Rais wa Jamhuri ua Muungano wa Tanzania,Dkt John Pombe Magufuli
UTANGULIZI
HIVI karibuni, kumekuwa na mfumko mkubwa wa wananchi kuwa na hamu ya kuijua siasa ya nchi yao nchini Tanzania. Hamu hii imetokana na
matukio mbalimbali ya mabadiliko yaliyoletwa na kimbunga cha serikali
ya awamu ya tano ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli katika sekta
mbalimbali ikiwemo maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ambayo
yamewagusa wananchi wengi.
Kutokana na mabadiliko haya nchini, wananchi wengi wamebaki kujiuliza ni nini kinachoendelea nchini, tupo wapi, tunatoka wapi na tunaelekea wapi. Wakati huohuo, wazee kwa vijana, wanalalamika mmomonyoko wa maadili katika jamii, uchumi ‘kukaza kwa vyuma’ na hali ya kisiasa nchini.
Kwa hivyo, ni vyema kwa wanafunzi, walimu, na wananchi ambao siyo wanasiasa na wanasiasa kwa ujumla wao – kujikumbusha itikadi zao za kisiasa zinazowaongoza ili waweze kubaini na kupambanua mambo yanayowagusa katika jamii zao nakatika uchumi wa taifa lao kutokana na itikadi za siasa.
Makala hii nimeigawa sehemu tatu: sehemu ya kwanza nitafafanua na
kudadavua maana ya itikadi ya siasa; sehemu ya pili nitaelezea itikadi
za vyama vya siasa vilivyomo nchini na vyama vinavyofuata itikadi
hizo; na sehemu ya tatu nayo nimeigawa katika sehemu tatu kwenye kila
itikadi ya siasa: nitachambua na kudadavua mtazamo wa uchumi, siasa na
jamii.
Madhumuni ni kutoa mchango wangu kwa taifa, na siyo kwa nia ya
kukebehi wengine wenye elimu zaidi yangu au wasio na elimu. Mheshimiwa
Rais John Pombe Magufuli amesema: “Definition ya mtu aliyepata
education, ni yule aliyepata education… iwe ni formal au informal,
akaitumia kwenye different environment, ku-solve matatizo ya pale“
(Magufuli, 2019). Nami nitaendelea kujielimisha ‘kwa kadiri ya uwezo
wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote’.
Matarajio ni kwamba mwisho wa makala hii, wananchi wataelewa na wataweza kupambanua tofauti za itikadi za kisiasa na mambo yanayohusu siasa kwa kutumialenzi ya itikadi za siasa. Na hatimaye, wananchi wa kawaida, viongozi, walimu na wanafunzi ambao ndiyo taifa la kesho wataendelea kufanyamaamuzi sahihi katika kuisaidia nchi na kuisaidia jamii iliyowazunguka. “…bila ya kuwa na mtazamo sahihi, taasisi zinaweza kupotezwa muelekeo wa madhumuni yake ya kweli”. Mwalimu Nyerere, 1968
ITIKADI ZA KISIASA
Neno ‘itikadi’, limetokana na mwanazuoni wa Kifaransa aliyetambulika
kwa jina la Antoine Destutt de Tracy (1754-1836), ambaye mwishoni mwa
karne ya 18 mpaka mwanzoni mwa karne ya 19 alikuwa akifanya utafiti wa
kutaka kujua chanzo cha ‘fikra’ za watu katika maisha yao.
Yaani, kwanini watu wanakuwa na mawazo ya kufanya maamuzi juu ya mambo mbalimbali. Na hapo ndipo neno ideology (itikadi) lilipozaliwa. Kwa
maana hiyo, neno itikadi (ideology) linamaanisha kuwa ni somo la
kisayansi linalosomea mawazo (ya kifikra) ya watu (Ball & Dagger,
1991, uk. 4).
Ufafanuzi wa neno itikadi kama linavyofafanuliwa na bwana Ball &
Dagger (1991), linamaanisha kuwa ni mawazo na fikra ambayo yanaelezea
na yanatathmini hali ya kijamii, na kuisaidia jamii ijitambue ilipo na
kuipangia mpango bora wa utekelezaji wa sera za kijamii na za kisiasa:
“An ideology is a… set of ideas that explains and evaluates social
conditions, helps people understand their place in society, and
provides a program for social and political action.” (Ball & Dagger,
1991, uk. 8).
Kwa maana hiyo, itikadi ni mkusanyiko wa mawazo ya kifikra
yanayotokana na imani ya dhati inayoitazama hali ya kijamii ilivyo na
jinsi inavyotakiwa iwe kwa kutoa muongozo na muelekeo maalum wa
kisiasa na wa kijamii ili kufikia malengo ya kuiona jamii hiyo
inavyotakiwa iwe katika hali zao za kimaisha. Muongozo na muelekeo huo
ndiyo unaotengeneza itikadi ya watu, na itikadi ya watu ndiyo inawapa
watu muongozo na muelekeo wa kuufuata.
