Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.
Ikiwa ni mwaka mmoja na nusu sasa tangu kufikishwa mahakamani kwa aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, (TRA) Harry Kitilya na wenzake wawili upande wa mashtaka umeieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa shauli hilo bado haujakamilika.
Kitilya pamoja na aliyekuwa miss Tanzania mwaka 1996, ambaye pia alikuwa Ofisa wa benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Graham Solomon ambao walifikishwa mahakamani hapo kwa Mara ya kwanza April 1, mwaka jana wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa USD Mil.6
Mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa kesi hiyo leo Novemba 3 ilifikishwa kwa ajili ya kutajwa ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi ameileza mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Alidai kuwa bado wanasubiri awamu ya pili ya upelelezi kutoka nchini Uingereza na kuomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi November 10, mwaka huu.
Katika kesi hiyo, washtakiwa wote wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya March 2013 na September 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola za Marekani 550 milioni kwa serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Uingereza.
Pia wanadaiwa kuwa March 2013 jijini Dar es Salaam walijipatia Dola za Marekani 6 milioni, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...