investment, 4JS Fitness Centre, CRDB Bank na Riadha Taifa, kwa kuunga mkono maandalizi. Amewahimiza wananchi, kampuni, taasisi, wazazi na vijana kujisajili mapema na kushiriki katika mbio hizo, akisisitiza kuwa ujumbe mkuu ni kulinda mazingira leo ili watoto warithi Tanzania safi na salama kesho.

Na Mwandishi Wetu, Simanjiro

NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Kinyasi Ole Millya, amewataka wakazi wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kuthamini na kuheshimu uteuzi unaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan badala ya kubeza nafasi wanazopewa viongozi kutoka wilayani humo.

Ole Millya, ambaye pia ni Mbunge wa Simanjiro, ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Kimotorok, Kata ya Loiborsiret, alipokutana na wananchi, kuwashukuru kwa ushirikiano wao na kusikiliza kero zinazowakabili.

Amesema tangu kuanzishwa kwa Wilaya ya Simanjiro, haijawahi kupata kiongozi katika nafasi ya Naibu Waziri, hivyo wananchi wanapaswa kuthamini nafasi hiyo na kushukuru kwa hatua iliyofikiwa.

“Wana Simanjiro, tukipata nafasi ya uteuzi hata kama ni ndogo, tunapaswa kushukuru kwa moyo mkunjufu na siyo kuibeza,” amesema Ole Millya.

Akizungumzia suala hilo, Diwani wa Kata ya Komolo, Saning'o Somii, amesema baadhi ya viongozi wastaafu wanapotosha jamii kwa kudai kuwa nafasi ya Naibu Waziri ni ndogo ikilinganishwa na nafasi ya Mkuu wa Mkoa ambayo baadhi yao waliwahi kushikilia.

“Mtu badala ya kukaa pembeni baada ya kukosa uongozi, anataka kwenye sherehe aimbiwe wimbo wa sifa kama yupo madarakani,” amesema Somii.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Terrat, Jackson Ole Materi, amewataka viongozi wastaafu kujiepusha na kauli zinazoweza kudhoofisha heshima ya viongozi waliopo madarakani na badala yake kuwaachia nafasi ya kutekeleza majukumu yao.

Amesema nafasi ya Naibu Waziri ina majukumu yanayohusisha masuala ya kitaifa na ushiriki katika shughuli za Baraza la Mawaziri, huku Mkuu wa Mkoa akisimamia shughuli za Serikali katika eneo lake la kiutawala.

“Mtu anasema yeye alikuwa Mkuu wa Mkoa ni nafasi kubwa kuliko nafasi ya Naibu Waziri, jambo ambalo siyo sahihi, kwani Naibu anazunguka nchi nzima na Mkuu wa Mkoa anaongoza mkoa mmoja, pia Naibu anakuwepo kwenye Baraza la Mawaziri tofauti na RC,” amesema Ole Materi.

Naye mkazi wa Kijiji cha Kimotorok, Nai Mollel, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Ole Millya kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

“Ningemuona mama yetu Samia ningemkumbatia na kumbusu mara 10 kama ishara ya kumshukuru kwa kumteua kuwa Naibu Waziri mtoto wetu Ole Millya,” amesema Mollel.

Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Wambura Igembya, amewataka wakazi wa Loiborsiret kuepuka siasa zisizo za kistaarabu na kuelekeza nguvu zao katika shughuli za maendeleo.

Naye Diwani wa Kata ya Loiborsiret, Ezekia Lesenga maarufu kama Mardadi, amempongeza Ole Millya kwa juhudi zake za kushughulikia migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Simanjiro.

Mardadi amesema katika kipindi cha kwanza cha ubunge wa Ole Millya, kuanzia mwaka 2015 hadi 2020, mawaziri wanane walifika katika kata hiyo kwa lengo la kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiikabili jamii.


LONDON, UINGEREZA — Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania ina mazingira rafiki ya uwekezaji yanayolenga kuvutia mitaji na kukuza shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali.

Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 9, 2026, alipokutana na kuzungumza na wawekezaji walioshiriki katika Kongamano la Kimkakati la Uwekezaji na Masoko ya Fedha lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Citi Bank nchini Uingereza.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu ameeleza kuwa mazingira ya uwekezaji nchini yanaimarishwa kupitia sera, sheria na miundombinu inayolenga kuwezesha shughuli za uwekezaji na kukuza ushiriki wa wawekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi.

Amezitaja sekta za benki na madini kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa za uwekezaji, huku akieleza umuhimu wa kuwepo kwa mazingira yanayowezesha mitaji kuingia nchini na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Dkt. Mwigulu yuko nchini Uingereza kwa ziara ya kikazi ya siku tano, inayolenga kutekeleza shughuli mbalimbali za kikazi.








Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo tarehe 09 Oktoba 2026, ametembelea DOC Medical Center nchini Qatar, kituo cha huduma za afya kinachotoa huduma kupitia idara nane za kitaalamu za kiafya, chini ya mwanzilishi wake na Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Emmanuel Tolessa.

Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amevutiwa na huduma zinazotolewa na kituo hicho, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya kupitia Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PSSSF, kwa lengo la kuanzishwa hospitali hii nchini Tanzania.

Kupitia mpango huo wa ushirikiano, DOC Medical Center inatarajiwa kuchangia vifaa tiba, wataalamu wa afya na baadhi ya madaktari, kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya nchini. Mradi huo unalenga pia kuanzisha huduma za hospitali na famasia, huku kukiwa na matarajio ya kukamilika kabla ya kuanza kwa michuano ya AFCON 2027.

DOC Medical Center ina uzoefu wa kutoa huduma za afya katika matukio makubwa ya kimataifa, ikiwemo michuano ya Kombe la Dunia la FIFA ya mwaka 2022 nchini Qatar.

Rais Dkt. Mwinyi amehitimisha ziara yake ya kikazi nchini Qatar leo na anatarajiwa kuelekea Madrid, Uhispania, kuendelea na ziara yake.



















NA DENIS MLOWE, IRINGA


CHUO Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kimeahidi kushiriki katika mbio za Kitonga Marathon zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 31, 2026, wilayani Kilolo mkoani Iringa, kikieleza kuwa zitakuwa fursa ya kuhamasisha afya, kutangaza taasisi na kuimarisha mahusiano na jamii.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Method Samuel, baada ya kupokea ugeni wa waratibu wa Kitonga Marathon waliotembelea chuo hicho kwa ajili ya kuhamasisha ushiriki wa taasisi hiyo katika mbio hizo.

Profesa Samuel amesema chuo kinapongeza juhudi za waandaaji kuja na wazo la kuandaa mbio hizo, akieleza kuwa ni ubunifu unaoweza kuleta manufaa mbalimbali kwa jamii, ikiwemo kuimarisha afya za washiriki na kutangaza vivutio na fursa zilizopo Kilolo.

Amesema ushiriki wa chuo hicho pia utasaidia kutangaza shughuli zake kwa umma, ili watu wengi zaidi wafahamu huduma na mchango wake katika jamii, sambamba na kutekeleza maelekezo ya Serikali kuhusu kuimarisha uhusiano kati ya taasisi na wananchi.

Ameongeza kuwa mbio hizo zitakuwa jukwaa la kujenga mahusiano mazuri kati ya chuo hicho na wadau wa Wilaya ya Kilolo, ambao ni sehemu ya jamii inayohudumiwa na taasisi hiyo.

Profesa Samuel amesema ushiriki huo utatoa fursa kwa wafanyakazi wa chuo kukutana na watu kutoka maeneo mbalimbali, kujenga mitandao ya mawasiliano na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala yenye manufaa kwa maendeleo ya jamii.

Amesema chuo kimejipanga kushiriki kikamilifu na kuunga mkono juhudi za waandaaji katika maandalizi ya mbio hizo, akihimiza wadau wengine kuunga mkono tukio hilo.

Wakati huohuo, mtangazaji maarufu nchini, Maulid Kitenge, amethibitisha kushiriki katika Kitonga Marathon kupitia ujumbe uliosambazwa kwenye ukurasa wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Siwema H. Jumaa.

