Na Said Mwishehe,Michuzi TV

JUBILEE Group Tanzania imezindua rasmi ukuta uliojengwa kuzunguka Shule ya Msingi Madenge iliyopo Temeke, Dar es Salaam lengo likiwa kutatua ya usalama na changamoto ya usumbufu uliokuwa ukiababishwa na usumbufu wapita njia hali iliyokuwa ikiathiri mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.

Hivyo kujengwa kwa ukuta huo wanaamini utachangia kuimarisha mazingira salama na tulivu ya elimu, hivyo kuwapa walimu nafasi bora ya kufundisha na wanafunzi mazingira mazuri ya kujifunza na kufanya vizuri kitaaluma.

Uzinduzi huo uliozinduliwa leo Agosti 7,2026 katika shule hiyo umehudhuriwa na maofisa Watendaji Wakuu wa Jubilee Life Insurance na Jubilee Health Insurance, Bi. Helena Mzena na Dkt. Harold Adamson, pamoja na viongozi wa serikali za mitaa, uongozi wa shule na wafanyakazi wa Jubilee Group Tanzania.

Jubilee Group Tanzania itaendelea kutekeleza shughuli za uwajibikaji kwa jamii (CSR) kwa lengo la kuleta mchango chanya katika elimu, afya na ustawi wa jamii, kwa kuamini kwamba jamii yenye maendeleo ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.

Awali akisoma risala ya shule ya msingi Madenge wilayani Temeke Mwalimu Edith Mchome amesema wanashukuru kujengewa ukuta huo na hivyo kuondokana na changamoto mbalimbali ambazo wanafunzi na walimu walikuwa wakizipata kwa kutokuwa na uzio.

“Kwa niaba ya wanafunzi wote wa shule ya msingi Madenge, tunayofuraha kubwa kutoa shukrani zeiu za dhati kwa "jubilee Insurance Life kuiwezesha shule yetu kujengewa uzio upande mmoja korofi sana, ambape hapo awali hatukuweza kusoma kwa uskivu nautuivu.

“Jubilee Insurance Life imeturejeshea utulivu na usikivu katika mazingira yetu ya shule

kwa upande huo wenye uzio huu.Kabla ya ukuta huu ambao sasa tuko salama na hakuna tena vurugu za wapita njia wala wavuta bangi waliokuwa wanakuja hapa shuleni.

“Pia tunashukuru kwa kutupatia msitu ambao umetusaidia kutunza mazingira yetu ya shule ambayo yamekuwa kivutio kama mlivyoona, msitu huo umetusaidia sisi wanafunzi na

walimu wetu kujikinga dhidi ya upepo mkali na hivyo kuepusha athari zaidi za upepo mkali.

“Pamoja na hayo msitu umetusaidia kupata hewa safi ambayo tumekuwa tukiifurahia kila siku,”amesema Mchome na kuongeza pia wanawashukuru Jubilee Insurance Life kwa kutuwezesha kupata vifaa vya usafi kama vile reki, majembe na fyekeo. Vifaa hivyo vinaendelea kuwasaidia kutunza mazingira yao na kuyafanya kuwa safi kila siku kama mnavyoshuhudia.”




Benki ya Absa Tanzania imezindua rasmi Absa Lipa Sasa, huduma mpya ya malipo ya kidijitali inayotumia mfumo wa TanQR, ikiwa na lengo la kuwawezesha wafanyabiashara na watumiaji kufanya malipo kwa haraka, usalama na urahisi kupitia mfumo mmoja unaokubalika na benki mbalimbali pamoja na mitandao ya simu nchini.

Huduma hiyo imejengwa kwa kuzingatia kiwango cha kitaifa cha TanQR chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na inawawezesha wafanyabiashara kupokea malipo kutoka benki mbalimbali na mitandao ya simu kwa kutumia QR Code moja, hivyo kurahisisha miamala na kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Absa Tanzania, Victor Nchimbi, alisema huduma hiyo imeundwa kurahisisha malipo kwa wafanyabiashara na wateja wao.

“Kupitia Absa Lipa Sasa, mfanyabiashara anahitaji QR Code moja tu kupokea malipo kutoka kwa wateja wanaotumia benki tofauti au mitandao mbalimbali ya simu. Hii inaondoa ulazima wa kutumia vifaa au mifumo mingi ya malipo, hivyo kupunguza gharama za biashara, kuongeza kasi ya miamala, kuboresha utunzaji wa kumbukumbu na kuimarisha usalama wa malipo. Kwa wateja, huduma hii inaleta uzoefu rahisi, salama na unaotegemewa wa kufanya malipo ya kidijitali,” alisema Nchimbi.

Alieleza kuwa uzinduzi wa huduma hiyo unaunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania za kuongeza ujumuishaji wa huduma za kifedha na kuharakisha matumizi ya teknolojia katika shughuli za kiuchumi kupitia mifumo ya malipo ya kidijitali.

Kwa kutumia uwezo wa mfumo wa TanQR, Absa Lipa Sasa inawawezesha wafanyabiashara kupokea malipo yote kupitia mfumo mmoja bila kuwa na ulazima wa kutumia mifumo au vifaa tofauti vya malipo.

