Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza Mawaziri wa Tanzania kuitisha kikao cha Kamati ya Pamoja ya Tanzania na Namibia (Joint Permanent Commission – JPC) ndani ya kipindi cha miezi 2 ili kujadiliana juu ya fursa mbalimbali za ushirikiano wenye manufaa kwa nchi hizo.

Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 27 Mei, 2019 wakati wa mazungumzo rasmi kati yake na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Hage Geingob yaliyofanyika katika Ikulu ya Windhoek nchini Namibia ambako ameanza Ziara Rasmi ya Kitaifa ya siku 2 nchini humo.

Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo baada ya yeye na Mhe. Rais Geingob kupokea taarifa kuwa kikao cha JPC hakijafanyika tangu mwaka 1999 na kusababisha masuala mengi yakiwemo ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kutopata msukumo wa kutosha.

Amebainisha kuwa licha ya uhusiano wa kihistoria na kidugu wa Tanzania na Namibia ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Namibia Mhe. Sam Nujoma, nchi hizo zimekuwa na kiwango cha chini cha ushirikiano wa kibiashara baina yake ambapo katika mwaka uliopita biashara iliyofanyika ilikuwa na thamani ya shilingi Bilioni 59.556 tu na kwamba nchini Tanzania kuna kampuni 2 tu za Namibia zinazofanya biashara.

Pamoja na kutoa maagizo hayo Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Geingob kwa kumualika kufanya Ziara Rasmi ya Kitaifa nchini Namibia na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wowote unaohitajika ikiwemo kushirikiana katika masuala ya kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii, usafiri wa anga, biashara, uwekezaji, utamaduni na kufundisha lugha ya Kiswahili ambacho baadhi ya nchi za Afrika zimeridhia kianze kufundishwa katika shule zake.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema kwa kutambua uhusiano wa kihistoria na kidugu, Tanzania inakamilisha maandalizi ya kufungua Ubalozi wake Jijini Windhoek ili kurahisisha masuala mbalimbali ya uhusiano, hususani katika uchumi ambayo yapo nyuma.

Kwa upande wake Mhe. Rais Geingob amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kufanya ziara hiyo na amesema Namibia inatambua na kuenzi mchango mkubwa wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Nyerere na Watanzania katika juhudi za ukombozi wa Namibia.

Amefafanua kuwa wakati wa kupigania uhuru wa Namibia, wapigania uhuru wa Namibia walipata nafasi ya kuweka kambi yao huko Kongwa Mkoani Dodoma ambako licha ya kupiga kambi walisaidiwa kupata mafunzo ya kijeshi na waliishi vizuri na wananchi wa eneo hilo jambo ambalo hawatasahau.

Mhe. Geingob ameungana na Mhe. Rais Magufuli kusisitiza umuhimu wa kutekeleza makubaliano yatakayowekwa katika kikao cha JPC na kwamba Namibia ipo tayari kuyatekeleza kwa maslahi ya Wanamibia na Watanzania.
Kabla ya kufanya mazungumzo rasmi, Mhe. Rais Magufuli amefanyiwa mapokezi rasmi ambapo amepigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi liliandaliwa kwa heshima yake katika viwanja vya Ikulu Jijini Windhoek.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli ametoa zawadi ya vitabu vya kusoma na kufundishia lugha ya Kiswahili na amemhakikishia Mhe. Rais Geingob kuwa Tanzania ipo tayari kutoa walimu na vitabu vya kufundishia Kiswahili nchini Namibia.

Nyakati za jioni Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Geingob wamefungua rasmi mtaa mkubwa uliopo katikati ya Jiji la Windhoek ambao umebadilishwa jina na kupewa jina la Julius K. Nyerere ikiwa ni kuenzi mchango wake mkubwa katika ukombozi wa Namibia na Bara zima la Afrika.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mtaa huo Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Namibia Mhe. Dkt. Geingob na Wanamibia wote kwa heshima hiyo na ameeleza kuwa Watanzania wanajisikia faraja kuona Namibia inatambua mchango mkubwa wa Hayati Mwl. Nyerere na Watanzania katika ukombozi wa nchi yao.

Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa Hayati Mwl. Nyerere alikuwa kiongozi shupavu, aliyepambana na ukoloni, ubaguzi wa rangi na kupigania usawa, na ametoa wito kwa viongozi wa Afrika kumuenzi Hayati Mwl. Nyerere na viongozi wengine wa Afrika waliotoa mchango mkubwa wakati wa ukombozi kwa vitendo.

Meya wa Jiji la Windhoek, Mhe. Muesee Kazapua amesema Namibia imeamua kulipanga upya Jiji hilo na kubadili majina yote ya mitaa na kuyapa majina ya viongozi wa Afrika waliotoa mchango mkubwa katika ukombozi na maendeleo, na kwamba mtaa uliopewa jina la Julius K. Nyerere unaungana na mitaa mitatu yenye majina ya viongozi waliotoa mchango mkubwa katika ukombozi ambao ni Robert Mugabe, Jan Jonkerweg na Mandume Ndemufayo.

Katika hafla hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Philip Mangula na Mtoto wa Baba wa Taifa Ndg. Makongoro Nyerere ambaye katika salamu zake kwa niaba ya familia ameishukuru Namibia kwa kuendelea kumuenzi na kumpa heshima Hayati Mwl. Nyerere na kwamba wanafamilia wanapokea heshima hiyo kwa umuhimu mkubwa.

Jioni hii, Mhe. Rais Magufuli amehudhuria Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Geingob kwa heshima yake. Hafla hiyo imehudhuriwa na Mke wa Rais wa Namibia Mhe. Mama Monica Geingos, Rais Mstaafu wa Kwanza wa Namibia Mhe. Sam Nujoma na Rais Mstaafu wa Pili wa Namibia Mhe. Hifikepunye Pohamba.

Kesho, Mhe. Rais Magufuli atamaliza Ziara Rasmi ya Kitaifa nchini Namibia ambapo atatembelea kiwanda cha Nyama kilichopo Jijini Windhoek na kisha ataondoka kwenda nchini Zimbabwe ambako atafanya Ziara Rasmi ya Kitaifa kwa mwaliko wa Rais wa Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa.
  
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Windhoek
27 Mei, 2019
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifunua kitambaa na mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob kuashiria uzinduzi rasmi wa mtaa Julius K. Nyerere ulipo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob alipokuwa akimuonyesha Makongoro Nyerere mtoto wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mtaa mpya unaoitwa JULIUS K. NYERERE uliopo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019. 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi na mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob mara baada ya kuzindua mtaa mpya wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere unaoitwa JULIUS K. NYERERE uliopo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipongezana na mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob mara baada ya kuzindua mtaa mpya wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere unaoitwa JULIUS K. NYERERE uliopo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019

 Mtaa mpya wenye jina Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere unaoitwa JULIUS K. NYERERE ukifunuliwa rasmi mara baada ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia. Mei 27, 2019
 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimweleza Mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob alichokiandika kwenye kitabu cha kumbukumbu kwa Lugha ya Kiswahili Katika kuhakikisha Kiswahili kinatangazwa kimataifa mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Jijini Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019.
 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifurahi na mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob wakati wa hafla ya kuzindua mtaa mpya wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere unaoitwa JULIUS K. NYERERE uliopo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia. Mei 27, 2019 

Picha namba 9  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwapongeza Watanzania wanaoishi Namibia mara baada ya kuzindua mtaa mpya wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere unaoitwa JULIUS K. NYERERE uliopo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019.PICHA NA IKULU

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...