Na Said Mwishehe,Michuzi Tv

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia (PPP Centre), David Kafulila ameeleza kuwa marekebisho ya sheria ya ubia yamefungua ukurasa mpya wa uwekezaji Tanzania, huku miradi 10 ikiwa imesainiwa tangu mwaka 2023.

Akizungumza leo Novemba 23,2026 katika semina ya siku mbili kwa wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia (PPP Centre), David Kafulila amesema mafanikio hayo ni hatua kubwa ikilinganishwa na kipindi cha miaka 13 tangu kuanzishwa kwa sheria ya ubia mwaka 2010, ambapo hakuna mradi wowote uliokuwa umesainiwa.

Amesisitiza mafanikio hayo yanatokana na maboresho ya mfumo wa ubia yaliyofanyika mwaka 2023, yaliyolenga kuimarisha ushiriki wa wawekezaji binafsi katika utekelezaji wa miradi ya umma.

“Mfumo huo umeanza kutoa matokeo kwa kuwezesha serikali kushirikisha wawekezaji wa ndani na nje katika miradi ya kimkakati, hatua inayosaidia kuongeza mitaji na kuharakisha maendeleo ya miundombinu.”

Ameongeza miongoni mwa miradi hiyo ni Kituo cha Usafirishaji na Uhifadhi wa Mizigo cha East Africa Logistics Centre kilichopo Ubungo, Dar es Salaam, ambacho kimehusisha uwekezaji wa kampuni ya China wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 300.

Pia amelitaja jengo kubwa la biashara eneo la Kariakoo lililojengwa na mwekezaji wa ndani.Miradi mingine ni uwekezaji katika shughuli za uendeshaji wa bandari na ushughulikiaji wa makontena, pamoja na mradi wa kuboresha Shirika la Reli Tanzania na Zambia (TAZARA), wenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 1.4.

Kafulila amesema miradi hiyo inaonesha umuhimu wa kutumia mitaji, utaalamu na teknolojia ya sekta binafsi katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, huku serikali ikipunguza utegemezi wa fedha za bajeti.

Katika kuimarisha uwezo wa kusimamia miradi hiyo, amesema idadi ya wataalamu wa ubia nchini imeongezeka kutoka watano hadi 265, hatua inayoongeza uwezo wa taasisi za umma kuandaa, kutathmini na kusimamia mikataba ya ubia.

Pia amesema Tanzania imepata nafasi ya tisa duniani na ya tatu barani Afrika, baada ya Afrika Kusini na Nigeria, kwa idadi ya wahitimu wa mafunzo ya kitaalamu ya ubia yanayotolewa kupitia programu ya APMG.

Amesisitiza mafanikio hayo yanaonesha juhudi za serikali katika kujenga rasilimali watu wenye ujuzi wa kuandaa na kusimamia miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Pia amesema bado kuna kazi kubwa ya kuongeza miradi ya ubia ili kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inatarajia sekta binafsi kuchangia asilimia 70 ya rasilimali zitakazohitajika katika utekelezaji wake.

Akizungumzia madhumuni ya semina hiyo kwa wahariri wa vyombo vya habari amesema imelenga kuwajengea uwezo wahariri kuhusu mfumo wa ubia ili waweze kuelimisha umma kuhusu fursa za uwekezaji na mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa.

Amewataka wahariri kuongeza ushirikiano na taasisi za serikali zinazotekeleza miradi ya ubia kwa kutoa taarifa sahihi na zenye kujenga uelewa, akisema hatua hiyo inaweza kuhamasisha taasisi nyingine kutumia mfumo huo.

Semina hiyo pia iliwashirikisha wawakilishi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), walioeleza mipango na mikakati yao ya kutumia mfumo wa ubia kutekeleza miradi iliyo chini ya mamlaka zao.

“Kituo cha Ubia kitaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma katika kujenga uwezo wa wataalamu na kuhamasisha maandalizi ya miradi mipya itakayowezesha sekta binafsi kushiriki zaidi katika maendeleo ya nchi.” 