Akizungumza zaidi kuhusu faida za huduma hiyo Nchimbi alisema QR Code hiyo moja inakubali malipo kutoka benki mbalimbali na mitandao ya simu huku uthibitisho wa miamala ukipatikana papo hapo.

Aliongeza kuwa mfumo huo unapunguza utegemezi wa fedha taslimu, kuongeza uwazi katika miamala ya malipo na kupunguza gharama za kupokea malipo, hususan kwa biashara ndogo, za kati na za kati zinazokua (MSMEs).

"Huduma hiyo inalenga kuwahudumia wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa, pamoja na wafanyabiashara wa sekta isiyo rasmi wanaohitaji njia salama, rahisi na yenye ufanisi ya kupokea malipo", aliongeza.

Kwa upande wake, Meneja Masoko, Mawasiliano na Chapa wa Benki ya Absa Tanzania, Beda Biswalo, alisema uzinduzi wa Absa Lipa Sasa unaakisi dhamira ya benki hiyo ya kuwasaidia wateja kufikia malengo yao kupitia suluhisho bunifu za malipo.

“Katika Absa tunaamini kuwa ‘Stori Yako Ina Thamani’ kwa sababu kila mteja, mjasiriamali na biashara ina ndoto zinazostahili kuungwa mkono. Absa Lipa Sasa inaonesha dhamira yetu ya kuwasaidia wateja wetu kukua kupitia huduma rahisi, salama na zinazopatikana kirahisi ambazo zinakidhi mahitaji yao ya kila siku.


Hivi ndivyo tunavyotekeleza lengo letu la ‘Kuiwezesha Afrika ya Kesho, Pamoja… Hatua Moja Baada ya Nyingine,’ huku tukichochea ujumuishaji wa huduma za kifedha na mageuzi ya kidijitali nchini Tanzania,” alisema Biswalo.

Kupitia Absa Lipa Sasa, wafanyabiashara watapanua wigo wa wateja wao, kupunguza hatari zinazotokana na matumizi ya fedha taslimu, pamoja na kujenga historia ya miamala ya kidijitali ambayo inaweza kusaidia kupata huduma nyingine za kifedha siku zijazo.

Huduma hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Benki ya Absa Tanzania wa kuendeleza mageuzi ya kidijitali na kuimarisha nafasi yake kama mshirika wa kuaminika wa kifedha na taasisi inayochangia maendeleo chanya ya jamii.

Absa Lipa Sasa imeanza kupatikana kwa wafanyabiashara kote nchini, ambapo usajili unaweza kufanyika katika matawi yote ya Benki ya Absa Tanzania au kupitia wasimamizi wa mahusiano ya wateja wa benki hiyo.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Absa, Bw. Victor Nchimbi (katikati), Meneja Masoko, Mawasiliano na Chapa, Bw. Beda Biswalo ( kushoto ) na Meneja Bidhaa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Devroda Kagusa wakifanya malipo kwa simu kwa kutumia mfumo wa malipo wa Absa Lipa Sasa, wakati wa uzinduzi wa mfumo huo jijini Dar es Salaam leo. Kupitia Absa Lipa Sasa, wateja wanaweza kulipa kutoka benki au mtandao wowote kwa kutumia QR code au lipa namba hivyo kurahisisha malipo kwa kutumia njia za kidigitali.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Absa, Bw. Victor Nchimbi (wa tano kushoto), Meneja Masoko, Mawasiliano na Chapa, Bw. Beda Biswalo (wa nne kushoto ) na Meneja Bidhaa Kitengo cha Biashara, Bi. Devroda Kagusa (wa tatu kulia), pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo, wakizindua mfumo wa malipo wa Absa Lipa Sasa, wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Kupitia Absa Lipa Sasa, wateja wanaweza kulipa kutoka benki au mtandao wowote kwa kutumia QR code au lipa namba hivyo kurahisisha malipo kwa kutumia njia za kidigitali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ameipongeza kampuni ya Yas kwa ushiriki wake katika Maonesho ya Nanenane ya Mkoa wa Lindi, akisema mchango wa sekta binafsi unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya kilimo na mageuzi ya kidijitali nchini.

Mhe. Sangu aliyasema hayo alipotembelea Banda la Yas na kupokea maelezo kuhusu huduma za mawasiliano na kifedha kidijitali zinazotolewa na Yas na Mixx.

Kwa upande wake, Meneja wa Biashara na Masoko wa Yas - Kanda ya Pwani Kusini, Bw. George Msofe, alisema maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwafikia wakulima na wananchi kwa kuwaelimisha kuhusu suluhisho za kidijitali zinazorahisisha mawasiliano, malipo na ukuaji wa biashara.

"Yas itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha teknolojia na huduma za kidijitali zinawafikia Watanzania wengi zaidi, hususan wakulima, ili kuwawezesha kuongeza tija na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali," alisema Msofe.






Serikali imeutaka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuimarisha programu zinazowawezesha wananchi kujitegemea badala ya kujikita katika utoaji wa misaada ya kijamii.


