Na FARIDA MANGUBE, MOROGORO
MKUU wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Queen Sendiga, amezindua rasmi namba maalumu ya simu itakayotumika na wananchi kupiga na kutoa kero, changamoto na maoni yao ili yaweze kupatiwa ufumbuzi kwa haraka.

Mhe. Sendiga amezindua huduma hiyo Novemba 9. 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Magadu, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mkoani humo.

Aidha amesema, hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati huku akisisitiza kuwa sasa ni wakati wa kuzifanyia kazi haraka changamoto zinazowakabili wananchi.

Amebainisha kuwa namba yansimu watakayotumia wananchi kuwasilisha kero zao bila malipo ni 0800114045 huku akibainisha kuwa gharama za kupiga simu hiyo bure imegharimiwa na Serikali.

Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limeiomba Serikali kuimarisha mfumo wa Tiba Asilia na Tiba Mbadala nchini kwa kuwekeza katika elimu, tafiti za kisayansi, udhibiti wa ubora wa dawa, uhifadhi wa mimea tiba na uwekezaji katika sekta hiyo.

Katika waraka wa mapendekezo ya kimkakati uliotolewa Novemba 2026, TRAMEPRO imependekeza Tanzania kujifunza kutoka Jamhuri ya India, ambayo imepiga hatua katika kurasimisha na kuendeleza mifumo ya tiba za jadi kupitia Wizara maalumu ya AYUSH.

Shirika hilo limeeleza kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa mimea tiba na maarifa ya jadi yaliyorithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, lakini bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili sekta hiyo iweze kuchangia kikamilifu katika afya ya jamii na uchumi wa taifa.

Miongoni mwa changamoto zilizobainishwa ni upungufu wa tafiti za kisayansi, mifumo ya mafunzo na viwango vya kitaaluma, vifaa vya kupima ubora wa bidhaa, pamoja na uharibifu wa mazingira unaosababisha kupungua kwa baadhi ya mimea tiba.

TRAMEPRO imependekeza pia kuimarishwa kwa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa kuongeza rasilimali watu, fedha, vifaa na mifumo ya kidijitali ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Aidha, shirika hilo limetaka kuanzishwa kwa mfumo wa mafunzo ya kitaaluma utakaowawezesha wataalamu wa tiba asili kupata elimu ya kisasa kuhusu usalama wa wagonjwa, matumizi sahihi ya dawa, maadili ya taaluma na umuhimu wa kuwapeleka wagonjwa kwenye huduma za kisasa pale inapohitajika.

Katika eneo la utafiti, TRAMEPRO imependekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), vyuo vikuu, taasisi za afya na wataalamu wa tiba asili ili kuchunguza kisayansi mimea tiba, viambato vyake, usalama na ufanisi wake.

Kwa upande wa uchumi, shirika hilo limehimiza Serikali kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mimea tiba, maabara za kupima ubora, uzalishaji wa bidhaa zenye viwango na upanuzi wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, TRAMEPRO imependekeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kuanzisha mazungumzo rasmi na Wizara ya AYUSH ya India ili kuwezesha kubadilishana uzoefu, mafunzo, teknolojia, tafiti za pamoja na fursa za uwekezaji.

Waraka huo pia unapendekeza utekelezaji wa mpango wa miaka mitano kuanzia 2027 hadi 2031, utakaoanza na tathmini ya mfumo uliopo, kuimarisha taasisi na mifumo ya udhibiti, kuendeleza tafiti na uzalishaji, kukuza uwekezaji na hatimaye kufanya tathmini ya matokeo.

TRAMEPRO imeiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kupokea na kutathmini mapendekezo hayo, kuitisha mkutano wa kitaifa wa wadau wa Tiba Asilia na Tiba Mbadala, pamoja na kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala, Sura ya 244.

Akieleza msimamo wa shirika hilo, Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, Boniventura F. Mwalongo, amesema maendeleo ya sekta hiyo yanapaswa kujengwa kwa ushirikiano wa Serikali, wataalamu, taasisi za utafiti, vyuo vikuu na sekta binafsi.

