Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Miao Deyu, amewasili nchini Novemba 23, 2026, kwa ziara ya kikazi inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China, kupitia majadiliano kuhusu masuala mbalimbali yenye maslahi ya pamoja kwa nchi hizi mbili.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Miao alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe akiwa ameambatana na  Viongozi wengine kutoka Tanzania na China, akiwemo Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Dkt. Suleiman Haji Suleiman na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian.

Wakati wa ziara hiyo, masuala yatakayojadiliwa ni pamoja na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Wang Yi, iliyofanyika mwezi Januari, 2026,  maendeleo ya mradi wa ukarabati na uboreshaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), pamoja na maeneo mengine ya ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia.

Aidha, ziara hiyo itahusisha mkutano wa utatu kati ya Tanzania, China na Zambia, utakaotoa fursa kwa nchi hizo kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mradi wa TAZARA, ikiwemo utekelezaji wake na nafasi yake katika kukuza biashara, usafirishaji na maendeleo ya uchumi wa kikanda.

Katika kuenzi urafiki na mshikamano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China, Mhe. Miao pia atatembelea makaburi ya wataalam wa China yaliyopo Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, kwa heshima ya raia wa China waliopoteza maisha wakati wa kushiriki ujenzi wa Reli ya TAZARA.

Vilevile, atashiriki warsha maalumu kuhusu TAZARA itakayofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Wilayani Kibaha, mkoani Pwani.

Ziara hiyo inatarajiwa kutoa fursa ya kuendeleza majadiliano kuhusu masuala ya kipaumbele kwa mataifa hayo mawili, kuimarisha ushirikiano uliopo na kuweka msingi wa utekelezaji wa mipango ya pamoja yenye manufaa kwa wananchi wa Tanzania, China na Zambia.

























Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka, ameitaka Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM) kuendelea kuzalisha wataalamu wenye ubunifu, uadilifu na uwezo wa kutatua changamoto zinazolikabili Taifa kupitia teknolojia na mifumo mbalimbali.

Dkt. Isaka amesema wataalamu wanaozalishwa na vyuo wanapaswa kuwa sehemu ya kutafuta suluhisho la changamoto za jamii kwa kutumia maarifa waliyonayo, ikiwemo kubuni mifumo inayorahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Amesema hayo wakati wa Kongamano la Kitaaluma la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza umuhimu wa wataalamu kuzingatia uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema pamoja na kuwa na ufaulu mzuri kitaaluma, mtaalamu anapaswa kuwa na maadili na kujitambua ili aweze kutumia ujuzi wake katika kutatua changamoto za wananchi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Jamii ina changamoto nyingi ambazo wataalamu wetu wanapaswa kuzitumia kama fursa za kuzitatua kwa kubuni teknolojia na mifumo mbalimbali itakayorahisisha maisha ya watu,” amesema.

Aidha, amesema mabadiliko ya teknolojia na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 yanatoa fursa kwa IFM kuboresha mitaala yake ili kuzalisha vijana wenye uwezo wa ubunifu, uzalishaji na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Amesema NHIF itatoa fursa kwa wanafunzi 10 bora wa mwaka wa tatu wa IFM kufanya mafunzo ya vitendo katika taasisi hiyo ili kuwajengea uzoefu wa kazi na kuwaandaa kwa fursa za ajira na kujiajiri.

Kwa upande wake, Mkuu wa IFM, Profesa Henry Chalu, amesema chuo hicho kitaendelea kuimarisha mifumo ya elimu inayozalisha wataalamu wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo ya nchi.
Amesema kongamano hilo ni sehemu ya mkakati wa chuo kuhamasisha tafiti na ubunifu unaolenga kutatua changamoto katika sekta mbalimbali, huku wanafunzi wakipata fursa ya kuwasilisha mawazo na mifumo waliyoibuni.

Profesa Chalu amesema chuo kinaendelea kusimamia misingi ya elimu inayowawezesha wanafunzi kutumia maarifa yao katika mazingira halisi ya kazi na kujibu mahitaji ya jamii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano hilo, Dkt. Shaban Ngole, amesema kongamano hilo limekuwa na mawasilisho mbalimbali yanayolenga kuonesha ubunifu wa wanafunzi na fursa zinazoweza kuwasaidia katika maisha yao ya kitaaluma na kiuchumi.