Akizungumza leo Agosti 6, 2026 Jijini Dar es salaam, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Regina Qwaray, amesema Dira 2050 inalenga kuijenga Tanzania yenye uchumi shindani, jumuishi na unaoinua maisha ya kila mwananchi, hivyo TASAF inapaswa kuongeza mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi ya wananchi.

“TASAF iondokane na dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kwamba jukumu lake ni kutoa misaada ya kijamii pekee, na badala yake ijikite katika kuwawezesha wananchi kujenga uwezo wa kujitegemea kupitia shughuli zenye tija zinazoongeza kipato cha kaya”. amesema.

Aidha, amesema TASAF inasimamia rasilimali kubwa za umma zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi, hivyo ni muhimu kuendelea kuimarisha misingi ya utawala bora, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa fedha za umma ili kuzuia ubadhirifu, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa programu na kuhakikisha uwajibikaji katika ngazi zote.

Sambamba na hayo, ametoa wito kwa TASAF kuendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijiti inayowezesha ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu na matokeo yake kwa wakati halisi, hatua itakayorahisisha kufanya maamuzi kwa kuzingatia takwimu sahihi na kuongeza uwajibikaji.

Vilevile, amesema ni muhimu kuendelea kuimarisha usalama wa taarifa za walengwa kwa kuzingatia viwango vya usalama wa mifumo ya TEHAMA na ulinzi wa taarifa binafsi, hivyo kujenga imani ya wananchi, kulinda faragha zao na kuhakikisha mifumo ya TASAF inabaki kuwa salama, ya kuaminika na endelevu.


 



Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SHIRIKA la VI Agroforestry linatarajia kufanya kongamano kubwa la vijana kuhusu kilimo misitu litakalofanyika mkoani Mara mwezi Oktoba mwaka huu, likiwa na lengo la kuwakutanisha zaidi ya washiriki 8,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika kongamano la wadau wa kilimo lililofanyika kwenye Maonesho ya Nane Nane katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkazi wa VI Agroforestry, Martha Olotu, alisema kongamano hilo linalenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu fursa zilizopo katika kilimo misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Vijana, Joel Nanauka, ambaye atazungumza na vijana kuhusu nafasi yao katika sekta hiyo.

Olotu alisema VI Agroforestry imekuwa ikifanya kazi nchini kwa miaka 30, ikianzia mkoani Mara kabla ya kupanua shughuli zake katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Lindi, Mtwara na Kagera. Aliongeza kuwa hadi sasa washiriki zaidi ya 3,000 tayari wamejisajili, huku lengo likiwa kufikia washiriki 8,000, kutoka 6,000 walioshiriki mwaka jana.

Alisema shirika hilo pia linakusudia kuanzisha mtandao wa mashirika yanayojihusisha na kilimo misitu ili kuimarisha ushirikiano na kuendeleza sekta hiyo.

Kwa upande wake, Edna Paul kutoka Counsenult alisema kilimo misitu kina mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza rutuba ya udongo na kuimarisha usalama wa chakula, hivyo kusaidia kupunguza utapiamlo.

Naye Mkurugenzi wa Civil Social Protective Foundation, Nemesi Kiliya, alisema wadau wanatarajia kuzindua jukwaa la wadau wa kilimo misitu litakalounganisha taasisi mbalimbali kushirikiana katika kukuza sekta hiyo.



MENEJA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi Ilala Musibu Shabani amesema kuwa TRA imejidhatiti kuhakikisha biashara zinakua kwa kukusanya kodi bila kuziathiri ukuaji biashara hizo.

Shabani ameyasema hayo leo Julai 6 Agosti, 2026 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Mtaa wa Kitonga, Kata ya Msongola iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa biashara ndiyo chanzo kikuu cha kodi ambazo ndiyo mhimili wa maendeleo na kujitegemea kwa taifa hivyo ni jukumu la TRA kuzilinda biashara na kuhakikisha zinakua.

“Biashara na kodi ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu. Tunaendelea kuimarisha ukaribu kwa kusikiliza changamoto zenu na kuzitatua ili ulipaji na ukusanyaji wa kodi usiwe kizuizi kwa biashara kustawi,” amesema Shabani.

Aidha, amewasisitiza wafanyabiashara hao kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kikodi ikiwemo kujisajili na kupata TIN, kufanya makadirio na kulipa kodi stahiki kwa wakati.

Kwa upande wao, wafanyabiashara wameipongeza TRA kwa kutenga siku ya Alhamisi kwa viongozi kusikiliza changamoto za walipakodi moja kwa moja, huku wakisifu ukaribu uliopo sasa baina ya TRA na walipakodi.





Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB) Lwaga Mwambande akizungumza na Waandishi wa habari kwenye Banda la DIB katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nane Nane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Dkt.John Samwel Malecela Nzuguni Jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BODI ya Bima ya Amana (DIB) imesema inaendelea kuchukua hatua za kuziimarisha taasisi za fedha zinazokabiliwa na changamoto za kifedha ili zisifilisike, hatua inayolenga kulinda amana za wananchi na kuzuia Serikali kutumia fedha nyingi kulipa fidia endapo taasisi hizo zitafungwa.

Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, alisema moja ya majukumu ya bodi hiyo ni kusaidia taasisi za fedha zenye changamoto kwa kuzipa udhamini au mikopo maalumu ili ziweze kurejea katika hali ya kawaida ya uendeshaji.

Alisema hatua hiyo ni ya busara zaidi kuliko kusubiri taasisi hizo zifilisike na baadaye kutumia fedha nyingi kulipa fidia kwa waweka amana.

"DIB inalenga kuhakikisha taasisi za fedha zinaendelea kuwa imara huku haki za wananchi walioweka fedha zao zikiendelea kulindwa," alisema.

Mwambande aliwahakikishia wananchi kuwa fedha wanazoweka katika benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinalindwa kupitia mfumo wa Bima ya Amana.

Alifafanua kuwa mteja anapoanza kuweka fedha katika taasisi ya fedha yenye leseni ya BoT, amana yake huingia moja kwa moja katika mfumo wa kinga ya amana bila kulazimika kulipa gharama yoyote ya ziada.

Aidha, alisema kiwango cha juu cha fidia kinachotolewa kwa sasa ni Shilingi milioni 7.5 kwa kila mweka amana endapo benki itafungwa.

Alieleza kuwa mteja mwenye amana isiyozidi kiwango hicho hulipwa fedha zake zote, huku mwenye amana inayozidi kiwango hicho akilipwa kwanza kiwango kilichowekwa na kisha kuendelea kudai salio lililobaki kupitia mchakato wa ufilisi wa benki husika.

Mwambande alisema Mfuko wa Bima ya Amana unachangiwa na benki na taasisi zote za fedha zinazopokea amana kutoka kwa wananchi, ambapo kila taasisi huchangia asilimia 0.15 ya jumla ya amana zake kila mwaka.

Aliongeza kuwa fedha hizo huwekezwa katika dhamana za Serikali na maeneo mengine salama ya uwekezaji ili kuhakikisha mfuko unakuwa na uwezo wa kutosha kulipa fidia pale inapohitajika.

Pia alisema, pamoja na jukumu la kulipa fidia kwa waweka amana, DIB ina wajibu wa kusimamia ufilisi wa benki zinazofungwa. Kwa sasa bodi hiyo inaendelea kusimamia ufilisi wa benki tisa zilizofungwa katika nyakati tofauti, ikiwa na lengo la kukusanya mali za benki hizo na kuwalipa wadai, hususan wale wenye amana zinazozidi kiwango kinacholindwa na bima ya amana.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeongeza kasi ya utafiti wa kijiosayansi nchini kwa lengo la kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini, kuongeza ajira, mapato ya Serikali na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa GST, Mhandisi Ally Samaje, alisema taasisi hiyo ndiyo msingi wa mnyororo mzima wa sekta ya madini kwa kuwa hukusanya, kuchakata, kuhifadhi na kusambaza taarifa muhimu za kijiosayansi kwa wawekezaji na wadau mbalimbali.

Alisema GST imekamilisha utafiti wa jiolojia kwa asilimia 98 ya eneo lote la Tanzania, huku utafiti wa kijiofisikia wa kiwango cha kawaida ukifikia asilimia 100, hatua inayowapa wawekezaji taarifa za awali kuhusu maeneo yenye fursa za madini.

Kwa upande wa utafiti wa kijiofisikia wa kina (High Resolution Airborne Geophysical Survey), alisema taifa limefikia asilimia 16, huku maandalizi ya kuongeza kiwango hicho yakiendelea kupitia programu mpya za urushaji ndege katika maeneo yenye rasilimali nyingi za madini.

Mhandisi Samaje alifafanua kuwa awamu ya kwanza ya programu hiyo itahusisha utafiti katika eneo linalokadiriwa kuwa asilimia 18 ya ukubwa wa nchi, hatua itakayoongeza kiwango cha utafiti huo hadi asilimia 34 mara baada ya kukamilika. Aliongeza kuwa mkandarasi wa kazi hiyo tayari amepatikana.

Alisema awamu inayofuata itafanyika katika maeneo ya katikati ya Tanzania yenye ukubwa wa takribani asilimia 19 ya nchi, jambo litakalowezesha kufikia zaidi ya asilimia 50 ya utafiti wa kijiofisikia wa kina kabla ya mwaka 2030, kama ilivyoainishwa katika malengo ya Serikali.

Akizungumzia utafiti wa kijiokemia, alisema GST imefikia asilimia 24 ya eneo la nchi, huku ikipanga kufanya tafiti katika maeneo mapya 18 ndani ya mwaka huu wa fedha ili kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 30.

Alieleza kuwa maeneo mengi yatakayofanyiwa utafiti yamechaguliwa kutokana na uwepo wa wachimbaji wadogo, ambao watanufaika na taarifa za kisayansi zitakazowasaidia kufanya uchimbaji kwa uhakika badala ya kubahatisha, kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato chao.

Aidha, alisema taarifa hizo zitawawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo kutoka taasisi za fedha, huku GST ikiwa tayari kuthibitisha matokeo ya tafiti zake ili kuongeza imani ya wakopeshaji.

