Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa uwekezaji mkubwa iliyoufanya katika teknlojia za elimu zinazorahisha ufundishaji na ujifunzaji wa walimu na wafaunzi nchini.

Pongeza hizo zimetolewa leo tarehe 08/10/2026 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Husna Sekiboko aliyeambatana na wajumbe wa kamati hiyo wallopofanya ziara ya kikazi katika makao makuu ya TET jijini Dar es salaam ili kujionea utendaji kazi unaoendelea katika taasisi hiyo.

“Tunawapongeza kwa hatua kubwa ya uandaaji wa mifumo mbalimbali inayorahisisha ufundishaji na ujifunzaji katika utekelezaji wa Mtaala ulioboreshwa ulioanza mwaka 2024,” amesema Mhe. Sekiboko.

Aidha, amesema katika kuelekea vikao vya Bunge kamati hiyo itaishauri Serikali kukaa na wadau wa kampuni za simu ili kuona namna gani inaondoa gharama za bando kwa ajili ya mifumo mbalimbali ili kuweza kutumika bila kikwazo kwa wanafunzi na walimu wote nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameishukuru kamati hiyo kwa maoni mbalimbali ya uboreaji wa elimu nchini waliyoyatoa na kueleza kuwa watafanyia kazi katika maeneo ambayo yameguswa ili kupatiwa ufumbuzi wa haraka kama walivyoshauri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba aliwasilisha taarifa ya utekelezaji miradi ya maendeleo, mafanikio na mahitaji ya Taasisi ambapo ameeleza utakelezaji wa shughuli mbalili zilizofanyika na namna TET ilivyoweza kujikita zaidi kwenye eneo la teknolojia inayosaidia ufundishaji na ujifunzaji nchini.

Amesema, teknolojia mbalimbali zilizopo kwa sasa ni pamoja na Maktaba mtandao (inayowezesha upatikani wa vitabu moja kwa moja), Open Public Shool (OpSchool), mfumo wa udhibiti ubora, mfumo wa Learning Management System (LMS).

DAR ES SALAAM

MAWAZIRI wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Msumbiji, Dkt. Rhimo Nyansaho na Cristóvão Artur Chume, wamehitimisha rasmi Mkutano wa Saba wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama kati ya nchi hizo mbili.

Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, umehitimishwa Oktoba 7, 2026, kwa kusainiwa kwa makubaliano mbalimbali yanayolenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa Tanzania na Msumbiji katika masuala ya ulinzi na usalama.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuendelea kuimarisha juhudi za nchi hizo mbili katika kulinda amani, utulivu na usalama wa wananchi, pamoja na kushughulikia kwa pamoja masuala yenye maslahi ya pamoja katika eneo la ulinzi na usalama.

Mkutano huo wa saba wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama pia ulilenga kuendeleza na kuimarisha maono ya waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Baba wa Taifa wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Hayati Samora Moisés Machel wa Msumbiji.

Viongozi hao waliweka msingi imara wa uhusiano wa kihistoria, kidugu na kimkakati kati ya Tanzania na Msumbiji, ambao umeendelea kudumishwa katika vipindi mbalimbali.

Maono hayo yanaendelea kuenziwa na viongozi wa sasa wa nchi hizo mbili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Chapo, kupitia kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.

Ushirikiano huo unatajwa kuwa sehemu muhimu ya kuendeleza amani, usalama na utulivu katika Tanzania, Msumbiji na ukanda wa kusini mwa Afrika

DAR ES SALAAM

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Uchumi na Fedha, Ndugu Jamal Kassim Ali, ameitaka CCM Mkoa wa Dar es Salaam kufanya tathmini ya mikataba na miradi ya chama, akisema baadhi ya mikataba iliyopo haina maslahi ya kutosha kwa chama.

Jamal ameyasema hayo leo, Oktoba 8, 2026, wakati akizungumza na Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam katika Ofisi Ndogo za CCM Lumumba, jijini Dar es Salaam.

Amesema ni muhimu kwa chama kupitia upya mikataba na miradi yake ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuhakikisha mali na rasilimali za CCM zinatumika kwa tija na kwa maslahi ya chama.

Aidha, amesema baadhi ya wawekezaji wamekuwa na mtazamo kwamba CCM ni “shamba la bibi”, akieleza kuwa hali hiyo imechangiwa na utaratibu wa muda mrefu ambao, kwa mujibu wake, chama kinapaswa kuufanyia marekebisho.