Amesema wanafunzi 10 wamepata nafasi ya kufanya mafunzo ya vitendo NHIF, hatua itakayowasaidia kuongeza ujuzi na uzoefu katika mazingira ya kazi.

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa IFM, Adrian Kachocho, amesema amebuni mfumo unaowasaidia wafanyabiashara kufuatilia mapato na matumizi ya biashara zao, hatua inayoweza kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi na kuboresha usimamizi wa biashara.

















Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeeleza kuwa maandalizi ya kuchimba kisima cha utafutaji wa mafuta katika Kitalu cha Tanga yanaendelea, huku uchimbaji huo ukitarajiwa kufanyika mwaka 2027 baada ya kubainika kwa maeneo matatu yenye viashiria vya uwepo wa mafuta.

Maeneo hayo yaliyotambuliwa kama Prospect 1, Prospect 3 na Prospect 5 yamebainika kupitia tafsiri mpya ya takwimu za mitetemo za pande tatu (3D seismic data) zilizokusanywa katika Kitalu cha Tanga.

Akizungumza jana wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya PURA kwa mwaka wa fedha 2025/26 katika kikao na wahariri na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni, alisema maandalizi ya uchimbaji wa kisima cha utafutaji yanaendelea.

Katika utekelezaji wa shughuli za utafiti, PURA pia iliendelea kusimamia tafiti za awali za mafuta na gesi asilia katika maeneo ya Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara.

Katika eneo la Eyasi-Wembere, ukusanyaji wa takwimu za mitetemo za pande mbili (2D seismic data) ulikuwa umefikia kilomita 772 kati ya kilomita 779 zilizopangwa hadi Juni 30, 2026, sawa na asilimia 99.

Kwa upande wa Lindi-Mtwara, ukusanyaji wa takwimu za mitetemo za pande tatu ulikuwa umefikia kilomita za mraba 257.96 kati ya kilomita za mraba 736.3, sawa na asilimia 35.

Aidha, katika Kitalu cha Ruvuma, PURA iliendelea kusimamia shughuli za uendelezaji wa gesi asilia, zikiwemo maandalizi ya uchimbaji wa kisima cha Chikumbi-1 (CH-1), ukarabati wa kisima cha Ntorya-1 (NT-1) na majaribio ya uzalishaji wa kisima cha Ntorya-2 (NT-2).

Katika Kitalu cha Mnazi Bay, PURA ilisimamia uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia katika mwaka wa fedha 2025/26, ambapo viwili vilikamilika na kuanza uzalishaji.

Visima hivyo ni Mnazi Bay Five (MB-5) chenye uwezo wa kuzalisha wastani wa futi za ujazo milioni 40 za gesi kwa siku na Msimbati Two (MS-2) chenye uwezo wa kuzalisha wastani wa futi za ujazo milioni 50 kwa siku.

Kisima cha tatu, Kasa-1X, kilikuwa cha utafutaji wa gesi asilia, ambapo kupitia uchimbaji wake kiasi cha futi za ujazo bilioni 223 za gesi asilia kiligundulika.

Katika kuimarisha usimamizi wa mapato ya Serikali, PURA kupitia ukaguzi wa gharama na mapato katika mikataba ya Uzalishaji na Ugawanaji Mapato (PSA) iliwezesha kuokolewa na kurejeshwa kwa Dola za Marekani 3,306,678, sawa na Sh8,861,897,040, katika fungu la ugawanaji wa mapato kutoka kwa waendeshaji wa vitalu husika.

Ukaguzi huo ulihusisha Kitalu cha Songo Songo kwa miaka ya 2023 na 2024, Vitalu Na. 1 na 4 kwa miaka ya 2023 na 2024 pamoja na Kitalu cha Ruvuma kwa mwaka 2024. Aidha, ukaguzi ulianza katika Kitalu cha Songo Songo kwa mwaka 2025 na Kitalu Na. 2 kwa mwaka 2023.

