WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekemea vikali vitendo vya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuvielekeza vyombo vya dola kuchukua hatua stahiki na kali kwa wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi katika ngazi za vijiji na kata kuhakikisha kuwa uuzaji na ugawaji wa maeneo unazingatia miongozo ya matumizi bora ya ardhi ili kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza, ikiwemo migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Dkt. Mwigulu ametoa maagizo hayo leo, Oktoba 26, 2026, wakati akizungumza na wabunge wa Mkoa wa Ruvuma, jijini Dodoma kufuatia vurugu zilizotokea hivi karibuni baina ya wakulima na wafugaji, ambazo zimesababisha madhara mbalimbali vikiwemo vifo.

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Serikali haivumilii vitendo vya uvunjifu wa sheria na amewataka wananchi kuheshimiana, kuvumiliana na kuzingatia sheria katika kutekeleza shughuli zao za kiuchumi.

Amesema Serikali haiungi mkono uchukuaji wa sheria mkononi, utaratibu huo ni kinyume cha Katiba na sheria za nchi, hivyo kila mwananchi anapaswa kufuata taratibu zilizowekwa na kuviachia vyombo vya dola kutekeleza wajibu wake.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa pole kwa wananchi wa Wilaya ya Tunduru na Watanzania wote walioathiriwa na matukio hayo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na makosa hayo.

Kuhusu matumizi ya ardhi, Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha ardhi inatumika kwa kuzingatia mipango na miongozo iliyowekwa kwa lengo la kuimarisha amani, kuzuia migogoro na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kwa usalama.

Pia, Waziri Mkuu ametoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda tunu za Taifa, hususan amani na mshikamano, akisisitiza kuwa tofauti za kiuchumi na matumizi ya ardhi zinapaswa kutatuliwa kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.

Kwa upande wao, wabunge wa Mkoa wa Ruvuma wameishukuru Serikali kwa hatua inazoendelea kuchukua kukabiliana na migogoro hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa matumizi ya ardhi pamoja na kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao.




Na Victor Masangu,Kibaha

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Nicas Mawazo amewahakikishia wawekezaji ambao ni wazawa kuwapatia maeneo kwa ajili ya uwekezaji mbali mbali kwa lengo la kuweza kutoa fursa za ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa halfa ya uzinduzi rasmi wa sehemu maalumu iliyojengwa kwa ajili ya michezo mbali mbali ya kubahatisha iliyopo karibu na stendi ya zamani kata ya maili moja katika jengo la kontena bar Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Sehemu hiyo ambayo ni mradi mkubwa wa Casino ya Kisasa ambayo inamilikiwa na kampuni inayotambulika kwa jina la Cleopatra Tanzania yenye lengo la kuwapa fursa watu wa aina mbali mbali kucheza michezo ya kubahatisha.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mstahiki Meya Dkt. Mawazo amempongeza mkurugenzi mkuu wa CLEOPATRA Juma Mlali kwa kuweza kuwekeza katika mradi huo ambao utasaidia katika upatikanaji wa fursa za ajira kwa vijana na watu wengine.

Aidha amebainisha kwamba uwekezaji huo ni mkubwa na ni moja ya hatua za kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kukuza uchumi kupitia uwekezaji ambao wameufanya.

Kadhalika Mstahiki Meya amesema kuwa akiwa meza kuu Mkurugenzi Mtendaji wa CLEOPATRA CASINO Juma Mlali amemweleza kuwa anatamani wapate eneo ili waweze kuwekeza kwa kujenga Kiwanda .

"Mimi nashukuru nimeshiriki katika halfa ya uzinduzi huu na kiukweli nimefurahishwa na juhudi zilizofanywa katika uwekezaji huu pia nawakaribisha sana ofisini ili tuweze kuwakopesha na kuwapa eneo la uwekezaji,"amebainisha Mstahiki Meya

Naye mkurugenzi mkuu wa CLEOPATRA amebainisha kwamba wanajivunia kwa kutoa ajira kwa vijana wengi katika mikoa yote nchini ."Tuna matawi nchi nzima na tumetoa ajira 400 na kwa upande wa uwekezaji tutaanza kujenga Kiwanda kwa ajili ya kutengeneza vinywaji mbalimbali" amebainisha Mkurugenzi Mlali.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa CLEOPATRA Asha Simba amesema kwa sasa wana maduka yapatayo zaidi ya 53 ambayo yapo katika mikoa mbali mbali ya Tanzania.