Jamal pia ameitaka CCM Mkoa wa Dar es Salaam kubuni vyanzo vipya vya mapato na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji yatakayosaidia kuimarisha uwezo wa chama kiuchumi.

Amesisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali za chama zinasimamiwa kwa ufanisi na kutumika katika kuimarisha shughuli na maendeleo ya CCM.

Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha

WASANII nchini wametakiwa kubadili mtazamo na kuanza kuzitazama kazi zao za sanaa kama biashara kwa kuzirasimisha, kusajili majina ya biashara na kulinda miliki bunifu ili kuongeza fursa za kukuza shughuli zao na ushindani katika soko.

Wito huo umetolewa na Msaidizi wa Msajili Mkuu, Mkurugenzi wa Miliki Bunifu kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Nassoro Mtavu, aliyewahimiza wasanii kutumia fursa zinazopatikana kupitia usajili na ulinzi wa kazi zao.

Mtavu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wadau wa sanaa katika Tamasha la Arusha Artisan Festival linaloendelea katika viwanja vya General Tyre, Njiro jijini Arusha.

Amesema BRELA imejipanga kuwasaidia wasanii kuelewa taratibu za usajili wa biashara pamoja na masuala ya majina ya biashara, alama za biashara na miliki bunifu yanayoweza kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya sanaa.

Amesema ushiriki wa BRELA katika tamasha hilo unalenga kutoa elimu kwa wasanii na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kurasimisha shughuli zao na kuhakikisha wanafanya biashara kwa kuzingatia matakwa ya sheria.

“Maonyesho haya yamekuwa fursa muhimu kwa wasanii na wafanyabiashara kupata elimu kuhusu namna ya kuendesha na kukuza shughuli zao kwa kuzingatia taratibu za kisheria,” amesema Mtavu.

Amesema wasanii wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuuliza maswali na kueleza changamoto zinazowakabili katika shughuli zao ili kupata majibu na ushauri kutoka kwa wataalamu wa BRELA.

Kwa mujibu wa Mtavu, baadhi ya changamoto zinazowakabili wasanii zinaweza kutatuliwa iwapo wataongeza uelewa kuhusu usajili wa biashara, majina ya biashara, alama za biashara pamoja na namna ya kulinda miliki bunifu.

Amesema usajili wa shughuli za sanaa unaweza kuwasaidia wasanii kuwa na utambulisho rasmi wa kibiashara na hivyo kuongeza uwezo wao wa kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana kwa wafanyabiashara waliosajiliwa.

Aidha, amesema ulinzi wa miliki bunifu ni muhimu kwa wasanii kwa kuwa kazi zao zinaweza kuwa na thamani kubwa kiuchumi na hivyo zinahitaji kulindwa dhidi ya matumizi yasiyoruhusiwa.

Mtavu amewataka wasanii kutumia mafunzo na huduma zinazotolewa na BRELA kama sehemu ya kujenga msingi imara wa biashara zao badala ya kutegemea kipaji pekee katika kuendesha shughuli zao.

Amesema msanii anayelinda kazi yake, anasajili shughuli zake na kuzingatia taratibu za kisheria ana nafasi kubwa ya kukuza thamani ya kazi zake na kufikia masoko mapana zaidi.

Ameongeza kuwa wasanii wanapaswa kutumia majukwaa kama Tamasha la Arusha Artisan Festival si kwa ajili ya kuuza na kutangaza kazi zao pekee, bali pia kujifunza namna ya kuzifanya kazi hizo kuwa biashara endelevu.

Amesema BRELA itaendelea kushirikiana na wadau wa sanaa kutoa elimu na kuwasaidia kuelewa huduma zinazotolewa na taasisi hiyo ili waweze kutumia ipasavyo fursa zilizopo.

Mtavu amewahimiza wasanii wengine ambao bado hawajar formalisha shughuli zao kuchukua hatua kwa kuanza mchakato wa usajili na kupata uelewa kuhusu namna bora ya kulinda kazi zao.

Amesema hatua hiyo itasaidia kujenga sekta ya sanaa yenye wasanii wanaoweza kutumia ubunifu wao kama chanzo cha ajira, kipato na biashara endelevu nchini.

Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha

TANZANIA imezindua Ajenda ya Kitaifa ya Maendeleo ya Mafundi na Uchumi wa Ubunifu, inayolenga kuweka mazingira bora kwa mafundi na wasanii kukuza shughuli zao, kufungua masoko mapya na kuchangia zaidi katika uchumi wa taifa.

Aidha kupitia ajenda hiyo, Tanzania inalenga kutengeneza zaidi ya ajira 600,000 na kuzalisha mapato ya dola za Marekani milioni 500 kwa mwaka ifikapo 2032.

Akizungumza katika uzinduzi wa ajenda hiyo jijini Arusha,Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania International Tourism Festival, Ibrahim Othman Jama, amesema ajenda hiyo ya miaka mitano inalenga kuunganisha sekta ya sanaa, utamaduni, biashara na utalii ili kuhakikisha kazi za mafundi na wasanii zinakuwa sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania.

Amesema ajenda hiyo imejengwa juu ya nguzo sita, ikiwemo kurasimisha, kusajili na kuweka mfumo wa kutambua mafundi na wasanii nchini, pamoja na kutumia teknolojia na mifumo ya kidijitali katika kukuza uchumi wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Jama, nguzo nyingine ni kufungua masoko mapya ndani na nje ya Tanzania, kulinda haki miliki za mafundi na wasanii pamoja na kuendeleza urithi wa vitendo na ubunifu unaotokana na tamaduni mbalimbali za Watanzania.

Amesema ajenda hiyo pia inalenga kuunganisha kikamilifu kazi za mafundi na wasanii katika uchumi wa utalii wa Tanzania, akisisitiza kuwa hadithi ya utalii wa Tanzania haiwezi kutenganishwa na hadithi ya ubunifu, sanaa na utamaduni wa Watanzania.

Jama amesema kupitia ajenda hiyo, Tanzania inalenga kusajili takribani mafundi 50,000, kuzalisha mapato ya dola za Marekani milioni 500 kila mwaka kutoka katika sekta hiyo na kutengeneza ajira 600,000 katika uchumi wa ubunifu ifikapo mwaka 2032.

Amesema malengo hayo pia yamezingatia usawa wa kijinsia na kuongeza nafasi za vijana kushiriki katika uchumi wa ubunifu, akieleza kuwa kundi hilo limekuwa likihitaji fursa zaidi za kuonyesha vipaji, kupata masoko na kujenga maisha kupitia kazi zao.

Ameeleza kuwa Tanzania International Tourism Festival ilianzishwa kwa lengo la kujenga majukwaa yanayokutanisha utamaduni, biashara na jamii, huku tamasha hilo likiwa sehemu ya utekelezaji wa dhamira hiyo kwa kuwaunganisha mafundi na wasanii kutoka maeneo mbalimbali nchini na wanunuzi, wawekezaji na wadau wengine.

Jama amesema zaidi ya wasanii na mafundi 100 wamepata nafasi ya kushiriki katika tamasha hilo, akibainisha kuwa thamani kubwa ya tukio hilo haiishii kwa washiriki waliopo Arusha bali inapaswa kuonekana katika mabadiliko ya maisha ya mafundi walioko vijijini na kwenye warsha mbalimbali nchini.

Amesema mafundi kama washonaji, wachongaji, wachoraji, wasusi na wanaofanya kazi za vyuma wamekuwa wakibeba historia na utamaduni wa Tanzania kupitia kazi zao, lakini mara nyingi hawapati kutambuliwa wala kulipwa kulingana na thamani ya kazi wanazozifanya.

Katika hatua nyingine, Jama ameiomba Serikali na wadau wa sanaa kuweka mifumo itakayowawezesha wasanii na mafundi kushiriki katika matukio ya kimataifa ili kupata fursa za kuonyesha kazi zao, kujenga mitandao ya kibiashara na kutafuta masoko nje ya Tanzania.

Amesema mabalozi na balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali zinaweza kuwa sehemu muhimu ya kufungua fursa hizo kwa kuwaunganisha wasanii na mafundi wa Tanzania na masoko ya kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa BASATA na taasisi nyingine za sanaa katika kuratibu fursa hizo.

Ameishukuru Serikali, Serikali ya Mkoa wa Arusha, viongozi wa Wilaya, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), COSOTA, Bodi ya Filamu, BRELA, taasisi za fedha, washirika wa maendeleo na wadau mbalimbali kwa kushirikiana katika kufanikisha tamasha hilo na ajenda hiyo.

