Na Karama Kenyunko, globu ya jamii
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaamuru Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay na cha Kijitonyama kufika mahakamani hapo kesho kueleza  kwanini wamekaa na mshitakiwa kituo cha polisi badala ya kumpelekeka gerezani.

Oktoba 10, mwaka huu mahakama ilitoa amri kwa mshitakiwa ambaye ni msimamizi wa mirathi wa mke wa marehemu, Daudi Balali, Elizabeth Balali (54) kwenda gereza la Segerea kwa sababu anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ambayo haina dhamana.

Amri hiyo imetolewa leo Oktoba 24,2019 na Hakimu Mwandamizi Mfawidhi, Kevin Mhina baada ya wakuu hao kukaa na mshitakiwa huyo kituo cha polisi badala ya kumpeleka gerezani kama amri ilivyotolewa.

Kesi hiyo leo ilikuja mahakamani hapo lakini  haikuweza kusikilizwa kutokana na mkanganyiko uliokuwepo baada ya mshitakiwa huyo kubainika hakuwepo gereza la Segerea na kwamba alikuwa kituo cha polisi.

Mshitakiwa huyo aliletwa mahakamani akitokea Kituo cha Polisi Kijitonyama alikokuwa amekaa kwa siku saba na Kituo cha Oysterbay alikaa siku saba.

Katika kesi hiyo, Elizabeth ambaye ni Mkazi wa Boko Magengeni,  anakabiliwa na mashtaka ya kujipatia Sh milioni 25 kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha.

Awali wakili Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai  kati ya Oktoba 19 na Desemba 21, 2017 Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia kiasi cha Sh milioni 25 kutoka kwa Dk Roderick Kisenge kwa ulaghai.

Mshitakiwa anadaiwa  kujifanya anamuuzia eneo la mita za mraba 900 ambalo halijapimwa lililopo eneo la Boko Dovya Kinondoni wakati akijua eneo hilo si lake.

Wankyo alidai katika kipindi hicho  mshitakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Dk Kisenge kupitia akaunti yake iliyopo Katika Benki ya CRDB wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya kusomewa mashtaka, Elizabeth hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza makosa ya Uhujumu Uchumi na Hakimu Mhina alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa sababu mashitaka ya utakatishaji fedha hayana dhamana kisheria.

Hivyo alielekeza mshitakiwa huyo kurudishwa rumande katika gereza la segerea hadi leo kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...