Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeshauri wakulima wasifanye kilimo cha zamani na badala yake watumie maabara yao kwa kupima udongo ili kuzalisha mazao yenye mahitaji ya kimataifa.
Imefafanua kwamba mazao yanapouzwa kimataifa lazima yawe yamekidhi viwango vya ili kuendana na soko la kimataifa.
Ushauri huo umetolewa leo kwenye Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea Sabasaba jijini Dar es Salaam na Ofisa Masoko na Mawasiliano wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Cletus Reuben Mnzava
Mnzava amesema kuwa ni wakati muafaka kwa wakulima nchini kuitumia mamlaka hiyo kwa lengo la kulima kilimo chenye tija na kwamba kwa kutumia maabara ya mkemia mkuu wa Serikali kupima udongo.
"Tunawashauri wakulima nchini kuhakikisha wanatumia maabara ya mkemia mkuu wa serikali kupima udongo kabla ya kupanda mbegu za mazao.Tunahitaji kuona wakulima wanapata mazao yaliyobora," amesema Mnzava.
Ametumia nafasi hiyo pia kueleza kuwa kwa wanaokwenda maonesho ya Sabasaba wafike kwenye banda la Mamlaka hiyo kwani kuna mambo mengi ya kujifunza ambayo wameyaandaa kwa ajili ya wananchi wote.
Ameyataja baadhi ya mambo ambayo wameyaandaa kwa ajili ya wananchi ni pamoja na kueleza namna wanavyopima vinasaba vya binadamu na masuala ya ubora wa bidhaa.
Pia usimamizi na udhibiti wa kemikali na kufafanua wale wote wanaojihusisha na mnyororo wa majukumu yao watapatiwa maelezo mazuri kwa lengo la kuhakikisha shughuli wanazozifanya zinakuwa na tija kwa maendeleo ya viwanda nchini Tanzania.
Alipoulizwa kwa mwananchi mmoja wananufaika vipi na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali amesema kuna faida nyingi na baadhi ya faida ni ubora wa bidhaa kwani mamlaka inafanya uchunguzi kwa niaba yao kuchunguza ubora wa bidhaa.Pia wanasaidia katika namna bora ya kufanya kilimo pamoja na biashara kwa mfano za asali na mazao yanayosindikwa.
Pia wanasaidia katika ujasiriamali mdogomdogo hasa wa kutumia kemikal katika kutengeneza batiki na faida nyingine wanasaidia kwa kuelimisha umma kuhusu ubora wa nafaka na namna ambavyo zinatakiwa kutunzwa.
"Pia tunasaidia katika kuwaeleza namna nzuri ya kutumia kemikali bila kudhurika.Ujumbe wetu kwa wananchi waje kwenye banda letu kwa ajili ya kuwapatia elimu ya uchunguzi wa kisayansi wa maabara kwa ajili ya afya mazingira pamoja na maendeleo endelevu ya viwanda nchini Tanzania," amesema Mnzava.
Ofisa Masoko na Mawasiliano wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Cletus Mnzava (katikati) wakijadiliana jambo na maofisa wengine wa mamlaka hiyo waliopo katika maonesho ya biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam
Mkemia Mwandamizi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Faustine Wanjala (kushoto)akiwa ameshika Muhogo na Karoti kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi waliofika kwenye banda lao lililopo maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...