Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
WANANCHI wa Karakata Relini wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam wameiomba Serikali kuwasaidia ili kuepukana na maafa yanayoweza kutokea baada ya nyumba zao zaidi ya 300 kuzingirwa na maji.
Wananchi wa maeneo hayo wamesema kwa sasa hatma ya usalama wao umebaki mikononi mwa viongozi wa Wilaya ya Ilala hasa kwa kuzingatia maji hayo yamekosa pakupita kutokana na ujenzi wa reli unaondelea.
Wakizungumza na Michuzi Blog leo Mei 8, 2019 jijini Dar es Salaam wananchi hao wamesema maji yalianza kujaa katika nyumba zao kuanzia jana jioni na leo hii hali imekuwa mbaya zaidi kwani hakuna anayeweza kuingia ndani ya nyumba na baadhi ya watu wamekaa juu ya paa za nyumba kujinusuru.
Mmoja wa wananchi ambaye naye nyuma yake imejaa maji amesema baadhi ya wananchi wananchi wanachokifanya ni kujaribu kuyaondoa maji yaliyokuwa ndani ya nyumba lakini wameshindwa kuyaondoa kwani maji ni mengi.
"Jana wananchi tuliamua kuchukua majembe ili kwenda kuchimba mirefeji ya maji ambayo imezibwa kutokana na ujenzi wa reli. Hata hivyo Polisi walituzuia na kwa kuwa tunaheshimu mamlaka zilizopo, tunasubiri ingawa tuko kwenye wakati mgumu sana.Hatujui maisha yetu yatakuwa katika mazingira gani,"amesema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Karakata Kennedy Simioni amesema jana jioni walipata taarifa kuhusu nyumba hizo kujaa maji ambazo ni zaidi ya 300.Pia Kanisa la Anglikaa na Msikiti nayo imezingiwa maji.
"Baada ya taarifa hizo mimi na Mwenyekiti wangu wa Mtaa Olutu tulikwenda eneo hilo na kwa kweli hali ni mbaya sana.Hivyo kwa siku ya jana tulichukua hatua kwa kuwasiliana na mamlaka zote zinahusika ikiwemo Kamati ya maafa ya Wilaya.
"Pia tumewasiliana na wahandisi wa Manispaa ya Ilala pamoja na Kampuni inayojenga reli ya kisasa.Lengo letu ni kupata ufumbuzi kwani kabla ya ujenzi wa reli maji yalikuwa yanakwenda vizuri lakini baada ya ujenzi kuanza maji yamekosa njia ya kupita kama zamani,"amesema Simioni.
Diwani Simioni amesema wamekwenda Wakala wa Ujenzi wa Barabara TARURA kutoa taarifa na wakaambiwa waandike barua na wakafanya hivyo na walishaiwasilisha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...