-Rais Samia kufungua mkutano mkubwa wa afya ya mama na mtoto Novemba 25, pia kusaini mkataba mpya na wakuu wa mikoa


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

VIFO vitokanavyo na uzazi nchini vimepungua kwa asilimia 80 kutoka vifo 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 huku pia vifo vya watoto chini ya miaka mitano navyo vimeshuka kwa asilimia 36, kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000.

Takwimu hizo zimetolewa leo Novemba 23,2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dkt Ahmad Makuwani, alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Dkt Makuwani amesema mafanikio hayo yametokana na mikataba ya uwajibikaji kati ya Rais na wakuu wa mikoa. Mkataba wa kwanza ulisainiwa mwaka 2018 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya "Jiongeze Tuwavushe Salama" na ulihusu afya ya uzazi, mama na mtoto.

Wakati mkataba wa pili ulisainiwa mwaka 2022 na ulihusu lishe ambapo kwa pamoja mikataba hiyo imeongeza uwajibikaji wa viongozi wa mikoa nchini kote.

Akifafanua amesema moja ya mafanikio makubwa ni wodi maalum za watoto wachanga, ambazo zimeongezeka kutoka 14 mwaka 2018 hadi 438 mwaka 2025. Kwa mara ya kwanza, wizara imetoa takwimu za watoto waliohudumiwa kwenye wodi hizo.

Amesema watoto 71,000 walilazwa mwaka 2025, na wengine 91,000 kati ya Januari na Septemba 2026. "Tulikuwa hatufanyi vizuri huko nyuma kwa kukosa huduma za watoto wachanga," amekiri Dkt Makuwani.

Ameongeza huduma pia zimesogezwa karibu na wananchi. Kati ya mwaka 2015/16 na 2024/25, zahanati zimeongezeka kutoka 4,127 hadi 6,589, vituo vya afya kutoka 535 hadi 1,067, na hospitali za wilaya kutoka 77 hadi 194. Kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanapata huduma ndani ya kilomita tano kutoka makazi yao.

Kwa upande wa fedha na vifaa, amesema bajeti ya sekta ya afya imepanda hadi shilingi trilioni 3.7 mwaka 2026/27, kutoka Sh.trilioni 2.46 mwaka 2023/24. Pia upatikanaji wa dawa za afya ya uzazi, mama na mtoto umefikia zaidi ya asilimia 85 katika miaka mitatu iliyopita.

“Magari ya kubebea wagonjwa yameongezeka kutoka 540 mwaka 2021 hadi 1,113 mwaka 2026. Hospitali zinazosambaza hewa ya oksijeni zimeongezeka kutoka 4 hadi 44.”

Akieleza zaidi amesema mfumo wa rufaa wa kielektroniki wa m-Mama, ulioanzishwa mwaka 2020, umesafirisha wagonjwa 250,000 hadi Agosti 2026. Kati yao, asilimia 81 ni akina mama, asilimia 18 ni watoto wachanga, na asilimia moja ni mama na mtoto kwa pamoja.

Ameongeza kwamba huduma za dharura pia zinaratibiwa kupitia makundi ya mawasiliano ya kidijitali (telemedicine) ya halmashauri, mikoa na kanda.

Dkt Makuwani amesema mafanikio hayo hayakutokana na sekta ya afya peke yake. Vijiji vyote 12,318 vimeunganishwa na umeme, ambao ni muhimu wakati wa upasuaji na kuhudumia wagonjwa mahututi.

“Vijiji 10,779, sawa na asilimia 83, vinapata maji safi, hali inayosaidia kuzuia maambukizi. Barabara zinazopitika wakati wote zenye urefu wa kilomita 144,300 zimefupisha safari za rufaa.”

Dk.Makuwani amesema mwitikio wa wajawazito umeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2022. Wanaohudhuria kliniki mara ya kwanza sasa ni asilimia 86, kutoka 84. Wanaohudhuria angalau mara nne wamepanda kutoka asilimia 65 hadi 81.

Amesema wanaojifungulia vituoni ni asilimia 85, kutoka 81 huku akieleza chanjo ya tatu ya PENTA imefikia asilimia 96 na ya Surua-Rubella asilimia 94, viwango vilivyo chini kidogo ya zaidi ya asilimia 98 na asilimia 97 za mwaka 2022.