Kitenge, ambaye pia ametaja ushiriki wa kundi la Crown Jogging la jijini Dar es Salaam, amewahimiza wananchi kujisajili mapema ili kushiriki katika mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu, katika eneo la Mlima Kitonga, wilayani Kilolo.

Amesema maandalizi ya kushiriki yako tayari, huku akitoa wito kwa wananchi na wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi kuunga mkono tukio hilo.

Kitonga Marathon inalenga kutumia michezo kama jukwaa la kuhamasisha afya, kutangaza utalii na fursa za uwekezaji, pamoja na kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuitangaza Wilaya ya Kilolo kwa watu kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Siwema H. Jumaa alisema mbio hizo zitahusisha mbio za barabarani za kilomita tano, 10 na 21, pamoja na trail run ya Mlima Kitonga, ambayo itafungua fursa kwa wananchi na wageni kushiriki shughuli za hiking na utalii wa asili katika eneo hilo.

Mkurugenzi Siwema alisema waandaaji wanatarajia kupata washiriki wasiopungua 800, huku usajili ukiendelea.

Alisema washiriki wa mbio za kilomita tano, 10 na 21 watalipia Sh50,000, huku watakaoshiriki mbio za kupanda Mlima Kitonga wakilipa Sh70,000 na kupata T-shirt, begi, medali na namba ya mshiriki.

Katika mbio za kilomita 21, mshindi wa kwanza atapata Sh1 milioni, wa pili Sh600,000 na wa tatu Sh400,000 kwa upande wa kilomita 10, washindi watatu wa kwanza kwa wanawake na wanaume watapata Sh500,000, Sh300,000 na Sh200,000 mtawalia.



Misugusu sasa kuhakiki magari 60

Kituo cha Uhakiki wa Vipimo kinachomilikiwa na Wakala wa Vipimo (WMA) cha Misugusu mkoani Pwani kimeongeza uwezo wa kuhakiki magari yanayosafirisha mafuta kutoka magari nane hadi 60 kwa siku, hatua inayowarahisishia wafanyabiashara na wasafirishaji kupata huduma kwa wakati.

Meneja wa kituo hicho, Mrisho Mandari, amesema kazi kubwa ya kituo ni kuhakiki magari yanayosafirisha mafuta ya petroli na dizeli kutoka Tanzania na nchi jirani, zikiwemo Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi.

Mandari amesema awali huduma hizo zilitolewa katika kituo cha Ilala, ambacho kilikuwa na uwezo wa kuhakiki magari manane kwa siku. Hata hivyo, Serikali ilijenga kituo kipya cha Misugusu ili kuongeza uwezo wa kuhudumia wateja na kupunguza muda wa kusubiri.

Amesema kwa sasa kituo kina uwezo wa kuhakiki magari 60 kwa siku, hivyo kuwawezesha wasafirishaji kutoka mikoa mbalimbali kufika, kupata huduma na kuendelea na shughuli zao bila usumbufu mkubwa.

Raymond George kutoka Kampuni ya Abood Morogoro amesema ameridhishwa na huduma alizopata baada ya kufika kituoni hapo asubuhi na kukamilisha zoezi la uhakiki siku hiyo hiyo. Amewahimiza wasafirishaji wengine kutoka mikoani kutumia kituo hicho ili kurahisisha shughuli zao.

Kwa upande wake, Anthony Mulenga kutoka Zambia, anayefanya kazi katika Kampuni ya Latitude, amesema kampuni yao hupeleka magari yale Tanzania kwa ajili ya uhakiki wa vipimo. Amesema wamekuwa wakipata huduma nzuri na kwamba madereva wao hawajawasilisha malalamiko kuhusu huduma wanazopata kituoni hapo.

Baadhi ya wateja wengine wameeleza kuridhishwa na muda unaotumika kukamilisha uhakiki, wakisema hurudi kituoni baada ya muda wa vyeti vyao vya uhakiki kuisha ili kufanya ukaguzi unaohitajika na kuendelea na shughuli za usafirishaji.