Mhandisi Samaje alibainisha kuwa utekelezaji wa programu hizo unawezeshwa na Mfuko wa Utafiti wa Madini unaotokana na fedha za retention zinazokusanywa kupitia sekta ya madini, ambazo zimeiwezesha GST kupanua shughuli zake za utafiti nchini.

Alisisitiza kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiosayansi utapunguza hatari kwa wawekezaji, kuongeza uwekezaji katika utafiti na uchimbaji wa madini, kuchochea uanzishaji wa migodi mipya, kuimarisha viwanda vinavyotumia madini kama malighafi na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.




Na Mwandishi Wetu, Dodoma
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kupitia kampuni ya ubunifu ya MaxwellTrack Technologies, kimebuni mfumo wa kidijitali unaolenga kusaidia kampuni za bima kufuatilia mienendo ya magari na kupata taarifa sahihi za mazingira ya ajali ili kurahisisha utoaji wa fidia.

Mfumo huo unafuatilia mwenendo wa gari kabla na wakati wa ajali, ikiwemo kasi ya gari, eneo lilipotokea tukio, muda wa ajali pamoja na taarifa nyingine muhimu zinazoweza kusaidia kubaini chanzo na mazingira ya ajali.

Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Mhadhiri Msaidizi wa UDOM na Mwanzilishi wa MaxwellTrack Technologies, Jospeter Kaizilege, amesema ubunifu huo umejikita katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa taarifa sahihi wakati wa kushughulikia madai ya fidia.

Amesema mara nyingi kampuni za bima hukumbana na changamoto ya kupata ushahidi wa kutosha kuhusu mazingira yaliyosababisha ajali, hali inayoweza kuchelewesha mchakato wa kufanya maamuzi kuhusu madai ya wateja.

“Changamoto kubwa imekuwa pale mteja anapopata ajali na kampuni ya bima kuhitaji uthibitisho wa mazingira yaliyosababisha ajali. Mfumo wetu unarekodi taarifa zote muhimu, hivyo unarahisisha kampuni ya bima kufanya maamuzi kwa kutumia ushahidi uliopo kwenye mfumo,” amesema Kaizilege.

Ameeleza kuwa mfumo huo umeundwa kwa kuzingatia mazingira ya Afrika, tofauti na baadhi ya vifaa vya GPS vinavyoagizwa kutoka nje ambavyo vinaweza kukumbana na changamoto za utendaji katika maeneo yenye mawasiliano hafifu.

Kwa mujibu wa Kaizilege, teknolojia hiyo inaweza kufanya kazi katika maeneo yenye changamoto za mawasiliano, hatua inayolenga kuhakikisha taarifa muhimu za gari na ajali zinapatikana kwa wakati unaohitajika.

Amesema matumizi ya mfumo huo yanaweza kusaidia kampuni za bima kupunguza migogoro inayohusiana na madai ya fidia, huku wateja wakinufaika na uwazi zaidi kutokana na kuwepo kwa taarifa za ajali zinazoweza kufikiwa kwa urahisi.

Kaizilege amesema wazo la ubunifu huo lilianza mwaka 2022 akiwa mwanafunzi wa UDOM, kama mradi wa mwisho wa masomo, kabla ya kuendelezwa kupitia programu za ubunifu za chuo hicho na hatimaye kuanzishwa rasmi kwa MaxwellTrack Technologies.

“Tumeanza rasmi kutoa huduma nchini Tanzania kwa takribani mwezi mmoja sasa na lengo letu ni kupanua huduma kwenda Kenya na Rwanda. Pia tunaendelea kushirikiana na mamlaka husika pamoja na kampuni mbalimbali za bima ili kuunganisha mfumo wetu na mifumo yao na kuhakikisha teknolojia hii inanufaisha sekta ya bima na usafirishaji kwa ujumla,” amesema Kaizilege.

* Kiongozi wa dini mwenye umri wa miaka 95 azuiliwa kwa mashtaka yanayohusiana na sheria za vyama vya siasa, bila kuhusisha tuhuma za vurugu.

* Waziri wa Sheria wa Korea Kusini ananukuu Biblia hadharani huku akitoa maoni kuhusu kundi la dini la wachache.

* Wataalamu wa haki za binadamu wanadai kuzuiliwa huko kunakiuka viwango vya kimataifa, ikiwemo Kanuni za Mandela za Umoja wa Mataifa na misingi ya Kikundi Kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu Kuzuiliwa Kiholela.

SEOUL, Korea Kusini – 6 Julai 2026 – Wasiwasi wa kimataifa unaendelea kuongezeka kufuatia kuzuiliwa na kushtakiwa kwa Mwenyekiti Lee Man-hee, mwenye umri wa miaka 95, kiongozi wa Kanisa la Shincheonji la Yesu, pamoja na matamshi ya hivi karibuni yaliyotolewa na Waziri wa Sheria wa Korea Kusini, Jeong Seong-ho.