Amesisitiza kuwa lengo la mapendekezo hayo si kuiga mfumo wa India, bali kujifunza kutokana na uzoefu wake na kujenga mfumo wa Tanzania unaozingatia mazingira, rasilimali na mahitaji ya nchi.

Kauli mbiu ya waraka huo ni: “Tuisimamie Tiba Asili kwa Maarifa, Tuiendeleze kwa Sayansi, Tuilinde kwa Sheria na Tuikuze kwa Uchumi.”

Meneja wa Masuala ya Uendelevu  wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita ( GGML) Bw. Gilbert Mworia akizungumza  wakati wa mkutano wa kufanya tathmini ya fedha za GGM Kili Challenge  against HIV & AIDS uliojumuisha taasisi zilizopata fedha hizo kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.
Bi Neema Julius kutoka Taasisi ya Konga la Waviu Arusha akiwasilisha namna taasisi hiyo ilivyonufaika na  mgao wa fedha zilizotolewa  na kampeni ya GGM Kili Challenge Against HIV & AIDS  wakati wa tathmini ya kikao kinachoendelea Moshi, mkoani Kilimanjaro
Wadau wakifatilia mada

Na Mwandishi Wetu
MOSHI, KILIMANJARO – GGM Kilimanjaro Challenge Against HIV & AIDS Trust kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imeanza kufuatilia utekelezaji wa miradi ya taasisi/mashirika zilizopokea fedha kupitia kampeni hiyo kwa msimu wa mwaka 2025/26 ili kutathmini mafanikio, changamoto na matokeo ya uwekezaji huo katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini.

Ufuatiliaji huo unafanyika kupitia semina ya siku mbili katika Hoteli ya Weruweru, jijini Moshi, mkoani Kilimanjaro, itakayofuatiwa na ziara ya siku tatu katika maeneo mbalimbali yanakotekelezwa miradi ya taasisi/mashirika hayo.

Akizungumza katika semina hiyo, Mwenyekiti wa Timu ya Ufundi, ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa TACAIDS, Bw. Nyangusi Laiser, alisema rasilimali zinazopatikana kupitia kampeni hiyo ni muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini.

Alisema licha ya hatua zilizopigwa katika kupunguza maambukizi, ugonjwa huo bado ni changamoto, huku vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wakiwa miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya maambukizi.

Aliongeza kuwa wanawake ndio kundi lilioathiriwa zaidi, likiwakilisha asilimia 80 ya maambukizi yote nchini, yanayohusisha watu 1,548,000, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2023.

“Wote tunafahamu kuwa rasilimali fedha kutoka kwa mashirika ya kimataifa zilizokuwa zikitumika kusaidia mapambano dhidi ya UKIMWI barani Afrika zimepungua.

Hivyo, kampeni hii inayosimamiwa na GGML kwa zaidi ya miaka 24 ni muhimu katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kutokomeza ugonjwa huu nchini,” alisema Bw. Laiser.

Katika uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji, taasisi zilizopokea fedha kupitia kampeni hiyo zilieleza kuwa ufadhili huo umekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya watu wanaoishi na VVU na UKIMWI.

Aliisema fedha hizo zimewezesha kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa ajili ya kuongeza kipato, kutoa elimu kuhusu kujikinga na maambukizi mapya, kuhamasisha matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARV) na kurahisisha upatikanaji wa huduma katika vituo vya tiba na matunzo (CTC).

Akielezea mafanikio ya mradi wao, Afisa wa Kikundi cha Jali Afya Yako, Epuka Maambukizi Mapya, Fuata Ushauri na Nasaha (KIJAEFA), Bw. Roymen Siria, alisema taasisi hiyo kupitia kampeni hiyo ya mwaka 2025/26 ilipokea mgao wa Sh milioni 30 ambazo zimewekezwa katika mradi wa uzalishaji wa unga wa lishe kwa ajili ya kuimarisha afya ya jamii na kuongeza kipato cha wanufaika.