 

Na Victor Masangu, Pwani

KATIBU Mkuu mpya wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Rugemarila Rutatina, amesema hatasita kuwachukulia hatua viongozi na watumishi watakaobainika kuchelewesha utekelezaji wa majukumu yao ndani ya chama hicho.

Amesema atahakikisha viongozi wanatimiza wajibu wao ipasavyo na kuacha kutoa visingizio visivyo na msingi, akisisitiza kuwa wakati wa maneno umepita na sasa ni kipindi cha kuchapa kazi kwa vitendo ili kuwatumikia wanachama na kulinda maslahi yao.

Rutatina ameyasema hayo wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi kwa uongozi mpya uliochaguliwa hivi karibuni, iliyofanyika katika makao makuu ya chama hicho na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, wastaafu pamoja na wanachama kutoka matawi mbalimbali, wakiwemo wa Mkoa wa Pwani.

Amesema viongozi na watendaji wanapaswa kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi, akionya kuwa hatachukulia kwa uzito mdogo vitendo vya uzembe katika utendaji.

“Kitu kikubwa ni watendaji na viongozi kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ipasavyo, kuweka mikakati ya kuwatumikia wanachama, na nitakuwa na msimamo mkali dhidi ya wale watakaobainika kufanya uzembe,” amesema Rutatina.

Aidha, amesema atashirikiana na viongozi wenzake kuweka malengo ya kuongeza idadi ya wanachama na kuimarisha chama ili kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa TUGHE, Aloisi Mapembe, amewataka viongozi waliochaguliwa kutobweteka baada ya kupata madaraka, badala yake waweke mikakati ya kuongeza wanachama na kuimarisha ushiriki wao katika chama.

Mapembe amesema kila kiongozi anapaswa kuweka mkakati wa kusajili angalau wanachama wapya 100 kwa mwaka, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupanua wigo wa chama na kuimarisha nguvu yake katika kutetea maslahi ya wafanyakazi.

Pia ameahidi kuwa katika kipindi chake cha uongozi ataanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi itakayoongeza kipato cha wanachama na kukifanya chama hicho kujitegemea kiuchumi.

Naye Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Pwani, Catherine Katele, amesema baada ya uchaguzi kukamilika, jukumu lililopo mbele yao ni kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza matarajio ya wanachama waliowapa dhamana ya kuwaongoza.

Amesema uongozi huo utajitahidi kurejesha imani waliyopewa kwa kuhakikisha unasimamia na kutetea maslahi ya wafanyakazi kwa mujibu wa wajibu wao.

Kwa upande wake, mwakilishi wa wafanyakazi, Sara Stephano, ameahidi kuwa watafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na uongozi mpya ili kuleta mabadiliko chanya katika utetezi wa maslahi ya wafanyakazi wa sekta ya afya na serikali nchini.



Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha

LICHA ya biashara nyingi kuendelea kushamiri nchini Tanzania, bado kuna changamoto ya uelewa kuhusu umuhimu wa kusajili alama za biashara na huduma, jambo linaloweza kuwaweka wafanyabiashara katika hatari ya kupoteza utambulisho wa bidhaa zao sokoni.

Usajili wa alama za biashara ni miongoni mwa hatua muhimu zinazomsaidia mfanyabiashara kutofautisha bidhaa zake na za wengine, kujenga utambulisho unaotambulika kwa wateja na kulinda maslahi yake katika soko lenye ushindani.

Akizungumzia suala hilo jijini Arusha, Msaidizi wa Msajili Mkuu kutoka Kurugenzi ya Miliki Bunifu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Nassoro Mtavu, amewataka wafanyabiashara kutumia fursa ya usajili kulinda majina, alama na ubunifu unaotambulisha biashara zao.

Mtavu ameyasema hayo wakati akizungumza na washiriki wa Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii wa Sanaa na Utamaduni yanayoendelea jijini Arusha , akieleza kuwa BRELA inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa Mtavu, majukumu ya BRELA yanajumuisha usajili wa kampuni za ndani na nje zinazofanya biashara nchini, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, pamoja na uvumbuzi unaohusiana na miliki bunifu.