Katika hatua nyingine, PURA imekamilisha uandaaji wa mfumo wa kuhifadhi kumbukumbu za hesabu za gharama na mapato ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini, unaojulikana kama PURA Cost Recovery Management System (CRMS), ambao umerahisisha uwasilishaji na uhifadhi wa taarifa za mapato na gharama kutoka kwa kampuni zinazojihusisha na shughuli za mkondo wa juu wa petroli nchini.

Katika kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli, thamani ya bidhaa na huduma zilizotolewa na kampuni za ndani ilikuwa zaidi ya Dola za Marekani milioni 30 mwaka 2026, ikilinganishwa na Dola milioni 14 mwaka 2025.

PURA imesema itaendelea kuimarisha utendaji na usimamizi wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli ili kuhakikisha sekta ya nishati inaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, huku ikiimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali, ikiwemo sekta binafsi, kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa gesi asilia kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.




Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imewezesha kuokolewa na kurejeshwa kwa Dola za Marekani milioni 3.3, sawa na Sh bilioni 8.86, katika fungu la ugawanaji wa mapato kupitia ukaguzi wa gharama na mapato ya kampuni zinazojihusisha na shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Akizungumza jana wakati akiwasilisha taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya PURA kwa mwaka wa fedha 2025/26, katika kikao na wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Charles Sangweni, alisema jumla ya Dola za Marekani 3,306,678, sawa na Sh8,861,897,040, ziliokolewa kupitia ukaguzi huo.

Alisema PURA ilikamilisha ukaguzi wa gharama na mapato katika Kitalu cha Songo Songo kwa miaka ya 2023 na 2024, Vitalu Na. 1 na 4 kwa miaka ya 2023 na 2024, pamoja na Kitalu cha Ruvuma kwa mwaka 2024.

Aidha, alisema mamlaka hiyo ilianza ukaguzi katika Kitalu cha Songo Songo kwa mwaka 2025 na Kitalu Na. 2 kwa mwaka 2023.

Katika kuimarisha usimamizi wa taarifa za kifedha, Sangweni alisema PURA imekamilisha uandaaji wa mfumo wa kuhifadhi kumbukumbu za hesabu za gharama na mapato ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini, unaojulikana kama PURA Cost Recovery Management System (CRMS).

Alisema mfumo huo umerahisisha uwasilishaji na uhifadhi wa taarifa za mapato na gharama kutoka kwa kampuni zinazojihusisha na shughuli za mkondo wa juu wa petroli nchini.

Katika hatua nyingine, alisema thamani ya bidhaa na huduma zilizotolewa na kampuni za ndani katika miradi ya mkondo wa juu wa petroli mwaka 2026 ilikuwa zaidi ya Dola za Marekani milioni 30, ikilinganishwa na Dola milioni 14 mwaka 2025.

Aidha, PURA iliendelea kusimamia na kuhakikisha kampuni zinazofanya shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini zinatekeleza programu na miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR), ikiwemo ujenzi wa Shule ya Msingi Likong’o katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, ujenzi wa majiko ya kisasa ya kupikia kwa kutumia nishati ya LPG katika shule nne zilizopo Kata ya Msimbati, Mtwara, na ufadhili wa vijana kusoma masuala ya ufundi katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mkoani Lindi.
Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) inatarajia kuwakutanisha Wahasibu, Wakaguzi na wadau mbalimbali wa Taaluma ya Uhasibu katika Mkutano Mkuu wa 39 wa Wahasibu 2026 utakaofanyika Novemba 24 hadi 27, 2026, jijini Dar es Salaam, kujadili mchango wa Taaluma ya Uhasibu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Sylvia Temu amesema mkutano huo utajumuisha shughuli za kijamii na kitaaluma, ambapo Novemba 24, Bodi hiyo itakabidhi vifaa tiba kwa Hospitali ya Mwananyamala na Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Watoto ya CCBRT jijini Dar es Salaam.

Amesema vifaa hivyo vimenunuliwa kupitia michango ya wahasibu mbalimbali waliojitokeza kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya nchini, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mchango wa wataalamu hao katika kusaidia jamii.