Mnamo tarehe 30 Juni 2026, Waziri Jeong alitangaza kupitia akaunti yake ya mitandao ya kijamii kuwa Mwenyekiti Lee amefunguliwa mashtaka akiwa rumande, akisema kwamba “adhabu kali ya jinai inayolingana na wajibu wake haiwezi kuepukika." Alimalizia ujumbe wake kwa kunukuu Mathayo 7:15: “Jihadharini na manabii wa uongo."Kanisa la Shincheonji la Yesu ni dhehebu la Kikristo lililoanzishwa nchini Korea Kusini mwaka 1984.

Dk. Massimo Introvigne, mwanasosholojia wa dini kutoka Italia, amechapisha makala mbili katika jarida la Bitter Winter, linalojihusisha na masuala ya uhuru wa dini na haki za binadamu. Makala ya kwanza, iliyochapishwa tarehe 24 Juni 2026, ilikosoa hatua ya kumweka rumande Mwenyekiti Lee, huku ya pili, iliyochapishwa tarehe 2 Julai 2026, ikitoa uchambuzi wa kina kuhusu kauli za Waziri Jeong.

Kuzuiliwa kwa Kiongozi wa Dini Mwenye Miaka 95: "Hatua Inayokiuka Viwango vya Kimataifa"

Mwenyekiti Lee alizuiliwa tarehe 24 Juni 2026 kwa tuhuma zinazojumuisha ukiukaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, na akafunguliwa rasmi mashtaka akiwa bado rumande tarehe 30 Juni.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, kati ya Julai 2021 na Januari 2024, Lee alidaiwa kuratibu usajili wa takribani wanachama 50,000 wa Kanisa la Shincheonji katika Chama cha People Power Party (PPP), kwa lengo la kushawishi uchaguzi wa ndani wa chama hicho wa urais na ubunge.

Dk. Introvigne amesema kuwa kumweka rumande kiongozi wa dini mwenye umri wa miaka 95 katika kesi isiyohusisha vurugu wala uhalifu mkubwa hakuzingatii kanuni ya uwiano inayotakiwa chini ya Kanuni za Kiwango cha Chini za Umoja wa Mataifa kwa Matibabu ya Wafungwa (Kanuni za Mandela), pamoja na misingi ya Kikundi Kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu Kuzuiliwa Kiholela.

Aidha, alilinganisha tukio hilo na kesi ya Han Hak-ja, mwenye umri wa miaka 83, kiongozi wa Family Federation for World Peace and Unification (Kanisa la Unification), ambaye pia anakabiliwa na kesi tofauti. Kwa mujibu wake:

 "Hili si suala linalohusu kundi moja la dini pekee; linaashiria mwenendo unaojitokeza ambapo kuzuiliwa kimwili kunatumika mara kwa mara dhidi ya viongozi wa dini wenye umri mkubwa."

Baada ya kukamatwa kwake, Kanisa la Shincheonji la Yesu lilisema kuwa Mwenyekiti Lee na kanisa zima walishirikiana kikamilifu katika hatua zote za uchunguzi, ikiwemo upekuzi na ukusanyaji wa ushahidi. Kanisa hilo lilieleza kuwa kuzuiliwa kwake ni “adhabu ya kimwili inayotolewa kwa mtuhumiwa mwenye umri wa miaka 95."

Kauli za Waziri wa Sheria na Hoja ya Kutokuwa na Upendeleo wa Serikali

Kwa mujibu wa Dk. Introvigne, jambo linalozua wasiwasi mkubwa zaidi ni muda ambao Waziri Jeong alitoa kauli zake. Waziri huyo alitoa wito wa hadharani wa kutolewa kwa “adhabu kali ya jinai" siku hiyo hiyo ambayo Mwenyekiti Lee alifunguliwa rasmi mashtaka akiwa rumande.

Dk. Introvigne alieleza kuwa pale afisa anayesimamia mfumo wa sheria na mashtaka anapotangaza hadharani hitaji la adhabu wakati kesi inaanza kusikilizwa, hatua hiyo inaweza kutafsiriwa kuwa ni kutoa hukumu kabla ya mahakama kuamua.

Vilevile, alibainisha kuwa afisa wa umma kutumia mstari wa Biblia ambao unaweza kumweka mshtakiwa katika taswira hasi kunaweza kuibua maswali kuhusu wajibu wa serikali wa kutokuwa na upendeleo wa kidini. Kwa kuwa matamshi ya Waziri wa Sheria yanaweza kutafsiriwa kama msimamo rasmi wa serikali, alisema tahadhari kubwa inapaswa kuzingatiwa.

Hoja Kuu ya Kisheria: Je, Kulikuwa na Kulazimishwa?
Hoja kuu katika kesi hii si iwapo wanachama walijiunga na chama cha siasa, bali ni iwapo walifanya hivyo kwa hiari au walilazimishwa.

Waendesha mashtaka wanadai kuwa ushahidi unaonyesha kuwepo kwa kampeni iliyopangwa ya kuwalazimisha wanachama kujiandikisha, huku Kanisa la Shincheonji la Yesu likisisitiza kuwa hakuna mwanachama aliyelazimishwa kwa nguvu wala kwa amri yoyote kujiunga na chama hicho.

Kwa mujibu wa Dk. Introvigne, uamuzi wa kesi hiyo utategemea ushahidi na hoja za kisheria zitakazowasilishwa kuhusu madai ya kulazimishwa.