Mafanikio hayo yameipa Tanzania heshima kimataifa. Rais Samia Suluhu Hassan alipewa tuzo ya Goalkeeper ya Gates Foundation Februari 2025, na ni Kinara wa Umoja wa Afrika kwenye huduma za mama na mtoto.

Dkt Makuwani amesema heshima hiyo inawafanya wasaidizi wa Rais "kutembea kifua mbele" kwa kuonyesha umahiri wao barani Afrika.

Mkutano wa tatu wa afya ya uzazi, mama, mtoto na lishe utafanyika Novemba 25 hadi 27, 2026. Umeandaliwa na Wizara ya Afya, OWM-TAMISEMI na wadau wa maendeleo. Rais Samia ndiye mgeni rasmi wa ufunguzi.

Katika mkutano huo, Rais atasaini Mkataba wa Pili wa Uwajibikaji na wakuu wa mikoa.Pia atazindua ripoti ya hali ya vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto nchini. “Rais Samia atakabidhi wakuu wa mikoa Mpango wa Nne wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto kama kitendea kazi.”

Ajenda kuu ya mkutano ni kujipanga kufikia malengo ya mwaka 2030. Vifo vya uzazi vinatakiwa kushuka chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000. Vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinatakiwa kuwa chini ya 25 kwa kila vizazi hai 1,000. Vifo vya watoto wachanga vinatakiwa kuwa chini ya 12 kwa kila vizazi hai 1,000.

Dkt Makuwani ametumia mkutano huo kutoa rai kwa vyombo vya habari kushiriki kikamilifu katika mkutano huo, kuendelea kuelimisha jamii kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto, na kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya ili wapate huduma bora bila kuumia kifedha.





▪️ Apigia chapuo matumizi ya akili unde katika shughuli za tume za uchaguzi

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka tume za uchaguzi za nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutumia ipasavyo teknolojia, mitandao ya kijamii na akili unde (AI) katika kuboresha usimamizi wa uchaguzi na kuimarisha demokrasia katika ukanda huo.

Dkt. Mwigulu amesema matumizi ya teknolojia za kisasa yana nafasi kubwa katika kuboresha mawasiliano, kutoa elimu kwa wapiga kura na kusambaza taarifa zinazohusu michakato ya uchaguzi kwa wakati, akisisitiza umuhimu wa kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia hizo ikiwemo usambazaji taarifa potofu.

“Kwa kuwa uchaguzi ni zoezi lenye hamasa kubwa kwa jamii, taarifa zisizo sahihi zinaposambazwa kwa kasi zinaweza kuwa na athari hasi na hata kusababisha migawanyiko katika jamii, kuathiri taswira ya taasisi za uchaguzi na kupunguza imani ya wananchi katika michakato ya kidemokrasia," amesema Dkt. Mwigulu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba 23, 2026) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 28 wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi za Nchi Wanachama wa SADC (ECF-SADC), katika hoteli ya Hyatt Regency - The Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa siku tatu unajadili usimamizi wa uchaguzi katika zama za mitandao ya kijamii na namna ya kuimarisha wajibu wa taasisi za usimamizi wa uchaguzi katika ukanda huo, ambapo Dkt. Mwigulu amesema mitandao ya kijamii imekuwa chanzo muhimu cha taarifa kwa wananchi wengi, hususan vijana, kutokana na uwezo wake wa kusambaza habari kwa haraka.

Amezitaka tume hizo kuendelea kujenga uwezo katika matumizi ya akili unde (AI), akieleza kuwa teknolojia hiyo inaendelea kukua na kubadilika kwa kasi, hivyo ni muhimu kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zake na kutumia fursa zinazotokana na maendeleo yake.

“Ni vyema mkaweka mikakati ya kukabiliana na changamoto za matumizi yake na kuona namna ya kutumia fursa ambazo zinaweza kupatikana kutokana na kuimarika zaidi kwa mifumo yake,” amehimiza Waziri Mkuu.

Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa usimamizi imara wa uchaguzi ni msingi muhimu wa kukuza demokrasia na ustawi wa jamii, hivyo amezitaka nchi za SADC kuendelea kuimarisha mifumo ya uchaguzi inayozingatia sheria, kanuni na misingi ya kidemokrasia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania - Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema ushiriki wa Tanzania katika ECF-SADC tangu kuanzishwa kwake mwaka 1998 umeiwezesha nchi kupata fursa za kujifunza na kubadilishana uzoefu na tume nyingine za uchaguzi katika ukanda huo kwani ushirikiano huo umesaidia kuimarisha mifumo ya uchaguzi na kujenga uwezo wa taasisi za usimamizi wa uchaguzi.

Naye, Rais wa Jukwaa la ECF-SADC, Jaji Dkt. Manuel Pereira da Silva, amesema jukwaa hilo lina jukumu la kuimarisha uhuru, kutopendelea upande wowote na kukuza weledi wa taasisi za usimamizi wa uchaguzi katika nchi wanachama pamoja na kujifunza mbinu mpya za usimamizi wa uchaguzi na kujenga mahusiano ya kikazi hata katika vipindi ambavyo nchi hazipo kwenye uchaguzi.

Mkutano huo wa 28 wa ECF-SADC umewakutanisha viongozi mbalimbali wakiwemo wenyeviti, makamishna, wakurugenzi na watendaji wa tume za uchaguzi kutoka nchi wanachama wa SADC, ukiwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa uchaguzi, changamoto za teknolojia na nafasi ya mitandao ya kijamii katika michakato ya kidemokrasia.







MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba ametoa wito kwa walimu wanao shiriki mafunzo ya mbinu za ufundishaji wa somo la Kiingereza (Jolly Phonics) kutumia MEWAKA zao ili kuwafundisha walimu ambao hawajapata fursa ya kushiriki mafunzo hayo.

Ametoa wito huo kwa njia ya darasa janja (smart class) leo Novemba 23, 2026 wakati akifungua mafunzo hayo  yanayotarajia kufanyika katikati mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Ruvuma na Lindi ili kukuza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa lugha ya kiingereza.

Dkt. Komba amesema,  mafunzo hayo yatasaidia kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Kiingereza huku, akiwahimiza walimu kufuatilia mafunzo kwa makini na kuomba ufafanuzi wa ziada pindi itapohitajika.

“Naomba sana mfuatilie kwa makini mafunzo haya ili muweze kupata ujuzi utakaowasaidia kuwafundisha wanafunzi katika madarasa yenu. Hakikisheni mnajifunza vizuri ili msaidie wanafunzi wenu kuelewa zaidi,” amesema Dkt. Komba.

Poa, Dkt. Komba amewashukuru Jolly Futures kwa kushirikiana na TET katika kutoa mafunzo hayo, yanayoendeshwa kwa mfumo wa darasa janja, huku wakufunzi wa TET na Jolly Futures wakiwasaidia walimu ana kwa ana.

Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo Bi. Sheba Moyo amesema kuwa, mafunzo hayo ni muhimu kwa walimu ambapo itasaidia wanafunzi shuleni kuelewa zaidi somo la kiingereza na kuwataka walimu hao waendelee kujifunza zaidi kupitia jumuiya zao za ujifunzaji kama vile MEWAKA.

Mafunzo yameanza katika Mkoa wa Dar es Salaam na yataendelea katika mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mbeya.













Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Miao Deyu, amewasili nchini Novemba 23, 2026, kwa ziara ya kikazi inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China, kupitia majadiliano kuhusu masuala mbalimbali yenye maslahi ya pamoja kwa nchi hizi mbili.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Miao alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe akiwa ameambatana na  Viongozi wengine kutoka Tanzania na China, akiwemo Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Dkt. Suleiman Haji Suleiman na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian.

Wakati wa ziara hiyo, masuala yatakayojadiliwa ni pamoja na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Wang Yi, iliyofanyika mwezi Januari, 2026,  maendeleo ya mradi wa ukarabati na uboreshaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), pamoja na maeneo mengine ya ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia.