“Tumewekeza katika ununuzi wa vifaa mbalimbali na kuanzisha uzalishaji wa unga wa lishe kama njia ya kujiongezea kipato na wakati huohuo kuchangia kuboresha afya ya jamii,” alisema Bw. Siria.

Alisema kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kusajili bidhaa zao katika taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili ziweze kukidhi vigezo vinavyohitajika na kuingia katika masoko ya kitaifa na kimataifa.

Aliongeza kuwa ukosefu wa kipato ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili watu wanaoishi na VVU, hivyo mradi huo unalenga kuwapatia fursa za kiuchumi zitakazowasaidia kujitegemea na kuboresha maisha yao.

Kwa upande wake, Bi. Neema Julius kutoka taasisi ya Konga la Waviu Arusha, ambayo pia ni mnufaika wa fedha hizo, alisema taasisi yao imejikita katika kutoa elimu kuhusu VVU na UKIMWI, kuhamasisha upimaji wa afya katika kaya na kuwaunganisha watu wanaobainika kuwa na maambukizi na huduma stahiki za matibabu.

“Taasisi yetu inajikita zaidi katika kutoa elimu kuhusu VVU na UKIMWI, kufanya upimaji wa afya katika kaya na kutoa rufaa kwa watu wanaobainika kuwa na maambukizi ili waweze kupata huduma sahihi katika vituo vya afya,” alisema Bi. Julius.

Alisema ufadhili huo umeongeza uwezo wa watoa huduma wa taasisi hiyo kuwafikia wananchi wengi zaidi na kutoa elimu inayolenga kupunguza maambukizi mapya na athari za VVU na UKIMWI katika jamii.

Akizungumzia mchango wa kampeni hiyo, Meneja wa Kili Trust, Bw. Stephen Mhando, alisema fedha zinazotolewa kwa taasisi hizo zinatokana na kampeni ya kuchangisha fedha kupitia kampeni ya kupanda mlima Kilimanjaro inayofanyika kila mwaka kwa njia ya miguu na baiskeli.

Alisema kampeni hiyo inalenga kukusanya rasilimali fedha kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa afua mbalimbali za mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali.

“Tumeendesha kampeni hii kwa zaidi ya miaka 24 sasa, huku ushirikiano wetu na TACAIDS ukiwa umeanza mwaka 2014. Lengo letu ni kuhakikisha ndoto ya kuwa na Tanzania isiyo na maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vinavyotokana na Ukimwi inatimia,” alisema Bw. Mhando.

Alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na michango ya taasisi na mashirika mbalimbali, bado kuna haja ya wadau kuendelea kushirikiana kwa kuwa maambukizi ya VVU bado yapo nchini.

“Ni muhimu wadau wote tuendelee kushikana mikono na kuimarisha juhudi hizi ili kuifanya Tanzania kuwa salama dhidi ya VVU na UKIMWI,” alisisitiza.

Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Uendelevu wa GGML, Bw. Gilbert Mworia, alisema upatikanaji wa rasilimali fedha ni nguzo muhimu katika kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, akizitaka taasisi, mashirika na vikundi vinavyotekeleza afua mbalimbali kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayoviwezesha kupata fedha dhidi ya mapambano hayo.

Alisema hatua hiyo itasaidia taasisi hizo kuendelea kutoa huduma kwa jamii hata pale ufadhili kutoka nje unapopungua au kukosekana.

“Tunawashauri kutumia fursa ya uwezeshaji unaotokana na kampeni ya GGM Kili Challenge kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayowapatia rasilimali fedha, ili muweze kuendelea kuhudumia jamii katika maeneo yenu hata kama ufadhili kutoka nje utapungua au kukatika,” alisema Bw. Mworia.

Akifafanua kuhusu madhumuni ya semina na ziara hiyo, Afisa Utawala wa kampeni ya Kili Challenge, Bi. Njile Mabula, alisema kukutana na taasisi wanazozisaidia pamoja na kutembelea maeneo yao ya utekelezaji ni utaratibu wa kila mwaka unaolenga kutathmini maendeleo ya miradi hiyo.