Nao baadhi ya vijana ambao walishiriki katiks uzunduzi huo wamepongeza juhudi za uwekezaji huo wa kuwepo na sehemu ya kisasa ambayo imetengwa kwa ajili ya michezo ya kubahatisha ambapo wameweza kupata fursa za ajira.









Na. Benny Mwaipaja, Mangapwani, ZANZIBAR.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Shirika la Bandari Zanzibar, kuanza mapema maandalizi ya vifaa, mifumo na watumishi watakaohitajika kutoa huduma katika Bandari Jumuishi ya Mangapwani ili kuhakikisha inaanza kufanya kazi kwa ufanisi mara tu ujenzi wake utakapokamilika.

Mhe. Balozi Omar ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake katika Mradi wa Ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Zanzibar, kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati na kujionea hatua zilizofikiwa, pamoja na kutathmini maandalizi ya taasisi zitakazohusika katika utoaji wa huduma bandarini hapo.ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Amesema Bandari ya Mangapwani ni miundombinu muhimu ya kimkakati kutokana na uwezo wake wa kuhudumia meli kubwa ujenzi wake utakapo kamilika mwaka 2028, hivyo inatarajiwa kuwa kituo muhimu cha shughuli za forodha na chanzo cha mapato ya Serikali kupitia ushuru wa forodha.

“Pamoja na ujenzi wa miundombinu ya bandari, ni muhimu taasisi zote zinazohusika na utoaji wa huduma kuhakikisha zinapanga kwa pamoja mahitaji yao ili kuepusha bandari kukamilika huku vifaa na mifumo muhimu ya uendeshaji ikiwa haijakamilika” alisema Mhe. Balozi Omar

Aidha, amesisitiza umuhimu wa Shirika la Bandari Zanzibar na TRA kuoanisha ratiba zao za utekelezaji ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati na shughuli za bandari zinafanyika kwa ufanisi.

Mhe. Balozi Omar alieleza kuridhishwa na taarifa ya maendeleo ya mradi iliyobainisha kuwa ujenzi umefikia takribani asilimia 20, hatua inayolingana na matarajio ya utekelezaji kwa kipindi husika, huku mkandarasi akiendelea na kazi katika eneo la mradi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar, Bw. Akif Ali Khamis, amesema Bandari Jumuishi ya Mangapwani ni miongoni mwa miradi muhimu inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwa kuimarisha shughuli za biashara na usafirishaji wa shehena ya mizigo.

Alisema ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni muhimu katika kuhakikisha bandari hiyo inakuwa kitovu cha biashara na inatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi.

Bw. Khamis alieleza kuwa ziara ya Waziri wa Fedha imekuwa fursa ya taasisi husika kujadili maendeleo ya ujenzi, kutambua changamoto zinazoweza kujitokeza na kuweka mikakati ya mapema ya kukamilisha maandalizi ya miundombinu na huduma zitakazohitajika bandarini hapo.

Alitaja baadhi ya mahitaji muhimu kuwa ni miundombinu ya kuhifadhi mizigo, vifaa vya ukaguzi wa mizigo ikiwemo midaki (scanners), pamoja na mifumo na vifaa vya TRA, vitakavyowezesha shughuli za forodha na usafirishaji wa mizigo ya transshipment kufanyika kwa ufanisi na bila usumbufu usio wa lazima.

“Bandari hii ya Mangapwani inatarajiwa kukamilika Septemba 2028 na kukabidhiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na awamu ya kwanza itakuwa na uwezo wa kuhudumia takribani makontena 250,000 hadi 300,000 kwa mwaka, pamoja na tani 500,000 hadi milioni moja za mizigo ya kawaida isiyohifadhiwa kwenye makontena” alisema Bw. Khamis.

Aliongeza kuwa bandari hiyo ina uwezo wa kupanuliwa katika awamu zijazo kupitia upanuzi wa maeneo ya kuhifadhi mizigo na miundombinu mingine, hatua itakayoongeza uwezo wake wa kuhudumia biashara na mizigo kwa kadiri mahitaji yatakavyoongezeka.