Amesema mkutano rasmi utaanza Novemba 25 na kufunguliwa na Waziri wa Fedha, Balozi Hamisi Mussa Omar, huku mada kuu ikijikita katika mchango wa Wahasibu na Wakaguzi wa hesabu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Ameeleza kuwa dira hiyo inalenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja za Marekani ifikapo mwaka 2050, huku pato la mtu mmoja mmoja likitarajiwa kufikia angalau dola 7,000. Pia inalenga kuimarisha elimu na uelewa wa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kuongeza uwezo wa wananchi kutumia na kuendeleza teknolojia katika shughuli za maendeleo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, siku ya pili ya mkutano, Novemba 26, itajadili masuala mbalimbali ya kitaaluma pamoja na afya ya mwili na akili, uwiano kati ya kazi na maisha binafsi na umuhimu wa wataalamu kutenga muda kwa ajili ya familia zao. Washiriki pia watapata fursa ya kushiriki michezo mbalimbali na kupata elimu ya afya kutoka kwa wataalamu.

Pia jioni ya tarehe 26 Novemba kutakuwa na hafla ya utoaji Tuzo kwa Taasisi za Umma, kampuni binafsi na Taasisi zisizo za kiserikali zilizofanya vizuri katika kuandaa taarifa bora za hesabu. Hafla hiyo itafanyika katika ukumbi wa mkutano wa APC Bunju jijini Dar es Salaam.

Amesema mchakato wa kupata washindi wa Tuzo hizo una ushindani mkubwa na unazingatia usiri, huku tathmini ikifanywa na wataalamu huru wenye ujuzi na uzoefu katika Taaluma ya Uhasibu na uandaaji wa taarifa za hesabu.

Ameongeza kuwa majina ya washindi yataendelea kuwa siri hadi wakati wa kutangazwa, akizihimiza Taasisi zote zilizoshiriki kuhudhuria hafla hiyo ili kushuhudia kutangazwa kwa washindi.

Mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa la kujadili mustakabali wa Taaluma ya Uhasibu nchini, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mchango wa Wahasibu na Wakaguzi wa hesabu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NBAA CPA Prof. Sylvia Temu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano mkuu wa 39 wa  mwaka wa Wahasibu 2026 utakaofanyika katika ukumbi wa mkutano wa APC Bunju jijini Dar es Salaam.



BURUDANI ya kasino inazidi kupamba moto ndani ya Meridianbet kupitia mchezo mpya wa Totally Headless II kutoka kwa kampuni maarufu ya utengenezaji wa michezo ya kasino, Games Global.

Mchezo huu umewasili kwa namna ya kipekee, ukiwaletea wapenzi wa kasino fursa ya kuingia katika ulimwengu wa maajabu, burudani na msisimko unaovutia. Bila kusahau kujisajili ili ufurahie msisismko huu leo ndani ya meridianbet.

Kupitia Totally Headless II, wachezaji wanakaribishwa kufurahia mazingira ya kipekee yaliyojaa matukio ya kusisimua, huku kila mzunguko ukiendelea kuongeza ladha ya burudani. Ni mchezo unaokualika kuchunguza ulimwengu wake wa kuvutia na kufurahia kila hatua ya safari yako ya kasino.

Kinachoufanya mchezo huu kuwa sehemu ya burudani inayostahili kuifahamu ni mchanganyiko wa ubunifu wa Games Global na msisimko unaotokana na kucheza. Kila unapozungusha, unapata nafasi ya kufurahia uzoefu tofauti huku ukiwa na matarajio ya matokeo yatakayokuletea furaha.

Sasa unaweza kuufurahia mchezo huu kupitia jukwaa la Meridianbet, ambalo linaendelea kukuletea michezo mbalimbali ya kasino kutoka kwa watengenezaji wanaotambulika. Totally Headless II ni fursa nyingine ya kuongeza ladha ya burudani yako kwa kuingia katika ulimwengu wake wa kipekee.