Alisema ziara hizo pia hutoa fursa ya kubaini mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji maboresho ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika ipasavyo na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, amekagua ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mbinga wenye thamani ya Shilingi bilioni 3.7, ambapo majengo 15 kati ya 29 yamekamilika tangu mradi huo uanze mwaka 2021.

Katika ziara hiyo, ameuagiza uongozi wa Halmashauri kutumia sehemu ya mapato yake ya ndani, yanayofikia wastani wa Shilingi bilioni 14.7 kwa mwaka, kuharakisha ukamilishaji wa baadhi ya  majengo hasa nyumba za wafanyakazi  badala ya kutegemea fedha za Serikali Kuu pekee.

Aidha, amepongeza mafanikio katika kuboresha huduma za uzazi na kupunguza vifo vya mama na mtoto vilivyoripotiwa hospitalini hapo kutoka 550 Kabla ya ujenzi wa hospitali hiyo hadi 106 tangu hospitali ilipoanza kutoa huduma. Akieleza sababu za idadi ya Vifo, Mganga Mkuu katika hospitali hiyo amesema  idadi kubwa ya Vifo inatokana na wajawazito kujifungulia nyumbani.

Akifikisha salamu za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wagonjwa, Makamu wa Rais amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha miundombinu na huduma za afya ili kulinda maisha ya mama na mtoto.









▪️ Ataka walimu wawili waliojitolea kwa zaidi ya miaka mitano waajiriwe kutokana na mchango wao katika ufaulu

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amevitaka vikundi vya Sungusungu kutowatenga wananchi wala kuwalazimisha kushiriki taratibu zinazokinzana na imani zao, akionya kuwa vitendo hivyo vinaweza kusababisha mgawanyiko katika jamii.

Ametoa maelekezo hayo leo (Jumanne, Novemba 10, 2026), wakati akisikiliza kero za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Singita, Kata ya Usanda, Jimbo la Itwangi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

“Kama mtu imani yake haimruhusu kuchanja, kwa kweli tusimlazimishe. Na wala tusimtenge,” amesema.

Maelekezo hayo yamefuatia malalamiko ya mwananchi, Simon John, aliyedai kuwa mchungaji wake ametengwa baada ya kukataa kushiriki baadhi ya taratibu za Sungusungu, huku waumini wakizuiwa kwenda kusali kwake.

Akizungumza na kiongozi wa Sungusungu aliyekuwapo mkutanoni, Waziri Mkuu amemtaka kuhakikisha mchungaji huyo hatengwi na anaendelea kupewa ulinzi.

“Msisumbuane na mchungaji mmoja huyo. Mpeni na ulinzi, wala msimtenge,” amesema.

Dkt. Mwigulu ameelekeza vikundi vya Sungusungu kuwaruhusu waumini, wakiwemo wanachama wa vikundi hivyo, kwenda kusali kwa mchungaji huyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru wa imani na ibada.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema atamwandikia Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais–Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ili walimu wawili wa kujitolea waliochangia Shule ya Msingi Masunula kushika nafasi ya pili kitaifa waajiriwe.

Shule hiyo ipo Kijiji cha Masunula, Kata ya Usule, wilayani Shinyanga. Amesema ameelezwa kuwa walimu hao wamefundisha kwa kujitolea kwa zaidi ya miaka mitano katika shule hiyo yenye walimu saba.

“Hawa waajiriwe kwa sababu tumeona matokeo yake,” amesema.

Amewapongeza walimu, wanafunzi na viongozi kwa mafanikio hayo, huku akielekeza tathmini ya gharama za ujenzi wa nyumba yenye makazi ya walimu wawili ifanyike na kuwasilishwa kupitia Katibu Tawala wa Mkoa ili kupunguza changamoto ya makazi katika shule hiyo.

Kuhusu huduma za afya, Waziri Mkuu amemwelekeza Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga kuwasilisha siku hiyo hiyo maombi maalumu ya ujenzi wa vituo viwili vya afya katika kata za Usule na Didia.