Amesema katika kipindi cha siku tano za tamasha hilo, Arusha itakuwa mwenyeji wa maonesho ya sanaa, biashara, warsha, mikutano ya kibiashara kati ya wafanyabiashara na wawekezaji (B2B), pamoja na filamu na shughuli zinazolenga kuonyesha utamaduni wa Tanzania.

Jama ametoa wito wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wasanii, mafundi, taasisi za fedha na wadau wa utalii ili ajenda hiyo iweze kutekelezwa na kutoa fursa kwa Watanzania wengi zaidi, hasa vijana, wanawake na jamii zinazotegemea kazi za ubunifu kama chanzo cha kipato.

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa tamasha hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa za Ufundi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bona Leoni Masenge, amewataka vijana na wanawake nchini kutumia vipaji vyao katika sanaa na ubunifu kama fursa ya kujiajiri na kuongeza kipato, badala ya kuuchukulia ubunifu kama njia ya burudani pekee.

Masenge amesema sanaa na ubunifu vina uwezo wa kuzalisha ajira na kujenga biashara, hivyo vijana wanapaswa kutumia vipaji walivyonavyo kuanzisha shughuli zinazoweza kuwapatia kipato na kuchangia maendeleo ya familia na jamii.

Amesema mtu anayeshona nguo, kufuma, kuchonga, kuchora, kupaka rangi, kutengeneza bidhaa za ngozi, kufua chuma, kubuni mavazi au kuhifadhi mbinu za jadi za sanaa siyo fundi pekee, bali ni mjasiriamali, mbunifu na mtunzi wa utamaduni wa Tanzania.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amewasili katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 8, 2026, kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12).

Mkataba wa Nairobi unalenga kuimarisha uhifadhi, usimamizi endelevu na ulinzi wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani katika eneo la Magharibi mwa Bahari ya Hindi.

Mkutano huo ulioanza Oktoba 6, 2026, unatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 9, 2026, na unaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 40 ya Mkataba wa Nairobi, ulioanzishwa mwaka 1985.

Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika mkutano huo ni mikakati ya kukuza uchumi wa buluu kupitia uvuvi endelevu, kukabiliana na uchafuzi wa mazingira ya bahari na athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuimarisha uhifadhi wa bayoanuai za baharini na maeneo ya pwani.

Katika jitihada za kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini, Benki ya NMB imezindua Dawati Maalumu la Huduma kwa Wateja Wenye Ulemavu, likiwa na huduma ya mawasiliano ya video inayosaidiwa na wakalimani wa lugha ya alama, hatua inayolenga kuondoa vikwazo vya mawasiliano na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki kwa watu wenye ulemavu.

Dawati hilo lililoanzishwa katika Kituo cha Mawasiliano cha NMB litahudumia wateja wenye ulemavu wa kusikia, kuona na viungo. Wateja wanaweza kupata msaada kupitia namba ya simu ya bure 0800 002002, huduma ya video kupitia WhatsApp inayosaidiwa na wakalimani wa lugha ya alama, pamoja na matawi ya NMB nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema huduma hiyo inalenga kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata huduma za kibenki kwa heshima na usawa, huku wakilindwa faragha zao na kupunguziwa utegemezi wa watu wengine wanapohitaji msaada.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Nemes Temba, aliipongeza NMB kwa kuanzisha dawati hilo, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza vikwazo vya mawasiliano na kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika matumizi ya huduma za kifedha nchini.

Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha

TANZANIA imezindua Ajenda ya Kitaifa ya Maendeleo ya Mafundi na Uchumi wa Ubunifu, inayolenga kuweka mazingira bora kwa mafundi na wasanii kukuza shughuli zao, kufungua masoko mapya na kuchangia zaidi katika uchumi wa taifa.

Aidha kupitia ajenda hiyo, Tanzania inalenga kutengeneza zaidi ya ajira 600,000 na kuzalisha mapato ya dola za Marekani milioni 500 kwa mwaka ifikapo 2032.

Akizungumza katika uzinduzi wa ajenda hiyo jijini Arusha,Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania International Tourism Festival, Ibrahim Othman Jama, amesema ajenda hiyo ya miaka mitano inalenga kuunganisha sekta ya sanaa, utamaduni, biashara na utalii ili kuhakikisha kazi za mafundi na wasanii zinakuwa sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania.