Amesema huduma hizo zina umuhimu mkubwa kwa wafanyabiashara wanaotaka kuimarisha biashara zao na kuhakikisha utambulisho wa bidhaa zao unalindwa dhidi ya matumizi yanayoweza kuathiri maslahi yao.

"Kwa mfanyabiashara, alama ya biashara si jina au nembo tu, bali ni sehemu ya utambulisho unaowasaidia wateja kuitambua bidhaa yake miongoni mwa bidhaa nyingine zinazopatikana sokoni, " amesema na kuongeza:

"Kwa mfano, wafanyabiashara wanaotengeneza bidhaa za sanaa, mavazi, bidhaa za ngozi na kazi za mikono wanaweza kujenga utambulisho wa biashara zao kupitia majina na alama zinazowatofautisha na washindani wao,".

Amesema ili kulinda utambulisho huo kwa njia ya kisheria, ni muhimu mfanyabiashara kupata taarifa sahihi kuhusu aina ya usajili unaohitajika na taratibu zinazotumika.

Mtavu ameeleza kuwa usajili wa kampuni, jina la biashara, alama ya biashara na uvumbuzi hutegemea mahitaji ya mfanyabiashara, huku akisisitiza kuwa baadhi ya masharti ya uendeshaji wa biashara ni ya lazima kwa mujibu wa sheria.

“Kwenye eneo hili, mfanyabiashara mwenyewe ataamua kusajili ili kulinda kampuni yake, jina la biashara, alama au uvumbuzi wake,” amesema Mtavu.

Ameongeza kuwa mfanyabiashara anaweza kuamua kama anataka kuendesha biashara yake kupitia kampuni iliyosajiliwa au kwa kutumia jina la biashara, kulingana na mahitaji yake.

Mbali na usajili wa kampuni na miliki bunifu, Mtavu amesema BRELA pia inasimamia masuala ya leseni za viwanda na leseni za biashara za kundi A, zinazohusisha biashara zenye wigo wa kitaifa na kimataifa.

Amebainisha kuwa mtu anayetaka kuendesha shughuli za biashara au kiwanda anatakiwa kuzingatia matakwa ya kisheria na kupata leseni inayohitajika kulingana na aina ya shughuli anayoifanya.

Wafanyabiashara wanapaswa kutofautisha kati ya usajili unaolenga kutambua na kulinda biashara zao na vibali vinavyotakiwa kisheria ili kuruhusiwa kuendesha shughuli husika.

Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii wa Sanaa na Utamaduni yanayoendelea jijini Arusha yamekuwa jukwaa la kukutanisha wadau wa sanaa, utamaduni na biashara, huku wafanyabiashara wakipata nafasi ya kuonesha bidhaa zao na kujenga mahusiano ya kibiashara.

Kwa wafanyabiashara wanaoshiriki maonyesho hayo, uelewa wa usajili wa alama za biashara na milki bunifu unaweza kuwa hatua muhimu katika kukuza biashara zao na kuongeza uwezo wa bidhaa za Kitanzania kushindana sokoni.

Ujumbe wa BRELA kwa wafanyabiashara ni kwamba, pamoja na kuzalisha bidhaa bora na kutafuta masoko, ni muhimu pia kufahamu taratibu za kusajili na kulinda utambulisho wa biashara zao ili kuimarisha misingi ya ukuaji endelevu wa biashara nchini.




Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha

SPIKA wa Bunge la Australia, Milton Dick, amechaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) baada ya kupata kura 182 sawa na asilimia 56 ya kura zote 

Akitangaza matokeo ya washindi, Rais anayemaliza muda wake Dkt Tulia Ackson amesema nafasi ya pili ilichukuliwa na Spika wa Azbeijan  Ms.Sahiba Gafarova  aliyepata kura 124 sawa na asilimia 38 na mgombea wa mwisho ni Spika wa Bunge la Chile Rojo Edward Silver aliyepata kura 21 sawa na asilimia 6.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Milton Dick, ameahidi kuimarisha demokrasia, amani na ushirikiano wa kimataifa, akiwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa umoja huo kwa kumwamini na kumpa dhamana ya kuongoza taasisi hiyo.