Itikadi zinaweza kufanya watu wawe wamoja na itikadi zinaweza kuwagawa
watu katika makundi. Tofauti za kiitikadi zinaweza kuleta madhara na
pia zinaweza kuleta umoja, upendo, mshikamano na amani.
Kwa kuwa sera za itikadi zinachukua hatua za kuifanyia kazi jamii, na kwa kuwa itikadi mbalimbali zinatofautiana kifikra, siyo ajabu tukiona itikadi
zikigongana mara kwa mara na hata mara nyingine hupelekea mpaka watu
wanaotoka sehemu moja au wa taifa moja kufanyiana uhasama, fitna,
chuki na uadui.
Sifa za uhasama, fitna, chuki na uadui zikitumika kama
ndiyo nyenzo katika kujenga jamii, jamii hiyo itakuja kuchuma
ilichokipanda. Kwasababu sifa hizo zitajifinyanga kwenye itikadi zao.
Kuijenga jamii iliyogawika na kuiweka kwenye jamii yenye umoja,
upendo, mshikamano na amani, inategemea sana msingi wa historia ya
watu walipotoka na siyo historia ya machimbuko ya pale walipogawanyika
kifikra. Taifa letu lipo njia panda. Ni muhimu kufanya maamuzi sahihi
ya kuamua wapi tunataka kwenda kwa kuangalia itikadi ipi itaweza
kutufikisha huko kama taifa – na kwa kuangalia wapi tulipo na wapi
tunatoka.
Kwa mfano, Tanzania msingi wa historia yake ni nchi ya
itikadi ya ujamaa. Hapa tulipo taifa letu la Tanzania limegawika
katika itikadi za kisiasa kuu tatu tangu kuanzishwa kwa siasa ya vyama
vingi mwaka 1992 – baada ya kuingiliwa na sera za kimagharibi miaka ya
‘80.
Zaidi ya miaka ishirini imepita tangu siasa ya vyama vingi ianze. Watu
wa nchi yetu wamekuwa bado wapo katika hali duni, na usawa wa kipato
unazidi kudidimia. Hii ukitoa miaka ya serikali ya awamu ya tano ya
Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ambaye bado hajatimiza hata miaka minne madarakani.
Na ninamaanisha kwamba athari za sera za kimagharibi
zilizoingia miaka ya ‘80 ndizo zilizoathiri awamu zilizopita kuanzia
awamu ya Alhajj Ali Hassan Mwinyi rais wa awamu ya pili, Mheshimiwa
Benjamin Mkapa rais wa awamu ya tatu na Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete rais wa awamu ya nne.
Halikadhalika, simaanishi kwamba matokeo
ya watu wetu wengi kuendelea kuwa na hali duni yametokana na viongozi
wetu waliopita, bali namaanisha kwamba yametokana na sera za
kimagharibi ambazo ‘kwa upande mwingine’ tunaweza kusema zilikuwa nje
ya uwezo wao kuzikabili. Tutakuja kuona huko mbele tunamaanisha nini.
Siamini kwamba taifa kuwa na vyama vingi ndiyo maendeleo ya nchi. Kuna
baadhi ya nchi barani Afrika zina vyama zaidi ya hamsini kwenye nchi
moja lakini watu wetu katika bara la Afrika ndiyo kwanza wanaendelea
kuwa maskini na hata matarajio ya kuwa na mustakbali wa ustawi ni
mdogo sana.
Pamoja na hayo, mara kwa mara hutokea matukio ya
changamoto ya vyama kwa kupoteza malengo ya maendeleo ya miradi ya
wananchi, kupiga majungu, na kuwa na mdomo mpana – kuliko muda huo
kutumika kwenye kuleta ustawi na maendeleo ya nchi na wananchi.
Kwa upande mwingine, ukiangalia nchi mfano wa Marekani (USA) tangu
ipate uhuru wake zaidi ya miaka mia mbili iliyopita mpaka hii leo
imeendeshwa na vyama viwili tu (Republicans na Democrats).
Halikadhalika, nchi ya China tangu ijipatie uhuru wake takriban miaka
sabini iliyopita mpaka hii leo imejiendesha yenyewe mpaka kufikia
malengo yake ya kimaendeleo kwa kupitia chama kimoja tu (Communist
Party of China).
Hii leo, nchi mbili hizi ndiyo nchi katika nchi
tajiri duniani, na ndiyo nchi katika nchi zenye nguvu duniani. Ingawa
ufafanuzi wa neno ‘maendeleo’ baina ya nchi na nchi unaweza
ukatofautiana, lakini hatuwezi kusema kwamba hawajapiga hatua kubwa
sana duniani pamoja na kuwa na vyama vichache au chama kimoja katika
kufikia malengo yao ya maendeleo.
Na la zaidi, vyama vya kisiasa vya
nchi zote hizi mbili, Marekani na China, vina itikadi mbili tofauti,
na kijiografia nchi zao zipo katika pande mbili tofauti za dunia,
lakini zote zimeweza kufikia malengo yao ya kimaendeleo. Kwa maelezo
haya nakusudia kusema kwamba, kuwa na vyama vingi siyo hoja. Hoja ni
kujitambua wapi tulipo, wapi tunatoka, wapi tunataka kuelekea, na
‘itikadi’ ipi itakayotuwezesha kufika huko kama taifa.