Vilevile, meridianbet wana michezo mingi ya kasino mtandaoni na mechi za kimataifa za kubashiri zenye ushindani mkubwa wa odds. Jiunge leo kwa kutembelea tovuti ya meridianbet au piga *149*10# kisha uanze safari yako ya ushindi.

Usibaki nyuma wakati burudani hii mpya imewasili! Tembelea Meridianbet, fungua mchezo wa Totally Headless II na ugundue msisimko unaokusubiri. Totally Headless II Zungusha, furahia msisimko na uwe sehemu ya burudani mpya ndani ya Meridianbet!


WIKENDI hii usikubali ikupite hivi hivi bila kufurahia burudani kwenye mechi za leo. Msako wa pointi 3 kama kawadia unaendelea huku baadhi ya wachezaji wakiendelea kupambania kupachika mabao.

Ligi kuu ya Uingereza EPL itapigwa mechi moja kali kati ya Brentford dhidi ya Everton, ukitarajiw akuwa mchezo wa kukata na shoka kutokana na aina ya uchezaji ambao hutumia timu zote mbili. Mechi itapigwa pale Gtech Community kila timu ikitaka ushindi siku ya leo.

Brentford wametoka kupoteza mechi yao liyopita, hivyo hii ni mechi ambayo wanaitazama kwa jicho lingine, wakati The Toffees wao wametoka kushinda mechi yao iliyopita kwa kishindo huku tofauti ya pointi kati yao ni 2 pekee. Je nani kushinda leo?

Kivumbi kingine kitakuwa kule LALIGA ambapo Elche atakuwa ugenini kupepetana dhidi ya Levante ambao mpaka sasa wapo nafasi ya 18 huku wenyeji wao wakiwa nafasi ya 17, na tofauti yao ikiwa ni pointi 1 pekee hadi sasa.

Yaani zinakutana timu mbili ambazo pointi 3 ni muhimu sana kwa kila mtu kutokana na nafasi walizpo kwenye msimamo wa ligi. Levante wanaingia kwenye mchezo huu wakitoka kupata sare tasa ya 0-0 dhidi ya Celta Vigo.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa wanaweza kucheza kwa nidhamu katika safu ya ulinzi, lakini wanahitaji kuongeza makali kwenye eneo la ushambuliaji ili kutumia vizuri nafasi wanazopata.

Elche wanakwenda kwenye mchezo huu wakitafuta kurejea kwenye ushindi baada ya kupoteza mabao 2-0 dhidi ya Real Betis. Wanahitaji kuboresha uimara wa safu yao ya ulinzi na kutumia vizuri nafasi za kushambulia.

Takwimu zinaonesha kuwa msimu uliopita kwenye mechi mbili walizokutana kwenye ligi, kila mtu alishinda nyumbani kwake. Je historia inaweza ikajirudia?.

Bila kusahau kuwa mechi hii unazipata kule Meridianbet ambapo pia unaweza ukapata taarifa za wachezaji ambao wanaweza kucheza na ambao ni majeruhi.

SERIE A kule Italia kuendelea pia ambapo AC Monza atamenyana dhidi ya Fiorentina ambapo mchezo huu unatarajiw akuwa na ushindani mkubwa sana kutokana na hali za timu zote mbili, yaani wote wapo chini kwenye msimamo wa ligi.

Wenyeji wanaingia kwenye mchezo huu nia yao ikiwa ni ushindi kwani mpaka sasa kwenye mechi 5 za mwisho wamepoteza 4 huku shida ikiwa ni safu yao ya ulinzi wakishinda kutumia nafasi pia.

Wageni wao Fiorentina wao hawana ule mwendelezo mzuri wa matokeo chanya kwani wanawez akushinda, kutoa sare na kufungwa lakini baadhi ya mechi wamefanya vyema kutokana na kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa akiwemo Mastantuono, Pellegrino na wengine wengi. Je nani kushinda leo?


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,  akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha African International Convention Centre (AICC), Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026) pamoja na kuzindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika, tarehe 23 Novemba, 2026.




 Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema mkoa huo umepokea jumla ya Shilingi trilioni 1.65 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa fedha hizo ili kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta Tija. 