Amesema anapokea jukumu hilo kwa unyenyekevu na kutambua wajibu mkubwa aliopewa wa kuhakikisha kila taifa, bila kujali ukubwa wake, utajiri au ushawishi wake, linaheshimiwa na kupata nafasi ya kusikilizwa katika jukwaa la kimataifa.

"kuchaguliwa kwangu ni ukumbusho kwamba demokrasia, kuheshimiana na ushirikiano bado ni misingi muhimu katika kuunganisha mataifa na kutafuta majibu ya changamoto zinazolikabili dunia," amesema.

Dick amesema atafanya kazi kwa karibu na wajumbe wa mabunge kutoka mataifa mbalimbali ili kujenga mazingira ya mazungumzo, kuimarisha uelewano na kutafuta maeneo ya kukubaliana licha ya tofauti za kisiasa, tamaduni, lugha na imani.

Amesisitiza kuwa changamoto za dunia, ikiwamo mabadiliko ya tabianchi, haziwezi kutatuliwa na taifa moja au eneo moja pekee, hivyo zinahitaji ushirikiano wa pamoja, akitaja umuhimu wa kuzingatia mazingira magumu yanayokabili mataifa ya visiwa vya Pasifiki na nchi ndogo.

Amesema katika uongozi wake atahakikisha kuwa sauti za mataifa yote zinasikilizwa na maslahi yake yanazingatiwa, akieleza kuwa hakuna nchi inayopaswa kutengwa katika mijadala ya kimataifa kwa sababu ya ukubwa wake, utajiri au nafasi yake ya kijiografia.

Katika hatua nyingine, Dick ametangaza mpango wa utekelezaji wa siku 100 za kwanza za uongozi wake, akieleza kuwa ataanza mara moja kufanyia kazi vipaumbele vilivyowekwa kwa ajili ya kuimarisha utendaji na malengo ya taasisi hiyo.

Amesema IPU ilianzishwa kwa maono ya kujenga taasisi inayotumia mazungumzo kutatua tofauti badala ya kuendeleza migawanyiko, huku ikitetea demokrasia na kuhimiza amani katika mataifa mbalimbali duniani.

Ameahidi kuongoza kwa unyenyekevu, uadilifu na heshima, akisisitiza kuwa atakuwa tayari kusikiliza maoni ya wajumbe na kuweka mbele maslahi ya IPU pamoja na wananchi wanaowakilishwa na mabunge yao.

Dick amesema mabunge yana wajibu mkubwa katika kipindi hiki cha changamoto na kutokuwa na uhakika duniani, kwa kuwa wananchi wanategemea viongozi wao kulinda demokrasia, kuimarisha amani, kutetea uhuru na kujenga mazingira bora kwa familia na watoto.

Ameongeza kuwa jukumu la kuendeleza misingi hiyo si la kiongozi mmoja pekee, bali ni wajibu wa pamoja wa wabunge na viongozi kutoka mataifa yote yanayoshiriki katika IPU.

Amesema anaamini kuwa mambo yanayoyaunganisha mataifa ni makubwa kuliko tofauti zinazoweza kuyatenganisha, hivyo amewataka wajumbe kuendelea kushirikiana katika kujenga mustakabali wenye amani, usalama na maendeleo.

Katika kuhitimisha hotuba yake, Dick ameomba mwongozo na hekima katika kutekeleza majukumu yake mapya, akieleza dhamira yake ya kutumia nafasi hiyo kujenga madaraja ya ushirikiano na kuimarisha demokrasia kwa manufaa ya watu wote duniani.




MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetwaa tuzo ya Uhusiano Bora na Vyombo vya Habari Tanzania kwa mwaka 2026 (Best Media Relations in Tanzania 2026), katika tuzo za umahiri wa uhusiano wa umma na mawasiliano.