Aidha, ziara hiyo itahusisha mkutano wa utatu kati ya Tanzania, China na Zambia, utakaotoa fursa kwa nchi hizo kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mradi wa TAZARA, ikiwemo utekelezaji wake na nafasi yake katika kukuza biashara, usafirishaji na maendeleo ya uchumi wa kikanda.

Katika kuenzi urafiki na mshikamano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China, Mhe. Miao pia atatembelea makaburi ya wataalam wa China yaliyopo Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, kwa heshima ya raia wa China waliopoteza maisha wakati wa kushiriki ujenzi wa Reli ya TAZARA.

Vilevile, atashiriki warsha maalumu kuhusu TAZARA itakayofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Wilayani Kibaha, mkoani Pwani.

Ziara hiyo inatarajiwa kutoa fursa ya kuendeleza majadiliano kuhusu masuala ya kipaumbele kwa mataifa hayo mawili, kuimarisha ushirikiano uliopo na kuweka msingi wa utekelezaji wa mipango ya pamoja yenye manufaa kwa wananchi wa Tanzania, China na Zambia.

























Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka, ameitaka Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM) kuendelea kuzalisha wataalamu wenye ubunifu, uadilifu na uwezo wa kutatua changamoto zinazolikabili Taifa kupitia teknolojia na mifumo mbalimbali.

Dkt. Isaka amesema wataalamu wanaozalishwa na vyuo wanapaswa kuwa sehemu ya kutafuta suluhisho la changamoto za jamii kwa kutumia maarifa waliyonayo, ikiwemo kubuni mifumo inayorahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Amesema hayo wakati wa Kongamano la Kitaaluma la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza umuhimu wa wataalamu kuzingatia uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema pamoja na kuwa na ufaulu mzuri kitaaluma, mtaalamu anapaswa kuwa na maadili na kujitambua ili aweze kutumia ujuzi wake katika kutatua changamoto za wananchi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Jamii ina changamoto nyingi ambazo wataalamu wetu wanapaswa kuzitumia kama fursa za kuzitatua kwa kubuni teknolojia na mifumo mbalimbali itakayorahisisha maisha ya watu,” amesema.

Aidha, amesema mabadiliko ya teknolojia na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 yanatoa fursa kwa IFM kuboresha mitaala yake ili kuzalisha vijana wenye uwezo wa ubunifu, uzalishaji na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Amesema NHIF itatoa fursa kwa wanafunzi 10 bora wa mwaka wa tatu wa IFM kufanya mafunzo ya vitendo katika taasisi hiyo ili kuwajengea uzoefu wa kazi na kuwaandaa kwa fursa za ajira na kujiajiri.

Kwa upande wake, Mkuu wa IFM, Profesa Henry Chalu, amesema chuo hicho kitaendelea kuimarisha mifumo ya elimu inayozalisha wataalamu wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo ya nchi.
Amesema kongamano hilo ni sehemu ya mkakati wa chuo kuhamasisha tafiti na ubunifu unaolenga kutatua changamoto katika sekta mbalimbali, huku wanafunzi wakipata fursa ya kuwasilisha mawazo na mifumo waliyoibuni.

Profesa Chalu amesema chuo kinaendelea kusimamia misingi ya elimu inayowawezesha wanafunzi kutumia maarifa yao katika mazingira halisi ya kazi na kujibu mahitaji ya jamii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano hilo, Dkt. Shaban Ngole, amesema kongamano hilo limekuwa na mawasilisho mbalimbali yanayolenga kuonesha ubunifu wa wanafunzi na fursa zinazoweza kuwasaidia katika maisha yao ya kitaaluma na kiuchumi.

Amesema wanafunzi 10 wamepata nafasi ya kufanya mafunzo ya vitendo NHIF, hatua itakayowasaidia kuongeza ujuzi na uzoefu katika mazingira ya kazi.

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa IFM, Adrian Kachocho, amesema amebuni mfumo unaowasaidia wafanyabiashara kufuatilia mapato na matumizi ya biashara zao, hatua inayoweza kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi na kuboresha usimamizi wa biashara.