Bw. Khamis alisema ujenzi wa bandari hiyo unatarajiwa kuimarisha uwezo wa Zanzibar katika kuhudumia biashara ya kimataifa, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kufungua fursa mpya za uwekezaji, na Kukamilika kwa mradi huo, sambamba na maandalizi ya mapema ya taasisi zinazohusika, kunatarajiwa kuweka mazingira bora ya uendeshaji wa bandari na kuongeza mchango wake katika mapato na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kushoto), akisikiliza maelezo  kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar, Bw. Akif Ali Khamis (kulia), wakati alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Zanzibar, kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati na kujionea hatua zilizofikiwa, pamoja na kutathmini maandalizi ya taasisi zitakazohusika katika utoaji wa huduma bandarini hapo ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kushoto), akizungumza jambo wakati alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Zanzibar, kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati na kujionea hatua zilizofikiwa, pamoja na kutathmini maandalizi ya taasisi zitakazohusika katika utoaji wa huduma bandarini hapo. Wa pili kushoto ni Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Bw. Mcha Hassan Mcha, na Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar, Bw. Akif Ali Khamis (kulia).

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Zanzibar)







📌 Ni kiwanda cha vinywaji baridi cha Simba beverages Limited kilichopo Kibaha mkoa wa Pwani;

📌 Asifu uwekezaji mkubwa bilioni 28 wa kiwanda hicho sambamba na asilimia 90 ya ajira za wazawa;

📌 Serikali yasisitiza uzalishaji wa bidhaa bora na salama, matumizi ya malighafi za ndani, uhamishaji wa teknolojia na uongezaji wa ajira kwa Watanzania.



KIBAHA, PWANI

Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), ameipongeza kampuni ya Simba Beverages Limited kwa uwekezaji wa takribani Shilingi bilioni 28 katika sekta ya viwanda nchini, akieleza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uchumi kupitia uzalishaji wa bidhaa nchini, kuongeza ajira na kupanua wigo wa mapato ya Serikali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho kilichopo katika eneo la viwanda la Zegereni, Kibaha, mkoani Pwani, Waziri Kapinga amesema,Serikali inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ya kufungua viwanda vipya nchini na kuvutia uwekezaji wa viwanda vipya ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.

Amesema sekta ya vinywaji baridi ni miongoni mwa sekta muhimu katika kukuza uchumi wa viwanda kutokana na mchango wake katika uzalishaji, ajira na uwekezaji, pamoja na kuunganisha shughuli nyingine za kiuchumi zikiwemo kilimo, usindikaji na usambazaji wa bidhaa. Amesisitiza kuwa maendeleo ya sekta hiyo yanapaswa kwenda sambamba na matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini ili kuongeza thamani ya rasilimali za ndani na kunufaisha wazalishaji wa Kitanzania.

Waziri Kapinga ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, huku akiwataka wawekezaji kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinazingatia sheria, kanuni na viwango vya ubora na usalama. Amesisitiza pia umuhimu wa kulinda wafanyakazi na kuboresha mazingira ya kazi ili kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Fadhili Nkurlu, amesema idadi ya viwanda katika Mkoa wa Pwani imeongezeka kutoka viwanda 387 katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi kufikia viwanda 768 kufikia Septemba 2026. Alieleza kuwa viwanda hivyo vinajumuisha viwanda vikubwa 33, vya kati 33, vidogo 248 na vidogo zaidi 454.

Ameongeza kuwa viwanda vikubwa na vya kati 38 vilikuwa katika hatua za ujenzi ila sasa vimekamilika, vikiwemo viwanda vikubwa 27 na vya kati 11, huku viwanda vingine 99 vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi na maandalizi. Aidha, alisema viwanda 35 vilivyopo katika maeneo ya uwekezaji mkoani humo vimechangia kuzalisha ajira za moja kwa moja 2,357 na ajira nyingine zisizo rasmi 6,062 zinazotokana na shughuli za kiuchumi zinazohusiana na viwanda hivyo.

Mhe. Nkurlu amesema Mkoa wa Pwani unaendelea kuweka kipaumbele katika kuvutia uwekezaji wa viwanda vipya, kuongeza ajira kwa vijana, kuhamasisha matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini na kusimamia ubora na usalama wa bidhaa zinazozalishwa. Ameeleza kuwa uwekezaji wa Simba Beverages Limited ni sehemu ya juhudi za kujenga uchumi imara na wenye ushindani kupitia sekta ya viwanda.

Kwa upande wake, Afisa mkuu wa fedha Surya Murthy, Afisa Mkuu wa Fedha (CFO) wa Simba Beverages Limited, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na viongozi wa Mkoa wa Pwani na Wilaya ya Kibaha kwa ushirikiano wao katika kuwezesha uwekezaji huo. Ameeleza kuwa uzinduzi wa kiwanda hicho ni hatua muhimu katika kuendeleza shughuli za uzalishaji nchini, kuongeza thamani ya bidhaa na kuimarisha minyororo ya ugavi, huku kampuni ikiendelea kutekeleza dhamira yake kupitia kaulimbiu ya “Imezaliwa Tanzania, Inatumikia Afrika.”

