Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MKURUGENZI wa Mashtaka Nchini (DPP), amemuondolea mashtaka ya utakatishaji fedha aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege.

Hatua hiyo imefikiwa leo Oktoba 22,2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi.

Mapema, wakili wa serikali Mwandamizi Ladslaus Komanya aliieleza mahakama kuwa, DPP amefanya mabadiliko madogo katika hati ya mashtaka kwa kumfutia mshtakiwa mashtaka ya utakatishaji fedha na kumsomea mashtaka mapya.

Pia ameieleza mahakama kuwa Mazungumzo kati ya DPP na mshtakiwa ya kukiri makosa yake bado yanaendelea.

"Mheshimiwa suala la makubaliano bado halijafikiwa muafala lakini kutokana na mazungumzo yanayoendelea, DPP ameridhia kufanya mabadiliko madogo katika hati ya mashitaka kwa kumfutia mashitaka ya utakatishaji fedha mshitakiwa," amedai Komanya

Katika hati mpya ya mashtaka, mshtakiwa Makandege anakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia hasara Serikali USD 980,000.

Katika shtaka la kwanza la kuongoza genge la uhalifu inadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18 mwaka 2011 hadi Machi 9, 2014 , ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mshtkiwa huyo ambaye si mtumishi wa umma akishirikiana na watumishi wa umma, waliweza kutekeleza njama za hila ili kujipatia fedha .

Inadaiwa, kati ya Januari 23 hadi Februari 10 mwaka 2014 katika benki ya Stanbic tawi la Kati, Wilaya ya Kinondoni na Benki ya UBL Ilala, Dar es Salaam, kwa nia ya udanganyifu, alijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), USD 380,000 na USD 600,000.

Katika shtaka la tatu inadaiwa, mshitakiwa huyo aliisababishia serikali hasara ya jumla ya USD 980,000.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Hakimu alimtaka mshtakiwa huyo kutojibu mashitaka kwakuwa mahakama hiyo haina Mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 4 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa ,mshitakiwa amepelekwa maabusu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...