Amesema ajenda hiyo imejengwa juu ya nguzo sita, ikiwemo kurasimisha, kusajili na kuweka mfumo wa kutambua mafundi na wasanii nchini, pamoja na kutumia teknolojia na mifumo ya kidijitali katika kukuza uchumi wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Jama, nguzo nyingine ni kufungua masoko mapya ndani na nje ya Tanzania, kulinda haki miliki za mafundi na wasanii pamoja na kuendeleza urithi wa vitendo na ubunifu unaotokana na tamaduni mbalimbali za Watanzania.

Amesema ajenda hiyo pia inalenga kuunganisha kikamilifu kazi za mafundi na wasanii katika uchumi wa utalii wa Tanzania, akisisitiza kuwa hadithi ya utalii wa Tanzania haiwezi kutenganishwa na hadithi ya ubunifu, sanaa na utamaduni wa Watanzania.

Jama amesema kupitia ajenda hiyo, Tanzania inalenga kusajili takribani mafundi 50,000, kuzalisha mapato ya dola za Marekani milioni 500 kila mwaka kutoka katika sekta hiyo na kutengeneza ajira 600,000 katika uchumi wa ubunifu ifikapo mwaka 2032.

Amesema malengo hayo pia yamezingatia usawa wa kijinsia na kuongeza nafasi za vijana kushiriki katika uchumi wa ubunifu, akieleza kuwa kundi hilo limekuwa likihitaji fursa zaidi za kuonyesha vipaji, kupata masoko na kujenga maisha kupitia kazi zao.

Ameeleza kuwa Tanzania International Tourism Festival ilianzishwa kwa lengo la kujenga majukwaa yanayokutanisha utamaduni, biashara na jamii, huku tamasha hilo likiwa sehemu ya utekelezaji wa dhamira hiyo kwa kuwaunganisha mafundi na wasanii kutoka maeneo mbalimbali nchini na wanunuzi, wawekezaji na wadau wengine.

Jama amesema zaidi ya wasanii na mafundi 100 wamepata nafasi ya kushiriki katika tamasha hilo, akibainisha kuwa thamani kubwa ya tukio hilo haiishii kwa washiriki waliopo Arusha bali inapaswa kuonekana katika mabadiliko ya maisha ya mafundi walioko vijijini na kwenye warsha mbalimbali nchini.

Amesema mafundi kama washonaji, wachongaji, wachoraji, wasusi na wanaofanya kazi za vyuma wamekuwa wakibeba historia na utamaduni wa Tanzania kupitia kazi zao, lakini mara nyingi hawapati kutambuliwa wala kulipwa kulingana na thamani ya kazi wanazozifanya.

Katika hatua nyingine, Jama ameiomba Serikali na wadau wa sanaa kuweka mifumo itakayowawezesha wasanii na mafundi kushiriki katika matukio ya kimataifa ili kupata fursa za kuonyesha kazi zao, kujenga mitandao ya kibiashara na kutafuta masoko nje ya Tanzania.

Amesema mabalozi na balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali zinaweza kuwa sehemu muhimu ya kufungua fursa hizo kwa kuwaunganisha wasanii na mafundi wa Tanzania na masoko ya kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa BASATA na taasisi nyingine za sanaa katika kuratibu fursa hizo.

Ameishukuru Serikali, Serikali ya Mkoa wa Arusha, viongozi wa Wilaya, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), COSOTA, Bodi ya Filamu, BRELA, taasisi za fedha, washirika wa maendeleo na wadau mbalimbali kwa kushirikiana katika kufanikisha tamasha hilo na ajenda hiyo.

Amesema katika kipindi cha siku tano za tamasha hilo, Arusha itakuwa mwenyeji wa maonesho ya sanaa, biashara, warsha, mikutano ya kibiashara kati ya wafanyabiashara na wawekezaji (B2B), pamoja na filamu na shughuli zinazolenga kuonyesha utamaduni wa Tanzania.

Jama ametoa wito wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wasanii, mafundi, taasisi za fedha na wadau wa utalii ili ajenda hiyo iweze kutekelezwa na kutoa fursa kwa Watanzania wengi zaidi, hasa vijana, wanawake na jamii zinazotegemea kazi za ubunifu kama chanzo cha kipato.

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa tamasha hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa za Ufundi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bona Leoni Masenge, amewataka vijana na wanawake nchini kutumia vipaji vyao katika sanaa na ubunifu kama fursa ya kujiajiri na kuongeza kipato, badala ya kuuchukulia ubunifu kama njia ya burudani pekee.