Nyongo aliyasema hayo wakati akielezea maendeleo ya mkoa huo kwa mwaka huu wa fedha na masuala ya mapato. 

Aidha alisema pamoja na fedha hizo za miradi ya maendeleo, Mkoa wa Pwani umejiwekea lengo la kukusanya Shilingi bilioni 112 katika mwaka wa fedha 2026/2027, ambapo hadi kufikia Oktoba mwaka huu ulikuwa umekusanya zaidi ya Shilingi bilioni 47.

Alisisitiza kuwa miradi ya maendeleo inapaswa kutekelezwa kulingana na fedha zilizotolewa, huku wakandarasi wakitakiwa kukamilisha kazi kwa wakati kwa kuzingatia masharti ya mikataba yao, ili wananchi waanze kupata huduma zilizokusudiwa bila ucheleweshaji usio wa lazima.

Kuhusu uwekezaji anasema Mkoa wa Pwani unaendelea kupokea wawekezaji kutokana na juhudi za kuboresha mazingira ya uwekezaji, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. 

Alifafanua kuwa mkoa huo una jumla ya viwanda 1,768, vikiwemo viwanda vikubwa 503, vya kati 248 na vidogo 1,017, pamoja na kongani 35 za viwanda, ikiwemo HWTZ SEZ.

Kuhusu upatikanaji wa nishati ya umeme, alieleza vijiji 409 vya mkoa huo vimefikiwa na huduma hiyo, huku usambazaji wa umeme katika vitongoji ukiendelea, ambapo mkoa unatarajia kufikia asilimia 95 ya vitongoji vilivyounganishwa na umeme ifikapo Desemba 2026.

Kuhusu changamoto za ardhi, Nyongo alibainisha kwamba mkoa unaendelea na mpango wa kuendesha kliniki za ardhi katika kila wilaya , kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi kwa kuzingatia haki na sheria.

Fursa zilizopo katika sekta za kilimo, viwanda, madini, utalii, nishati na maji zinaendelea kuwa chachu mkoani hapo katika kukuza uchumi wa mkoa na kuongeza mapato, huku Nyongo akisisitiza usimamizi mzuri wa rasilimali na fedha za umma ni muhimu katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora, inakamilika kwa wakati na kutoa huduma zinazotarajiwa kwa wananchi.



Mtumishi wa Mungu Yona Simon Katwiga ameandaa kitabu kinachoitwa nchi ya Tanzania kinachoeleza alama 13 zilizopo Tanzania ambazo kwa tafsiri yake ya kiimani zina uhusiano na maandiko ya Biblia na makusudi ya Mungu kwa taifa, kikitarajiwa kuzinduliwa mwaka 2027.

Katwiga, ambaye ni muumini wa Kanisa la Tanzania Mission Revival Church (TMRC) jijini Dodoma, amesema ameandika kitabu hicho akiamini kuwa ameongozwa na Mungu kuwasilisha ujumbe kuhusu nafasi ya Tanzania katika kutimiza makusudi yake, akieleza kuwa baadhi ya alama zilizopo nchini zina maana inayozidi tafsiri zake za kawaida za kijiografia na kihistoria.

Miongoni mwa alama 13 alizozitaja ni Mlima Kilimanjaro, lugha ya Kiswahili, Mto Nile, Jiwe la Bismarck lililopo Mwanza, mti wa Mkusu, Ziwa Ngosi, jiwe lenye umbo la ramani ya Afrika, mchanga unaotembea wa Ngorongoro, madini ya Tanzanite, kimondo cha Mbozi, Hifadhi ya Kitulo, Ziwa Victoria na Hifadhi ya Ngorongoro.

Akifafanua kuhusu Mlima Kilimanjaro, Katwiga amesema mlima huo una umuhimu wa kipekee katika tafsiri yake ya kiimani, akihusisha vilele vyake vitatu vya Kibo, Mawenzi na Shira pamoja na njia saba za kuupanda na matumizi ya namba hizo katika Biblia, ameutaja mlima huo kuwa madhabahu ya Mungu na ishara ya utukufu wake nchini Tanzania.