Kutokana na ufafanuzi wa neno itikadi hapo juu, tumeona kwamba ili
jamii iweze kujitambua wapi inaelekea, lazima itambue inafuata itikadi
ipi katika kufikia maendeleo yake. Itikadi ni imani, na itikadi ni
msingi wa maendeleo, bila ya kuwa na msingi madhubuti wa itikadi jamii
yetu itayumba, na kuyumba kwa jamii “…nchi yetu itayumba” (Nyerere,
1990).
Kwa mfano, chama cha siasa, hakiwezi kuwa chama madhubuti iwapo
msingi wake ni itikadi ya kijamaa kisha kiwe kinatekeleza sera za
itikadi ya kiliberali. Halikadhalika, chama chenye kufuata itikadi ya
kiliberali hakiwezi kuwa madhubuti iwapo msingi wake ni itikadi ya
kiliberali kisha kigeuke kiwe kinatekeleza sera za itikadi ya kijamaa.
Itikadi ni roho ya chama, itikadi ni chombo cha safari, lakini pia
itikadi ni mfano wa moyo, bila ya kuwa na moyo wenye afya madhubuti,
mwili utakumbwa na maradhi ya mara kwa mara. Chama cha siasa na
uongozi wa chama cha siasa hauwezi kuwa na itikadi mbili kwa wakati
mmoja. Waswahili wamesema “Mwenda tezi na omo, marejeo ngamani”.
Itikadi ya kisiasa haiendeshwi kwa muongozo wa nje ya itikadi yenyewe.
Chama au nchi isiyofuata itikadi inaweza ikaelekea pabaya. Wanasayansi
bwana Ball & Dagger (1991) kwenye maandishi yao wamesema, kama
tunataka kutenda mambo yetu kwa ufanisi na kuishi kwa amani, lazima
tujue maana ya itikadi za kisiasa ambazo zimetushawishi sisi na
zimeshawishi wengine fikra zao na matendo yao: “If we wish to act
effectively and live peacefully, then, we need to know something about
the political ideologies that have influenced so profoundly our own
and other people’s political attitudes and actions” (Ball & Dagger,
1991, uk. 3).
Siasa ni sayansi: ni njia ya kufikia malengo. Siasa siyo sayansi ya
moja na moja ni mbili. Siasa ni kukabiliana na hali na changamoto za
kila siku zinazojitokeza ambazo za jana huwa siyo sawa na za leo
katika masuala ya wananchi na taifa. Siasa ni kupinduka na siyo
kupindukia.
Chama cha siasa na uongozi wa chama cha siasa hauwezi
ukalala leo na imani ya itikadi moja, kisha kesho kuamka na itikadi
nyingine. Kwasababu hatari yake ni kwamba hatujui kesho kutwa wataamka
na itikadi ipi. Na hii siyo afya kwa uongozi wa nchi na siyo afya kwa
wananchi wanaoongozwa.
Ni muhimu kuwa wawazi katika maslahi ya taifa ili tuweze kusaidiana
kama watu wa taifa moja. Kwasababu sisi Watanzania kiasili tunapendana
kama ndugu na tunalipenda taifa letu. Mheshimiwa Rais Magufuli (2018)
kwenye hotuba yake alipokuwa jijini Mwanza katika utiaji wa saini wa
mkataba wa meli mpya, chelezo na ukarabati wa meli ya MV BUTIAMA na MV
VICTORIA, alisema: “…tunatakiwa tuzivae challenge …kwa wakati huu
nitawaambia ukweli …na ukweli saa nyingine unauma, lakini baadaye
ukweli hufurahisha” (Magufuli, 2018).
Pamoja na kuwepo kwa itikadi mbalimbali za kisiasa duniani, lakini
itikadi kuu tatu ndiyo zinazotawala dunia hivi sasa: Ujamaa
(Socialism), Uliberali (Liberalism), na Uhafidhina (Conservatism).
Katika sehemu hii ya makala, tutaangalia kwa kuchambua, kudadavua na
kukosoa hitilafu za itikadi za vyama vya siasa viliopo nchini. Vyama
vinavyofuata itikadi hizo ni kama ifuatavyo:
Chama cha CUF, kinafuata itikadi ya Uliberali (Liberalism);
Chama cha CHADEMA, kinafuata itikadi ya Uhafidhina (Conservatism);
Chama Cha Mapinduzi (CCM), NCCR na ACT, vinafuata itikadi ya Ujamaa (Socialism).
“Msipotambua historia yenu, mtaingiliwa na wanafiki, waongo,
watawapoteza muelekeo – mwenye kusikia na asikie”. Rais John Pombe Magufuli, 2019
Imeandikwa na:
Saleh J. Katundu
20/06/2019
Itaendelea…
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...