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa katika hafla hiyo, Simba Beverages Limited imewekeza katika uzalishaji wa vinywaji baridi vyenye gesi pamoja na vifungashio vya plastiki. Mitambo ya kiwanda hicho ina uwezo wa kuzalisha chupa 12,000 za vinywaji baridi kwa saa, huku kampuni ikitarajia kuzalisha ajira za moja kwa moja 100 na ajira nyingine 200 zisizo za moja kwa moja kadri shughuli zake zitakavyopanuka.

Aidha, kampuni hiyo imeeleza kuwa inatumia zaidi ya asilimia 90 ya malighafi zinazopatikana nchini, hatua inayochangia kuimarisha mnyororo wa thamani wa uzalishaji wa ndani. Kampuni pia inalenga kuongeza mauzo yake hadi Sh bilioni 15.4 ifikapo mwaka 2027 na Sh bilioni 33 ifikapo mwaka 2030, kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa katika uzinduzi huo.

Uwekezaji wa Simba Beverages Limited unaonesha nafasi ya sekta binafsi katika kuendeleza viwanda nchini, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi unaotegemea uzalishaji wa bidhaa na matumizi ya rasilimali zinazopatikana ndani ya nchi. Serikali inaendelea kuhimiza wawekezaji kutumia malighafi za ndani, kuongeza thamani ya bidhaa, kuhamisha teknolojia na kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya sekta ya viwanda.
































Na Mwandishi Wetu
BANDARI SACCOS, kwa kushirikiana na Bandari Foundation, imeendelea kuimarisha ushirikiano na jamii kupitia shughuli za uchangiaji damu, upimaji wa afya bila malipo na utoaji wa elimu ya afya. Shughuli hizo ni sehemu ya juhudi za kuboresha ustawi wa wananchi na kuwasaidia kupata huduma muhimu za kijamii.

Akizungumza katika viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar Es Salaam leo Oktoba 26, 2026 kuhusu shughuli hizo, Mtendaji Mkuu wa Bandari SACCOS na mjumbe wa Bandari Foundation, Godfrey Rwehumbiza, amesema taasisi hizo zimejipanga kuhamasisha wananchi kujitokeza kuchangia damu, huku zikiendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa zoezi hilo, vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa na mchango wa uchangiaji damu katika kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

Rwehumbiza amesema shughuli hizo pia zinahusisha upimaji wa afya bila malipo, kwa kushirikiana na wadau wa afya, wakiwamo Hospitali ya Bandari na Hospitali ya Temeke, ili kuwawezesha wananchi kufahamu hali zao za kiafya na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu.

Kwa upande wake, Mwanachama wa Bandarini Saccos na mwanachama pia wa Bandarini Foundation, Juhudi Nyambuka amesema wananchi watapata elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, yakiwamo magonjwa ya moyo na kisukari, pamoja na umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza na kuchukua hatua stahiki mapema.

Nyambuka amesisitiza kuwa huduma hizo hazilengi watu wanaotaka kuchangia damu pekee, bali pia wananchi wanaohitaji kupima afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu. Hivyo, amewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kujifunza zaidi kuhusu afya zao na namna ya kujikinga na magonjwa mbalimbali.

Aidha, amesema waandaaji wameweka utaratibu wa kufikisha huduma za uchangiaji damu katika maeneo mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wake. Taasisi, vikundi na maeneo yenye watu wasiopungua 10 wanaohitaji huduma hiyo yanaweza kutoa taarifa kwa waandaaji ili timu ya wataalamu ifike walipo na kutekeleza zoezi hilo.

Amesema utaratibu huo unalenga kuwafikia wananchi ambao wanaweza kushindwa kufika katika kituo kikuu cha shughuli hizo, huku akieleza kuwa huduma hizo zitapatikana katika maeneo yatakayopangwa kwa kushirikiana na waandaaji.

Kwa mujibu wa wazungumzaji hao, shughuli hizo zinatarajiwa kuendelea hadi Oktoba 19, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchangiaji damu na kutumia huduma za afya zinazotolewa.

Mbali na huduma za afya, Bandari SACCOS na Bandari Foundation zinaendelea kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kutoa elimu ya fedha kwa jamii. Wananchi pia watapata fursa ya kufahamu huduma na masharti ya kujiunga na Bandari SACCOS, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hizo kuimarisha ustawi wa jamii.




Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph, amesema wizi wa mita za maji ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili mamlaka hiyo, baada ya zaidi ya mita 100 kuibwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

Amesema takwimu za DUWASA zinaonesha kuwa vitendo hivyo vinaendelea kuwa changamoto katika usimamizi wa huduma za maji, huku baadhi ya vifaa vinavyoibwa vikidaiwa kutumika kwa shughuli nyingine zisizohusiana na matumizi yake ya awali.

Mhandisi Joseph, ameyazungumza hayo leo jijini Dodoma katika Mkutano na waandishi wa habari ambapo amesema ufuatiliaji uliofanywa umebaini kuwa baadhi ya mita hizo hutumika kutengeneza bangili, huku nyingine zikiishia kuuzwa kama vyuma chakavu. Hali hiyo inaibua wasiwasi kuhusu uharibifu wa vifaa vinavyotumika katika utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, DUWASA imekubaliana na baadhi ya wateja kufunga mita za maji ndani ya nyumba au katika maeneo yenye ulinzi, ikiwa ni hatua ya kupunguza uwezekano wa vifaa hivyo kuibwa. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mita zinakuwa salama huku mamlaka ikiendelea kutoa huduma kwa wateja wake.

Hata hivyo, Mhandisi Joseph amesema utaratibu wa kufunga mita ndani ya nyumba nao una changamoto zake, hasa pale watumishi wa DUWASA wanapohitaji kuingia katika maeneo ya wateja kwa ajili ya kufanya usomaji wa mita. Amesema baadhi ya wananchi hawatoi ushirikiano unaohitajika, hali inayowapa watumishi hao wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yao.

Ameeleza kuwa katika baadhi ya matukio, watumishi wanaofika kufanya usomaji wa mita hukumbana na mazingira yasiyo rafiki, ikiwemo kufunguliwa mbwa, jambo linaloweza kuwazuia kutekeleza majukumu yao kwa urahisi. Kutokana na hali hiyo, ushirikiano wa wananchi unahitajika katika kulinda mita za maji, kurahisisha usomaji wake na kuimarisha utoaji wa huduma. DUWASA inaendelea kukabiliwa na jukumu la kuhakikisha vifaa hivyo vinalindwa dhidi ya wizi huku wananchi wakitakiwa kutoa ushirikiano kwa watumishi wake.






Na Mwandishi Wetu, Korogwe

WANANCHI wa Kijiji cha Vuje, kilichopo Kata ya Bungu Korogwe Vijijini, wameingia kwenye furaha kubwa baada ya kushuhudia mkandarasi akabidhiwa rasmi mradi wa maji wa shilingi milioni 107.65 utakaokomesha adha ya ukosefu wa huduma hiyo iliyodumu kwa zaidi ya miongo mitano tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1972.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi katika hafla hiyo ya kihistoria iliyovuta hisia za wengi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Vuje, Muhammad Dhahabu, alieleza namna jamii ilivyoteseka kwa muda mrefu kusaka maji na kupoteza imani kutokana na ahadi za mara kwa mara zilizokosa utekelezaji, akimshukuru Mbunge wa Jimbo, Timotheo Mnzava, kwa kuwatendea haki.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bungu, Stephen Mdoe, licha ya kuishukuru serikali kwa uamuzi huo wa kishujaa, aliwasilisha kilio cha wananchi kuhusiana na uhaba wa maeneo ya kilimo kufuatia mashamba ya chai yaliyozunguka kijiji hicho kutelekezwa na wakulima kupigwa marufuku kuyatumia kwa mazao ya muda mfupi kama mahindi na magimbi.


Akiweka wazi takwimu za mradi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe, Muharami K. Mohamedi, alieleza kuwa mradi huo unatekelezwa na kampuni ya kizalendo ya Amani Civil and Water Works, ukilenga kuwanufaisha wakazi 1,297 kupitia ukarabati wa banio huko Sakale, matanki ya maji, na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 4.5 kwa kipindi cha miezi mitatu.


Akihutubia kwa niaba ya Mbunge Mnzava, mwakilishi wake Shebila Idd — ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira — alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowawezesha wakazi wa Vuje kulala kwa amani, huku wananchi wakicheza na kuimba nyimbo za kumsifu kiongozi huyo mkuu wa nchi.


"Rais Samia amedhihirisha kuwa yeye ni daktari wa kutatua na kutibu changamoto mbalimbali zinazotukabili sisi wananchi, hakika ni mama msikivu sana," alisema Shebila.