Vilevile, ameahidi kutafuta shilingi milioni 76 za kukamilisha Zahanati ya Mwamkanga ili wananchi waanze kupata huduma.








Na Pamela Mollel, Arusha

WAKULIMA wametakiwa kuongeza uzalishaji kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya viwanda na masoko nje ya nchi kwani kuna fursa kubwa ya masoko kutokana na ongezeko la mahitaji kwa ajili ya usindikaji wa vyakula na upanuzi wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa jijini Arusha leo na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Darsh Industries Limited inayozalisha bidhaa za vyakula kupitia chapa ya Red Gold ,Bhadresh Pandit wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, linalofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha.

Bhadresh amesema kampuni hiyo ina viwanda viwili vilivyopo Arusha na Iringa, vinavyoshirikiana kwa karibu na wakulima ili kupata mazao yanayotumika kuzalisha bidhaa mbalimbali za chakula.

Ameongeza kuwa ,kampuni hiyo inahitaji mazao yakiwemo nyanya, pilipili mbuzi, pilipili mwendokasi, karanga na matunda mbalimbali kama machungwa, mananasi na matunda damu, ambayo hutumika kama malighafi katika uzalishaji.

Ameeleza kuwa kupitia mazao hayo kampuni huzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo michuzi (sauces), jam na bidhaa nyingine za vyakula, huku ikiendelea kuimarisha uzalishaji wa bidhaa zilizoandaliwa kwa matumizi ya moja kwa moja (Ready to Eat).

"Moja ya malengo ya kushiriki maonesho hayo ni kutangaza bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo, pamoja na kukutana na wakulima ili kujenga ushirikiano utakaowawezesha kulima mazao yenye soko la uhakika."amesema Bhadresh.

Amesisitiza kuwa kilimo kina fursa kubwa ya kibiashara, hivyo wakulima wanapaswa kuongeza uzalishaji ili kunufaika na mahitaji ya viwanda vinavyotegemea mazao ya ndani.

Akizungumzia fursa za soko, amesema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani inatarajiwa kuongeza idadi ya wageni watakaotembelea nchi na kutumia huduma mbalimbali ikiwemo hoteli, ambazo ni miongoni mwa maeneo yanayopatikana bidhaa za kampuni hiyo.

Ameongeza kuwa, ongezeko la wageni na matumizi ya bidhaa hizo linaweza kuongeza mauzo ya kampuni, kupanua uzalishaji na kutoa nafasi ya kuongeza ajira kwa Watanzania.

"Ukuaji wa biashara hiyo utaongeza pia manunuzi ya mazao kutoka kwa wakulima wa ndani na kuchangia mapato ya serikali kupitia ulipaji wa kodi."amesema Bhadresh.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutumia bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo kwa wingi ili kusaidia kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kupanua soko la mazao yanayozalishwa na wakulima.

Aidha ameiomba serikali kuendelea kuwawezesha wakulima na kutatua changamoto zinazowakabili ili waweze kuzalisha mazao kwa wingi na ubora unaohitajika na viwanda.

Amesema kampuni hiyo tayari inauza bidhaa zake katika nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi na Zambia, huku ikilenga kupanua zaidi masoko yake.

Amesisitiza kuwa ili kufikia malengo hayo, ni muhimu kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima, viwanda na serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za kutosha, kukuza uzalishaji wa ndani na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Amefafanua kuwa ,kiwanda hicho cha kusindika nyanya kilichopo mkoani Iringa kina uwezo wa kuchakata zaidi ya tani 250 za nyanya kwa siku, huku kikiendelea kupokea mazao kutoka kwa wakulima wanaotaka kuingia katika ushirikiano wa kibiashara na kampuni hiyo.

Mkurugenzi wa masoko wa kampuni hiyo, Darsh Pandit amewahamasisha vijana nchini kuwekeza katika kilimo kwa kuwa ni sekta yenye fursa kubwa za kiuchumi, huku ikiwataka wakulima kutumia fursa ya kuuza mazao yao moja kwa moja viwandani.