Amesema namba tatu na saba zina nafasi maalumu katika maandiko ya Biblia, akitoa mifano ya kinara cha taa chenye matawi saba, kuta za Yeriko kuzungukwa mara saba na maelekezo ya nabii Elisha kwa Naamani kujitosa katika Mto Yordani mara saba ili apate uponyaji.

Katika maelezo yake, Katwiga pia amehusisha kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru na simulizi ya Mtumishi wa Mungu Musa katika kitabu cha Kutoka 3:1-22, akisema tukio hilo linafanana na kijiti kilichowaka moto bila kuteketea ambacho Mungu alimtokea Musa katika Mlima Sinai, Kwa mtazamo wake, kufanana kwa matukio hayo pamoja na uwepo wa milima kunabeba ujumbe wa kiimani kuhusu Tanzania.

Ameongeza kuwa milima ina nafasi muhimu katika simulizi za Biblia, akirejea kisa cha Ibrahimu kupewa maelekezo ya kumtoa mwanawe Isaka mlimani kama sadaka, kinachoelezwa katika Mwanzo 22:1-3, pamoja na Musa kukutana na Mungu mlimani kama ilivyoandikwa katika Kutoka 19:9-12. Kwa tafsiri yake, matukio hayo yanaonesha umuhimu wa milima kama maeneo ya kukutana na Mungu na kuweka maagano.

Katwiga amesema Mwenge wa Uhuru una ujumbe unaozidi tafsiri za kawaida za kihistoria, akidai kuwa kwake ni ishara ya agano kati ya Mungu na Watanzania, pamoja na nuru inayopaswa kuenezwa duniani, amehusisha pia alama hiyo na kile anachokiita nafasi ya Tanzania katika kutimiza kusudi la Mungu kwa mataifa.

Aidha, ametoa wito kwa Watanzania kudumisha umoja, amani, haki na mshikamano, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuwapenda na kuwaombea viongozi wao, akimtaja Rais wa nchi kuwa miongoni mwa viongozi wanaopaswa kuungwa mkono na kulindwa.

Amesema kitabu hicho kinalenga kuwasaidia Watanzania kutambua na kutafakari kile anachokieleza kuwa kusudi la Mungu kwa taifa lao, huku akiwahimiza wananchi kufuatilia maelezo zaidi kupitia chaneli yake ya YouTube ya Amani kwa Wote



Na. Peter Haule, WF, Dar es Salaam


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ametoa wito kwa Watanzania kushirikiana katika kurejesha na kuimarisha maadili mema katika jamii, akisisitiza kuwa jukumu la kujenga jamii yenye maadili si la Serikali pekee, bali linawahusu wazazi, walezi, walimu, viongozi wa dini na kila mwanajamii.

Mhe. Omar ameyasema hayo wakati wa hafla ya ugawaji wa zawadi kwa washiriki na washindi wa mashindano ya Sira ya Mtume Muhammad (SAW) yaliyoandaliwa kupitia Kampeni ya Rudisha Maadili kwa Jamii na Uzinduzi wa Huduma ya Daktari wangu kupitia Mfuko wa Bima ya Mufti, iliyofanyika katika Msikiti wa BAKWATA, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Amesema suala la maadili ni jambo la msingi katika maendeleo ya jamii na linapaswa kuanzia katika familia, kuendelezwa shuleni, katika nyumba za ibada na maeneo mbalimbali ya kijamii.

“Hapo awali malezi ya watoto yalikuwa jukumu la pamoja la wazazi na jamii nzima, huku walimu na viongozi wa dini wakichangia katika kuwajenga watoto katika misingi ya heshima, nidhamu na uwajibikaji, kwa sasa kuna changamoto katika mfumo wa malezi, hali inayohitaji jamii kutafakari upya wajibu wake na kuchukua hatua za pamoja kurejesha utamaduni wa kulea watoto katika misingi ya maadili mema”, amesema Mhe. Balozi Omar.

Aidha, ametoa pongezi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kusisitiza umuhimu wa maadili katika jamii.