Aliongeza kuwa: "Mashtaka haya yanaweza kuhalalisha kuadhibiwa kwa ushiriki wa kawaida wa kiraia kwa sababu tu wahusika ni wanachama wa kundi la dini la wachache."

Aidha alisema:
"Wanachama wa Shincheonji, kama raia wengine wote wa Korea Kusini, wana haki ya kujiunga na chama cha siasa na kumuunga mkono mgombea wanayemchagua."

“Doa katika Sifa za Kidemokrasia za Korea Kusini"

Kwa mujibu wa Dk. Introvigne, suala hili linafuatiliwa kwa karibu na jumuiya za kimataifa zinazojihusisha na uhuru wa dini, si kama swali la hatia au kutokuwa na hatia kwa kundi moja la dini pekee, bali kama kipimo cha namna taifa la kidemokrasia linavyotekeleza kwa usawa utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu kwa makundi ya dini ya wachache au yenye mitazamo inayozua mijadala.

Alionya kuwa iwapo matamshi ya viongozi waandamizi wa serikali yataonekana kuathiri uhuru wa mahakama, haki ya mshtakiwa kupata usikilizwaji wa haki au uhuru wa kisiasa wa waumini, athari zake zinaweza kuvuka mipaka ya kesi moja na kudhoofisha imani ya umma katika utawala wa sheria na ulinzi wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wake, demokrasia ya kweli lazima ihakikishe kuwa makundi ya wachache yanapata taratibu na ulinzi wa haki sawa na unaotolewa kwa wananchi wengine wote.

Dk. Introvigne ameielezea hali hiyo kuwa “doa katika sifa za kidemokrasia za Korea Kusini,"akisisitiza kuwa ni suala linalostahili kupewa uangalizi wa kimataifa.

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Bia leo, Serengeti Breweries Limited (SBL) inaungana na maadhimisho hayo kwa namna ya kipekee baada ya bidhaa zake kuthibitika kuwa na viwango vya kimataifa. Mafanikio hayo yamekuja kufuatia Serengeti Lite, Serengeti Lager na Serengeti Lemon kutunukiwa Tuzo za Gold Quality Awards 2026 kutoka taasisi maarufu duniani ya Monde Selection.

Tuzo za Gold Quality Awards zinazotolewa na Monde Selection hutolewa kwa bidhaa zinazokidhi viwango vya juu vya ubora vinavyotambulika kimataifa baada ya kupitia mchakato makini wa tathmini unaofanywa na jopo huru la wataalamu wa kimataifa. Bidhaa hupimwa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo ubora wa jumla, ladha, mwonekano, ubunifu, taarifa kwa watumiaji pamoja na uzoefu wa mtumiaji, ili kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyotambulika duniani.

Monde Selection ilianzishwa mwaka 1961 mjini Brussels, Ubeligiji, ikiwa ni taasisi huru ya kimataifa inayojihusisha na tathmini ya ubora wa bidhaa za walaji. Kwa zaidi ya miaka 65, taasisi hiyo imekuwa ikitathmini maelfu ya bidhaa katika makundi mbalimbali, ikiwemo vyakula, bia, vinywaji vikali, bidhaa za afya na lishe pamoja na vipodozi. Kila mwaka, tathmini hizo hufanywa na wataalamu zaidi ya 80 kutoka mataifa mbalimbali, huku bidhaa kutoka takribani nchi 150 zikiwa zimewasilishwa kwa ajili ya kufanyiwa tathmini kwa kipindi chote.

Mafanikio haya yanaakisi dhamira endelevu ya Kampuni ya Serengeti ya kuzalisha vinywaji vya ubora wa kiwango cha kimataifa kupitia uwekezaji unaoendelea katika teknolojia za kisasa za uzalishaji, mifumo madhubuti ya uhakiki wa ubora, pamoja na ubunifu unaomweka mlaji katika kitovu cha kila hatua ya shughuli zake.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Ugavi wa SBL Joseph Cheloti, alisema tuzo hizo ni uthibitisho wa dhamira kuu ya kampuni katika kuhakikisha bidhaa zake zinadumisha viwango vya juu vya ubora.

"Kupokea Tuzo za Gold Quality Awards kutoka Monde Selection ni heshima kubwa na uthibitisho kuwa bidhaa zetu zinakidhi viwango vya ubora vinavyotambulika kimataifa. Tunajivunia mafanikio haya ambayo yanadhihirisha kujitolea kwa wafanyakazi wetu, ubora wa malighafi tunazotumia pamoja na uimara wa mifumo yetu ya uzalishaji. Zaidi ya yote, tunawashukuru wateja wetu kwa kuendelea kutuamini na kutuunga mkono."

Aliongeza kuwa kampuni itaendelea kuwekeza katika ubora, ubunifu na maendeleo ya bidhaa ili kuhakikisha watumiaji nchini Tanzania na katika masoko mengine wanaendelea kupata vinywaji vinavyokidhi viwango vya juu vya ubora duniani.