Masenge amesema sanaa na ubunifu vina uwezo wa kuzalisha ajira na kujenga biashara, hivyo vijana wanapaswa kutumia vipaji walivyonavyo kuanzisha shughuli zinazoweza kuwapatia kipato na kuchangia maendeleo ya familia na jamii.

Amesema mtu anayeshona nguo, kufuma, kuchonga, kuchora, kupaka rangi, kutengeneza bidhaa za ngozi, kufua chuma, kubuni mavazi au kuhifadhi mbinu za jadi za sanaa siyo fundi pekee, bali ni mjasiriamali, mbunifu na mtunzi wa utamaduni wa Tanzania.

Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania, Harriet Lwakatare, akichangia damu kwa ajili ya kuongeza akiba ya damu katika Benki ya Damu nchini na kusaidia kuokoa maisha ya watu wanaohitaji huduma hiyo. Zoezi hilo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026, inayoangazia umuhimu wa kuwahudumia wateja huku pia ikichangia ustawi wa jamii.

Mchango wa damu una umuhimu mkubwa katika kusaidia wagonjwa wanaohitaji damu wakati wa matibabu na huduma nyingine za dharura.

Tukio hilo limefanyika tarehe 7 Oktoba 2026, jijini Dar es Salaam, likiwa sehemu ya shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Vodacom Tanzania katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 yenye kaulimbiu “Zaidi ya Huduma ni Ukaribu!

Baadhi ya washiriki waliojitolea kuchangia damu kupitia zoezi lililoandaliwa na Vodacom Tanzania wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026, jijini Dar es Salaam. Zoezi hilo linalenga kuchangia kuongeza akiba ya damu katika Benki ya Damu Taifa na kusaidia kuokoa maisha ya watu wanaohitaji huduma hiyo.

Mmoja wa wateja wa Vodacom aliyejitolea kuchangia damu akifanyiwa vipimo vya afya kabla ya kuchangia damu wakati wa zoezi lililoandaliwa na Vodacom Tanzania Plc katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja. Tukio hilo limefanyika jana jijini Dar es Salaam, likiwa sehemu ya shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Vodacom Tanzania katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 yenye kaulimbiu “Zaidi ya Huduma ni Ukaribu!

Baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja baada ya tukio la uchangiaji damu wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja . Tukio hilo limefanyika jana jijini Dar es Salaam likiwa sehemu ya shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Vodacom Tanzania katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 yenye kaulimbiu “Zaidi ya Huduma ni Ukaribu”

Na Clement Sanga, Iringa

MKUU wa Wilaya ya Kilolo, Atupele Mwakibete, amewataka wakulima na wadau wa kilimo wilayani humo kuchangamkia fursa zinazotokana na zao la parachichi, akisema lina nafasi kubwa ya kuongeza tija na kipato kwa wananchi wa Nyanda za Juu Kusini.

Mwakibete ametoa kauli hiyo baada ya kushiriki Mkutano wa Tatu wa Wadau wa Zao la Parachichi uliofanyika jijini Dodoma, uliowakutanisha wadau mbalimbali kujadili mustakabali, mafanikio na mipango ya kimkakati ya kuendeleza kilimo cha zao hilo nchini.

Amesema kupitia mkutano huo alipata fursa ya kukutana na kubadilishana mawazo na wadau kutoka Halmashauri ya Busokelo mkoani Mbeya, akiwemo uongozi wa Kampuni ya Itecado Farm pamoja na Umoja wa Wakulima wa Parachichi Busokelo (UWAPABU).

Amesema majadiliano hayo yalilenga namna ya kuongeza tija, uzalishaji na ushirikiano miongoni mwa wadau katika kuendeleza kilimo cha parachichi.

Aidha, Mwakibete ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kwa mipango yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwemo kugawa miche bora ya parachichi, kukamilisha ujenzi wa vituo vya kukusanyia mazao na kuwawezesha vijana kupitia mpango wa BBT Ugani ili kuwafikia wakulima katika maeneo ya vijijini.

Amesema fursa hizo ni muhimu kwa wakulima wa Kilolo, hivyo amewataka wananchi na wadau wa kilimo wilayani humo kuzitumia kikamilifu kwa kuanzisha na kuendeleza kilimo cha parachichi kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kipato na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.