Akizungumzia mashindano ya Sira ya Mtume Muhammad (SAW), Mhe. Omar amesema mashindano hayo yamekuwa sehemu ya kutoa elimu kwa washiriki kuhusu maisha na mafundisho ya Mtume, huku akisisitiza kuwa lengo la elimu hiyo halipaswi kuishia katika kushiriki mashindano au kupata zawadi.

Amesema washindi waliopata zawadi wanastahili pongezi, lakini kwa maana pana, kila aliyeshiriki na kupata elimu kupitia mashindano hayo ni mshindi, kwa sababu mafanikio makubwa yatakuwa pale elimu hiyo itakapotumika katika maisha halisi.

Vilevile Mhe. Balozi Omar ametoa shukrani kwa waandaaji wa kampeni hiyo, washiriki na wadau wote waliofanikisha mashindano hayo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika kurejesha na kudumisha maadili mema kwa maendeleo ya jamii ya Watanzania.

Kwa upande wake Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za dini na jamii katika kuimarisha maadili na kuchochea maendeleo ya Watanzania.

Amesema ujenzi wa jamii yenye maadili mema unahitaji kila upande kutekeleza wajibu wake kwa kushirikiana, huku akibainisha kuwa maendeleo ya nchi yanapaswa kuzingatia maeneo muhimu ya elimu, uchumi, afya na ustawi wa jamii.

Sheikh Dkt. Zubeir ameeleza kuwa Serikali na wadau wengine wanapaswa kuendelea kuweka mazingira yatakayowezesha wananchi kupata elimu na huduma muhimu, pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Naye Meneja Mahusiano wa Taasisi ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Bi. Khadija Maulid, akizungumzia suala la Bima kwa wote, ametoa wito kwa Watanzania kushirikiana na kuunga mkono Mfuko wa Bima ya Mufti katika kuhamasisha upatikanaji wa huduma za bima ya afya, hususan kwa wananchi wenye uhitaji.

Amesema ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha Watanzania wanapata fursa ya kupata huduma za matibabu bila kukabiliwa na changamoto kubwa za kifedha pale wanapougua.

Awali Mtoto Rehema Suleiman Kizenza aliyeibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya Sira ya Mtume Muhammad (S.A.W), baada ya kuonesha umahiri na uelewa mkubwa kuhusu maisha, mwenendo na mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W), alisema somo la Sira ya Mtume lina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila siku, hususan kwa watoto na wanafunzi, kwa kuwa linawafundisha maadili mema.

Alisema kujifunza Sira ya Mtume kunamsaidia yeye na wanafunzi wenzake kuwa waaminifu, wakweli, wenye huruma, wanyenyekevu na wenye kuzingatia adabu katika maisha yao ya kila siku.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiagana na  Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir baada ya hafla ya ugawaji wa zawadi kwa washiriki na washindi wa mashindano ya Sira ya Mtume Muhammad (SAW) na Uzinduzi wa Huduma ya Daktari wangu kupitia Mfuko wa Bima ya Mufti,  iliyofanyika katika Msikiti wa BAKWATA, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akitoa zawadi kwa Ikram Khalfan Kanuti ambaye ni miongoni mwa washindi wa mashindano ya Sira ya Mtume Muhammad (SAW) iliyofanyika katika Msikiti wa BAKWATA, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akitoa wito wa kurejesha maadili mema wakati wa hafla ya ya ugawaji wa zawadi kwa washiriki na washindi wa mashindano ya Sira ya Mtume Muhammad (SAW) na Uzinduzi wa Huduma ya Daktari wangu kupitia Mfuko wa Bima ya Mufti,  iliyofanyika katika Msikiti wa BAKWATA, Kinondoni, jijini Dar es Salaama.

Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za dini na jamii katika kuimarisha maadili na kuchochea maendeleo ya Watanzania.


Baadhi ya washiriki wa hafla ya ugawaji wa zawadi kwa washindi wa mashindano ya Sira ya Mtume Muhammad (SAW) na Uzinduzi wa Huduma ya Daktari wangu kupitia Mfuko wa Bima ya Mufti,  wakifuatilia mambo mbalimbali, katika Msikiti wa BAKWATA, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Dar es Salaam)