Mbali na bidhaa hizo tatu za bia, chapa ya vinywaji vikali ya kampuni hiyo, TZEE, pia ilitunukiwa Tuzo ya Gold Quality Award 2026. Kupokea Tuzo nne za Gold Quality Awards kwa wakati mmoja kunazidi kuimarisha nafasi ya Kampuni hiyo, kama miongoni mwa wazalishaji wa vinywaji wanaozingatia ubora unaotambulika kimataifa, huku ikiendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania na kuonesha ubora wa bidhaa zake katika jukwaa la dunia.



Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM, Idara ya Organizesheni, Paul Chacha amesema uongozi wake utasimamia uchaguzi wa haki na usawa ndani ya chama, akisisitiza kuwa hakuna mwanachama atakayepokonywa haki yake kutokana na ushawishi wa fedha au mamlaka ya watu binafsi.

Akizungumza katika makao makuu ya CCM jijini Dodoma wakati wa mapokezi ya viongozi wapya walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama, Chacha amesema CCM ndiyo chama kilichojipanga zaidi nchini na kinaendelea kuwahakikishia Watanzania amani, maendeleo na matumaini ya maisha bora.

Amesema uchaguzi ndani ya chama unapaswa kuwa wa haki na uwazi ili kumpata kiongozi anayestahili kwa ridhaa ya wanachama, huku akiahidi kusimama imara kulinda misingi ya demokrasia bila kuyumbishwa na shinikizo lolote.

Chacha ametoa onyo kwa watu wanaokusudia kutumia fedha kujinufaisha kisiasa, akisema ni heri fedha hizo zikaelekezwa kwenye uwekezaji au biashara kuliko kutumika kuwarubuni wapiga kura.

Aidha, amesisitiza kuwa CCM haitamvumilia mtu yeyote atakayejaribu kununua kura au kushawishi wanachama kwa fedha ili kupata nafasi za uongozi, akibainisha kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaokiuka maadili ya chama.

Vilevile, amesema chama hakitasita kuwachukulia hatua watu wanaotumia nafasi au mamlaka ya ndugu zao kuingilia mchakato wa uchaguzi na kutoa maelekezo yanayokandamiza haki za wanachama.

Kwa mujibu wa Chacha, uchaguzi wa haki ndio msingi wa kupata viongozi wenye uwezo wa kukijenga chama na kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu na uwajibikaji.






Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, ameipongeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kwa mchango wake katika kuwawezesha wakulima kupata masoko yenye ushindani kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Mhe. Chande ameyasema hayo leo Agosti 6, 2026, baada ya kutembelea banda la WRRB katika Maonesho ya 88 yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, jijini Dodoma.

Amesema WRRB imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha biashara ya mazao kwa kuwawezesha wakulima kupata masoko yenye ushindani, kuongeza thamani ya mazao yao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Aidha, ameipongeza WRRB kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na kutoa wito kwa wadau wa sekta ya kilimo kuendelea kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Maonesho ya Nane Nane ya mwaka 2026 isemayo, "Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," kwa kuimarisha mifumo ya masoko, kuongeza tija katika uzalishaji na kuhakikisha wakulima wananufaika na fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa mazao.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uratibu Huduma ,Bw. Mwita Thomas ameeleza kuwa WRRB itaendelea kuboresha huduma zake, kuimarisha usimamizi wa mfumo huo kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa chachu ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi.

DODOMA

Mfumo wa kuagiza mafuta kwa ajili ya matumizi ya miezi miwili inayofuata umeiwezesha Tanzania kuendelea kuwa na bidhaa za mafuta za kutosha, licha ya vita na changamoto nyingine zinazoathiri soko la dunia.

Hayo yameelezwa na Mhandisi Rehema Mahundi katika siku ya sita ya Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

Mhandisi Mahundi alisema moja ya maswali yanayoulizwa zaidi na wananchi ni namna Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja unavyoiwezesha nchi kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta, hasa wakati wa migogoro na vita katika maeneo mbalimbali duniani.

Akijibu swali hilo, alieleza kuwa PBPA hutangaza zabuni kila mwezi kwa ajili ya kuagiza mafuta yatakayotumika nchini katika miezi miwili inayofuata. Utaratibu huo unajulikana kama M+2.

“PBPA huingia mikataba na wazabuni walioshinda zabuni hizo ili kuhakikisha bidhaa za mafuta zinafika nchini kwa wakati, hata changamoto zinapojitokeza katika soko la dunia,” alisema Mhandisi Mahundi.

Alisema kupitia mfumo huo, Tanzania imeendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta wakati wote na kwa gharama zinazoakisi hali halisi ya soko la dunia.

Katika Maonesho ya Nanenane, PBPA imeendelea kutoa elimu kuhusu Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja kwa watu kutoka makundi mbalimbali, wakiwamo wanafunzi, wakulima, wajasiriamali, wafanyabiashara pamoja na wawakilishi kutoka taasisi za elimu na sekta binafsi.

Mhandisi Mahundi amewakaribisha wananchi kutembelea Banda la PBPA katika Viwanja vya Nanenane jijini Dodoma ili kupata elimu zaidi kuhusu namna mfumo huo unavyosimamia mnyororo wa uagizaji, usimamizi na upokeaji wa bidhaa za mafuta nchini.