Tuzo hiyo imetolewa Oktoba 8, 2026, katika hafla ya Tuzo za Umahiri wa Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano (PR & Communications Awards), zilizoandaliwa na Chama cha Uhusiano wa Umma Tanzania (PRST).

Utambuzi huo unaakisi mchango wa TMDA katika kutumia vyombo vya habari kufikisha taarifa na elimu sahihi kwa umma kuhusu masuala ya dawa na vifaa tiba, pamoja na umuhimu wa mawasiliano yenye weledi na ufanisi.

Tuzo hizo hutolewa kila mwaka na PRST kwa kuzingatia kura za wadau mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuhamasisha ubora katika taaluma ya uhusiano wa umma na mawasiliano nchini.


Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesisitiza umuhimu wa kuhakikisha elimu ya uwekezaji inawafikia wananchi wote bila kujali hali zao za kimwili au uwezo wa kiuchumi, ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika masoko ya mitaji nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha kwa watu wenye ulemavu, Mkuu wa Uhusiano wa Umma wa CMSA, Charles Shirima, amesema kuwa kuwawezesha wananchi kupata maarifa ya kifedha ni hatua muhimu katika kuongeza akiba za ndani na kukuza uchumi jumuishi.

"kampeni hii ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Wawekezaji Duniani (World Investor Week), mpango wa kimataifa unaoratibiwa na Shirika la Kimataifa la Tume za Dhamana (IOSCO) kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu uwekezaji salama na wenye taarifa sahihi",amesema Shirima

Amesema kuhamasisha wananchi wengi zaidi kushiriki katika uwekezaji ni muhimu katika kujenga utajiri binafsi na kuimarisha uchumi wa taifa.

Shirima amesema kuwa CMSA imeshirikiana na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) kutoa mafunzo yatakayowawezesha washiriki kuelewa fursa mbalimbali za uwekezaji na namna ya kuzitumia kuboresha maisha yao.


"Mafunzo hayo yamejikita katika namna masoko ya mitaji yanavyofanya kazi, utaratibu wa kununua hisa pamoja na mbinu bora za kusimamia fedha binafsi",amesema Shirima

Aidha, Shirima amesema CMSA hutumia njia mbalimbali kufikisha elimu hiyo kwa wananchi, zikiwemo warsha za ana kwa ana, semina za mtandaoni na mitandao ya kijamii, huku makundi yanayolengwa yakijumuisha wanafunzi, walimu, viongozi wa maeneo na wananchi kwa ujumla.

Amesema lengo ni kujenga mazingira jumuishi ya uwekezaji kwa kuhakikisha wananchi wa makundi mbalimbali wanapata maarifa na fursa za kushiriki katika masoko ya mitaji.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa SHIVYAWATA, Jonas Mbago, amesema mafunzo hayo yamesaidia kurahisisha dhana za kifedha ambazo awali zilionekana kuwa ngumu kueleweka, huku yakiwafahamisha washiriki njia mbadala za kusimamia na kukuza akiba zao.

Mbago amesema watu wengi katika jamii wamekuwa na mazoea ya kuhifadhi fedha majumbani au kwenye akaunti za benki zenye riba ndogo, hali inayoweza kupunguza fursa za kukuza fedha zao.


“Mafunzo haya yametutambulisha katika njia mpya za uwekezaji zinazoweza kuboresha usalama wetu wa kifedha,” amesema, huku akiiomba Serikali kupanua programu kama hizo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi nchini.

Naye Mwenyekiti wa chama kinachowakilisha watu wenye 'Psoriasis', ugonjwa sugu wa ngozi unaosababisha kutokea kwa mabaka mazito yenye magamba, Dorothy Malechela, amesema wananchi wanapaswa kuachana na tabia ya kuhifadhi fedha bila kuzizalisha na badala yake kujifunza fursa za uwekezaji zinazodhibitiwa kisheria.

Amesema mipango sahihi ya kifedha inaweza kuwasaidia watu kukuza biashara zao, kuimarisha usalama wa kifedha na kufikia malengo yao ya muda mrefu.