Shebila aliwataka wananchi wa Korogwe kuendelea kumlinda na kumuunga mkono Mbunge Mnzava, akisisitiza kuwa amefanya makubwa yaliyowashinda watangulizi wake katika sekta za maji, umeme, barabara, afya na elimu, jambo linalofanya jimbo hilo kupiga hatua kubwa za maendeleo.


"Mheshimiwa Mnzava ni mbunge tunatakiwa tumlinde, asituponyoke, tumuunge mkono, kazi zetu tunazomtuma anazifanya, waliomtangulia hawakuwa na Kasi kama yake," alisema Shebila.

Akizungumza kwa njia ya simu na wananchi hao, Mbunge Timotheo Mnzava alisisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo ni uthibitisho tosha wa namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyotatua kero za wananchi kwa vitendo.


"Leo (Oktoba 25, 2026), tumefanya jambo kubwa na la kipekee kukabidhi mradi huu wa maji, tumshukuru sana mhe Rais kwa anajali matatizo ya wananchi wake," alisema.

Mnzava alisema alipofika katika Kijiji hicho alipopewa kero ya maji hakuwa akipata usingizi na anamshukuru Rais kumpatia fedha ambazo zimeweza kutimiza ahadi yake.


Mnzava alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni wa pamoja na diwani na Mwenyekiti wa Kijiji hicho ambaye alikuwa akifuatilia kuona fedha zinapatikana ili wananchi waondokane na kero hiyo.

Mbunge huyo aliwataka wakazi wa Vuje kushirikiana kwa karibu na mkandarasi ili kazi ikamilike kwa ubora uliokusudiwa.

NA DENIS MLOWE - MVOMERO 


MKUU wa Wilaya ya Mvomero, Richard Kasesela, amewahimiza wanawake wa wilaya hiyo kutumia rasilimali walizonazo kujitengenezea mitaji ya kuanzisha na kukuza biashara, badala ya kusubiri mikopo kutoka taasisi za kifedha zenye masharti, huku akiwataka kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha ili kujikwamua kiuchumi.

Kasesela ametoa rai hiyo wakati akifungua Kongamano la Wanawake wa Tarafa ya Mlali lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, akisisitiza kuwa mtaji haupaswi kutazamwa kwa upande wa fedha pekee, bali pia thamani ya vitu ambavyo mtu anamiliki lakini havitumiki ipasavyo.

Amesema wanawake wanaweza kuanza kujikusanyia mitaji kwa kuuza vitu vilivyohifadhiwa majumbani kwa muda mrefu bila kutumika, vikiwemo nguo, viatu na vitu vingine vyenye thamani, kisha kuelekeza fedha watakazopata katika shughuli za uzalishaji na biashara.

“Si kwamba vitu hivyo havina thamani, vina thamani lakini havina tija kama havitumiki. Kwa nini usivitoe ukaviuza na kupata mtaji wa kuanzia?” amesisitiza Kasesela.

Akieleza uzoefu wake binafsi, Kasesela amesema aliwahi kuuza nguo alizokuwa hazitumii na kupata karibu shilingi laki tatu na zaidi, akibainisha kuwa hatua hiyo inaonesha namna rasilimali zilizopo majumbani zinavyoweza kuwa chanzo cha mtaji wa kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Aidha, amewataka wanawake kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha kwa kupanga bajeti kabla ya kuanza shughuli za kila siku na kuepuka manunuzi yasiyokuwa kwenye mipango yao, akieleza kuwa matumizi yasiyopangwa yanaweza kuzuia fedha ambazo zingetumika kujenga mtaji.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum wa Tarafa ya Mlali, Rachael Kingu, amesema changamoto zinazowakabili wanawake wengi ni pamoja na ukosefu wa mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara, pamoja na kukosa elimu kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo yao.

Amesema kongamano hilo limelenga kuwapatia wanawake elimu kuhusu fursa hizo ili kuwawezesha kuzitumia kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Naye Diwani wa Kata ya Mzumbe, Stanslaus Matangalu, ameshukuru Serikali kwa juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa makundi maalumu.

Matangalu amesema katika Kata ya Mzumbe, zaidi ya shilingi milioni 100 zimetolewa kwa vikundi sita vya wanawake, vikundi viwili vya vijana na kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu.

Katika kongamano hilo, washiriki wamepatiwa elimu kuhusu fursa za kiuchumi na masuala mbalimbali kutoka kwa wataalamu wa taasisi zilizoshiriki, zikiwemo Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), SAT, Benki ya CRDB na Benki ya NMB.