Pandit, amesema kampuni hiyo inajihusisha na usindikaji wa mboga na matunda kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali za chakula.

"Kampuni hii inazalisha bidhaa zaidi ya 40, zikiwemo tomato paste, tomato sauce, pilipili na siagi ya karanga (peanut butter), huku bidhaa zake zikitambulika kupitia chapa ya Red Gold ambayo imepata hadhi ya Superbrand katika Afrika Mashariki."amesema Pandit.

Amesema kampuni hiyo imewekeza katika viwango vya ubora kwa kupata vyeti vya TBS, ISO na Halal, hatua inayolenga kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa katika masoko ndani na nje ya nchi.

"Kampuni yetu inashirikiana na wakulima zaidi ya 5,000 kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Iringa, Morogoro na Arusha, ambapo hununua mazao moja kwa moja kutoka kwa wakulima ili kuhakikisha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji."amesema .

Amefafanua kuwa, kiwanda chao cha kusindika nyanya kilichopo mkoani Iringa kina uwezo wa kuchakata zaidi ya tani 250 za nyanya kwa siku, huku kikiendelea kupokea mazao kutoka kwa wakulima wanaotaka kuingia katika ushirikiano wa kibiashara na kampuni hiyo.

Ameongeza kuwa kiwanda kikuu cha kampuni hiyo, kipo eneo la Njiro jijini Arusha na kuwataka wakulima wenye mazao yanayohitajika kufika viwandani hapo ili kupata maelekezo kuhusu namna ya kuanzisha ushirikiano wa kibiashara.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Darsh Industries Limited ,Bhadresh Pandit akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, linalofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha.





Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read Tanzania, Bi. Joan Ndaambuyo Minja (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba (kulia) wakisaini hati ya makubaliano kupanua ushirikiano eneo la uimarishaji wa stadi za kusoma na kuandika kwa watoto, pamoja na kukuza stadi za maisha na usawa wa kijinsia kwa vijana, hususan wasichana, hafla iliyofanyika ofisi za TET jijini Dar es Salam.


Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read Tanzania, Bi. Joan Ndaambuyo Minja (kushoto) akibadilishana nyaraka na Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba (kulia) mara baada ya kusaini hati ya makubaliano kupanua ushirikiano eneo la uimarishaji wa stadi za kusoma na kuandika kwa watoto, pamoja na kukuza stadi za maisha na usawa wa kijinsia kwa vijana, hususan wasichana, hafla iliyofanyika ofisi za TET jijini Dar es Salam.



Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read Tanzania, Bi. Joan Ndaambuyo Minja na Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba (kulia) wakionesha hati za makubaliano mara baada ya kuzisaini kwenye ofisi za TET jijini Dar es Salam.

SHIRIKA la Room to Read, limeingia makubaliano na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), ikiwa ni sehemu ya kuendeleza, kuimarisha na kupanua ushirikiano eneo la uimarishaji wa stadi za kusoma na kuandika kwa watoto, pamoja na kukuza stadi za maisha na usawa wa kijinsia kwa vijana, hususan wasichana.

Akizungumza katiha hafla hiyo leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkazi wa Room to Read, Bi. Joan Ndaambuyo Minja alisema wanatambua na kuthamini dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora, jumuishi na yenye kumjengea maarifa, stadi na uwezo wa kushiriki katika maendeleo ya Taifa, hivyo lina kila sababu ya kuunga mkono juhudi hizo.

Alisema shirika hilo linauchukulia ushirikiano na Serikali kuwa ni sehemu ya kutekeleza vipaumbele vya kitaifa katika sekta ya elimu, badala ya kuwa utekelezaji wa programu za Room to Read moja kwa moja.

“…Leo ni siku muhimu katika historia ya ushirikiano kati ya Taasisi ya Elimu Tanzania na Shirika la Room to Read Tanzania. Utiaji saini wa Hati hii ya Makubaliano unaweka msingi rasmi wa kuendeleza, kuimarisha na kupanua ushirikiano wetu katika maeneo mawili muhimu: uimarishaji wa stadi za kusoma na kuandika kwa watoto, pamoja na kukuza stadi za maisha na usawa wa kijinsia kwa vijana, hususan wasichana,” alisema, Bi. Minja.

