Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi, Desemba 14,2020 inatarajia kutoa hukumu dhidi ya mfanyabiashara Ayubu Kiboko na mke wake Pilly Mohammed Kiboko wanaotuhumiwa kusafirisha gramu 251.25 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Uamuzi huo umetolewa leo Desemba 2, 2020 na Jaji Lilian Mashaka baada ya pande zote mbili, ule wa Jamuhuri na utetezi kumaliza kuwasilisha hoja za majumuisho, huku upande wa mashtaka ukidai wameweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa washtakiwa wametenda kosa na upande wa utetezi ukidai kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa washtakiwa wametenda kosa wanaokabiliwa nalo.
Katika kesi hiyo jumla ya mashahidi sita na vielelezo 16 vya upande wa mashtaka vilifikishwa mahakamani hapo kama sehemu ya ushahidi.
Mapema wakili wa upande wa utetezi, Majura Magafu akitoa hoja za majumuisho amedai kuwa,hakuna ushahidi hata chembe uliowasilishwa Mahakamani hapo, unaonyesha kuwa washtakiwa hao mtu na mkewe walikuwa na nia moja ya kutenda kosa.
Amedai katika kesi kama hiyo ili kuonekane kama washtakiwa walikuwa na nia moja ni lazima washtakiwa wangekula njama lakini hakuna shahidi aliyethibitisha kuwa washtakiwa walikula njama kwanza na wala hakuna aliyethibitisha kuwa walikuwa wakifahamu uwepo wa dawa za kulevya nyumbani kwao.
Aidha Magafu katika majumuisho yake pia amedai shahidi wa tatu katika kesi hiyo, Insp.Emmanuel Ambilikile aliieleza mahakama katika ushahidi wake kuwa walipewa taarifa ya kiitelejensia kuwa mshtakiwa Kiboko anahusika na biashara ya dawa za kulevya, ambapo taarifa hiyo inatakiwa iwe na vielelezo kama haina itabaki tu kuwa taarifa ya kusikia.
Pia, Magafu amedai kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha mtiririko wa kielelezo cha dawa za kulevya, kwani kielelezo kinapokamatwa ni lazima kuonekane mtiririko wa sehemu zote kilikopita na makabidhiano hadi pale kinapofikishwa mahakamani.
"Aliyekuwa mkamataji wa kesi hii walikabidhiana kienyeji, hapakuwepo na rekodi na kama walikuwa nayo kwa nini hawakuleta kitabu cha usajili mahakamani kama sehemu ya ushahidi. Amedai kutokuwepo kwa mtiririko kwa makabidhiano ya vielelezo kunaleta shaka kujua kama dawa zilizokamatwa ndio hayo ziliyotumika kwa ajili ya uchunguzi.
Kwa upande wake, wakili wa Serikali Salim Msemo akiwasilisha hoja za majumuisho amesema upande wa mashtaka wamethibitisha pasipo kuacha shaka kuwa washtakiwa wote wawili wametenda kosa hilo.
Ameeleza kiwa vielelezo vya dawa za kulevya vilipatikana nyumbani kwa washtakiwa na katika utetezi wao washtakiwa hao walithibitisha kuwa upekuzi ulifanyika nyumbani kwao walithibitisha kuwa nyumba yao ninalo eneo la ngazi la kuhifadhi viatu ambapo ndio dawa hizo zilipokamatwa.
Aidha ameeleza kuwa kuhusu kumkamatwa kwa dawa hizo, Msemo ameeleza kuwa wameweza kuthibitisha hilo kwa kuwa washtakiwa walisaini hati ya kumkamata mali na hivyo kwa kusaini hati hiyo wanakubaliana kuwa kulichosainiwa kip ndani ama kimechukuliwa.
Aidha, mtiririko wa kukabidhiana vielelezo haukukatika kwa namna yoyote ile kwani shahidi watatu na shahidi wa sita alieleza mlolongo mzimannamna makabidhiano ya vielelezo yalivyokuwa yakifanyika mpaka vilipofikishwa mahakamani.
Msemo amefafanua kuwa, mashahidi wote waliohusika katika mnyororo huo wa vielelezo walifika mbele ya mahakama na kutoa ushahidi wao.
"Mheshimiwa Jaji mashahidi wote waliotoa ushahidi wao tunaomba mahakama uwaone walikuwa ni wa kuaminika kwani mnyororo wa vielelezo unathibitishwa kwa nyaraka ama maneno. Kwa mazungunzo ama maandishi hivyo vyote vimefanyika, mazungumzo mashahidi wote sita walikuja hapa mbele yako na kutoa ushahidi wao na kielelezo pia tulileta na kilikuwa sahihi na tulifuata taratibu zote zinazoingatiwa", ameeleza Msemo.
Amesema washtakiwa katika utetezi wao walidai hakuna upekuzi uliofanyika kitu ambacho siyo cha kweli, upekuzi ulifanyika na shahidi wa sita alishuhudia upekuzi huo.
"Ni rai yetu kwa mahakama uwaone washtakiwa wana hatia katika makosa wanayoshtakiwa nayo". Amesema Msemo.
Mbali na wakili Msemo, mawakili wengine wa Serikali wanaoendesha kesi hiyo, Costantine Kakula na Candid Nasua.
Katika kesi ya uhujumu uchumi namba 29/2018, Kiboko na mkewe wanadaiwa, Mei 23, 2018 eneo la Tegeta Nyuki Masaiti wilaya ya Kinondoni, walisafirisha dawa za kuÄşevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 251.25.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...