Alibainisha kuwa makubaliano waliosaini yanaendana na mwelekeo wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, inayosisitiza umuhimu wa elimu yenye ubora, usawa wa fursa, ujumuishi na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika kuendeleza elimu nchini.

Aliongeza kuwa Sera inatambua kuwa jukumu la kuboresha elimu si la Serikali pekee. Linahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, taasisi zake, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau wa maendeleo, wazazi na jamii kwa ujumla.

“…ushirikiano huu unaendana na matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga Taifa lenye watu wenye maarifa, ujuzi, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii. Dira hii inatukumbusha umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu kuanzia hatua za awali za ujifunzaji, kuimarisha elimu yenye ubora na kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume, wasichana na wavulana wanapata fursa sawa za kujifunza, kuendeleza vipaji vyao na kushiriki katika maendeleo ya Taifa,” amesisitiza, Bi. Joan Minja.


Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read Tanzania, Bi. Joan Ndaambuyo Minja (kulia) akizungumza kwenye hafla ya kusaini hati ya makubaliano kupanua ushirikiano eneo la uimarishaji wa stadi za kusoma na kuandika kwa watoto, pamoja na kukuza stadi za maisha na usawa wa kijinsia kwa vijana, hususan wasichana, naTaasisi ya Elimu Tanzania (TET).


Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read Tanzania, Bi. Joan Ndaambuyo Minja (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba (kulia) wakisaini hati ya makubaliano kupanua ushirikiano eneo la uimarishaji wa stadi za kusoma na kuandika kwa watoto, pamoja na kukuza stadi za maisha na usawa wa kijinsia kwa vijana, hususan wasichana, hafla iliyofanyika ofisi za TET jijini Dar es Salam.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba akizungumza katika hafla hiyo, alisema miongoni mwa malengo makuu ya Hati ya Makubaliano waliosaini ni Kushirikiana katika uandaaji, kupitia na kuhuisha vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili viendane na viwango vya Mitaala ya Taifa, kwa kuzingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, na Mwongozo wa Kitaifa wa Mitaala ya ElimuMsingi, kwa lengo la kuimarisha ubora na ufanisi wa ujifunzaji wa stadi za msingi.

Alisema mengine muhimu waliokubaliana na katika ushirikiano huo ni, kuimarisha umahiri wa walimu kupitia mifumo ya mafunzo ya ualimu kabla ya kuanza kazi na mafunzo endelevu kwa walimu walio kazini, kwa kuandaa na kutekeleza mafunzo kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa Maendeleo na Usimamizi wa Walimu pamoja na vipaumbele vya kitaifa vya kuimarisha umahiri wa walimu na kuboresha ufundishaji na ujifunzaji darasani.

Aidha alibainisha na

Pia tumekubaliana; kuwezesha upatikanaji wa elimu bora kwa usawa na bila ubaguzi, kwa kuzingatia mahitaji ya kijinsia, kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia pamoja na vipaumbele vya elimu jumuishi vilivyoainishwa.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read Tanzania, Bi. Joan Ndaambuyo Minja (kushoto) akibadilishana nyaraka na Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba (kulia) mara baada ya kusaini hati ya makubaliano kupanua ushirikiano eneo la uimarishaji wa stadi za kusoma na kuandika kwa watoto, pamoja na kukuza stadi za maisha na usawa wa kijinsia kwa vijana, hususan wasichana, hafla iliyofanyika ofisi za TET jijini Dar es Salam.
Picha ya pamoja.


NA MWANDISHI WETU

BODI ya Korosho Tanzania (CBT) imewahakikishia wawekezaji wanaojenga viwanda vya kubangua korosho nchini kuwa watapata malighafi za kutosha kuendesha shughuli zao, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uwezo wa viwanda vya kubangua korosho nchini ifikapo mwaka 2030.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Francis Alfred, amesema bodi itahakikisha wawekezaji wanaotumia fedha nyingi kujenga viwanda hawajikuti wakishindwa kuviendesha kutokana na uhaba wa korosho ghafi.

Alfred ametoa kauli hiyo Novemba 7, 2026, mkoani Mtwara, wakati wa kikao cha wadau wa korosho kilichoandaliwa na Benki ya NMB, kikihusisha wabanguaji, wanunuzi na wafanyabiashara kujadili fursa za ufadhili zinazolenga kutatua changamoto katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Amepongeza hatua ya NMB kuwakutanisha wadau hao, akisema ushirikiano kati ya taasisi za fedha na wafanyabiashara wa korosho ni muhimu katika kuongeza uzalishaji na kufanikisha azma ya nchi ya kupanua uwezo wa viwanda vya kubangua korosho ifikapo mwaka 2030.

Aidha, amezihimiza taasisi nyingine za fedha kuwa karibu na wadau wa sekta hiyo ili kutambua mahitaji yao na kutoa masuluhisho yanayochochea ukuaji wa biashara.

Alfred pia amezitaka benki kuhakikisha malipo ya wakulima yanafanyika kwa wakati ili kuwawezesha kutimiza mahitaji yao ya kifedha na kujiandaa kwa shughuli zinazofuata za uzalishaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Biashara ya Kilimo kwa Wateja Wakubwa wa Benki ya NMB, Christopher Mwalugenge, amesema benki hiyo imejipanga kusaidia biashara za korosho katika msimu wa 2026/2027 kupitia masuluhisho mbalimbali ya kifedha.

Amesema huduma hizo zinalenga kuwawezesha wanunuzi wa korosho kupitia minada na masoko ya awali kupata mitaji ya kununua mazao kwa wakati na kwa kiwango kinachohitajika, huku wabanguaji wakipata fedha za kununua malighafi za kuendesha viwanda vyao.

Mwalugenge amesema NMB pia inatoa masuluhisho ya kifedha yanayokidhi mahitaji ya wasafirishaji wa korosho nje ya nchi, ili kuwawezesha kufanya manunuzi kwa wakati na kutekeleza mikataba yao ya biashara katika masoko ya kimataifa.

Ameongeza kuwa benki hiyo imeimarisha huduma zake za malipo na miamala ili kurahisisha shughuli za biashara katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani wa korosho.

Kikao hicho kinatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za fedha na wadau wa korosho, hususan katika kuongeza upatikanaji wa mitaji, kuchochea ubanguaji wa korosho nchini na kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati.













Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa vigae pamoja na masinki ya choo kutoka kampuni ya Twyford wenye thamani ya shilingi milioni 24, ikiwa ni sehemu ya mchango wa kampuni hiyo katika kuunga mkono juhudi za kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya. 


Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga wa MNH, Bi. Redempta Matindi, ameishukuru kampuni ya Twyford kwa kuonesha moyo wa kujali na kushirikiana na hospitali hiyo katika kuboresha mazingira ya kutolea huduma. Amesema msaada huo ni muhimu kwa kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha miundombinu na kuongeza ubora wa mazingira yanayotumiwa katika utoaji wa huduma.

Kwa upande wake, Riz Zhao Mkurugenzi Msaidizi wa kampuni ya Twyford ameeleza kuwa kampuni hiyo inatambua umuhimu wa kushirikiana na jamii pamoja na taasisi mbalimbali katika kuchangia maendeleo ya sekta muhimu nchini, ikiwemo sekta ya afya. Amesema msaada huo ni sehemu ya jitihada za kampuni hiyo kurejesha kwa jamii na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Muhimbili katika kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi. 

Muhimbili inaendelea kuthamini ushirikiano na michango inayotolewa na wadau mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya na kuboresha miundombinu yake. Ushirikiano huo unaonesha umuhimu wa wadau wa sekta binafsi kushiriki katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika mazingira salama na rafiki.