Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo, ameipongeza mamlaka hiyo kwa kuandaa Mpango Mkakati wa Shirika (CSP) wa miaka mitano na Mpango wa Muda Mrefu (LTTP) wa miaka 25 unaozingatia uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.

Mabeyo ametoa pongezi hizo jijini Arusha wakati wa kikao cha Bodi ya Wakurugenzi kinachojadili utekelezaji wa shughuli za mamlaka hiyo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kuanzia Julai hadi Septemba.

Amesisitiza kuwa uhifadhi wa ikolojia ya Hifadhi ya Ngorongoro na Pori la Akiba la Pololeti unapaswa kupewa kipaumbele na kulindwa kwa nguvu zote kutokana na mchango wake katika kuimarisha uhifadhi, kulinda ajira za Watanzania na kuongeza mapato ya Serikali kupitia utalii.

Ameeleza kuwa mapato yanayotokana na utalii huchangia kuboresha huduma za jamii na kuchochea maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Abdul-Razaq Badru, amesema mipango hiyo imezingatia nyaraka na miongozo mbalimbali ya Serikali, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025–2050 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2025–2030.










Afisa  Mtendaji Mkuu wa Self Microfinance  Fund Santiel Yona akizungumza na wahariri kuhusiana na mafanikio na Mikakati ya Taasisi hiyo huduma za  Mikopo ya Kifedha  Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia  Positive Cooker Atukuzwe Nkya akuzungumza kuhusiana na wanavyoshirikiana na Self Microfinance Fund kutoa kutoa mikopo ya nishati Safi ya Kupikia.
Afisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) Alex Malanga akizungumza kuhusiana na Ofisi hiyo ilivyojipanga katika Taasisi zilizochini ya Msajili kutoa taarifa za maandeleo
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa TEF ,Bakari Kimwanga akizungumza kuhusiana na umuhimu wa taarifa kwa wananchi kuhusiana na huduma za kifedha za Mikopo zinazotolewa na Self Microfinance Fund ,jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya matukio katika picha Katika mkutano uliohusisha wahariri na Self Microfinance Fund

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MFUKO wa Self Microfinance Fund umeeleza kuwa umejipanga kupanua wigo wa huduma za mikopo nafuu kwa wananchi, hususan wakulima, wafugaji na wajasiriamali, ili kuwawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Hatua hiyo inalenga kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa mfuko huo, ikiwamo kuwapa wananchi fursa ya kupata huduma za kifedha na kuondoa dhana kwamba Watanzania hawakopesheki kutokana na changamoto za urejeshaji wa mikopo katika taasisi za kifedha.

Hayo yameelezwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa mfuko huo, Santiel Yona, wakati wa kikao kazi kati ya taasisi hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina na wahariri wa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam, kilicholenga kueleza mafanikio yaliyopatikana.

Yona alisema katika mwaka wa fedha 2024/2025, mfuko huo umechangia upatikanaji wa ajira 262,624, huku ukiendelea kutoa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wajasiriamali.

Alisema mfuko huo una uwezo wa kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 54, hivyo kuwataka Watanzania kutumia fursa hiyo kuendeleza shughuli zao za uzalishaji na biashara.

Akizungumzia urejeshaji wa mikopo, Yona alisema kiwango cha urejeshaji kimefikia asilimia 95, hali inayoonesha mwenendo mzuri katika usimamizi wa mikopo inayotolewa na taasisi hiyo.

Alisema mfuko umeweka mikakati ya kuendelea kuimarisha urejeshaji wa mikopo kwa kufanya tathmini ya uwezo wa wakopaji, kuchunguza sababu zinazowafanya baadhi yao kushindwa kulipa kwa wakati na kuweka utaratibu wa kuwasaidia kurejesha mikopo yao.

Alifafanua kuwa hatua hizo ni pamoja na kuingia mikataba mipya pale inapohitajika na kuwaongezea wakopaji muda wa kurejesha mikopo kulingana na taratibu zilizowekwa.

“Aliyekopa ni lazima arejeshe fedha alizokopa. Tunaweza kumuongezea muda wa kulipa hadi miaka miwili, kuingia naye mkataba mpya na kujua sababu zilizomfanya ashindwe kurejesha mkopo wake kwa wakati,” alisema Yona.

Kwa upande wake, Manongi alisema katika kipindi cha miaka mitatu, Self Microfinance Fund imefanikiwa kufungua matawi 12 yanayotoa huduma katika kanda mbalimbali nchini, hatua inayolenga kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi.

Alisema mafanikio mengine ni pamoja na kutoa gawio la Sh milioni 490.9 na kupata faida ya Sh bilioni 3.19 baada ya kodi.

Aidha, alisema mfuko huo unashiriki katika juhudi za kukuza matumizi ya nishati safi kupitia mradi wa mikopo ya majiko yanayotumia umeme kwa ufanisi, kwa kushirikiana na kampuni ya Positive Cooker.

Aliongeza kuwa mfuko huo pia unatoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa bajaji na pikipiki, zinazoweza kutumiwa na wajasiriamali wadogo katika kuendesha na kupanua shughuli zao za kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Afisa Mtendaji Mkuu alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake katika kuwezesha mafanikio ya Self Microfinance Fund.
Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Latifa Mohammed Khamis akizungumza jambo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Richard Muyungi wakati wa ufunguzi wa kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo Oktoba 27, 2026 Jijini Dar es Salaam kujadili maandalizi ya Tanzania kuelekea Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama Wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 31).
Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa akizungumza jambo wakati wa wa ufunguzi wa kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo Oktoba 28, 2026 Jijini Dar es Salaam kujadili maandalizi ya Tanzania kuelekea Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama Wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 31).
Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na maendeleo endelevu (IUCN), Bw. Ghaamid Abdulbasat akizungumza wakati wa kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo Oktoba 28 2026 Jijini Dar es Salaam kujadili maandalizi ya Tanzania kuelekea Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama Wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP) 31.

TANZANIA imeainisha vipaumbele vya kitaifa vitakavyoongoza majadiliano ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 31) unaotarajia kufanyika tarehe 9-20 Novemba mwaka huu nchini Uturuki.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Latifa Mohammed Khamis wakati akifungua kikao cha Makatibu Wakuu kuhusu maandalizi ya Tanzania kuelekea Mkutano wa (COP 31).

Dkt. Latifa amesema wakati wa majadiliano ya mkutano huo, Tanzania inatarajia kuwasilisha vipaumbele vinavyohusiana na fedha za tabianchi, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na upunguzaji wa uzalishaji wa gesi chafuzi.

Ametaja vipaumbele vingine kuwa ni utekelezaji wa Makubaliano ya Paris, uhamishaji wa teknolojia, kujenga uwezo, masoko ya kaboni chini ya Ibara ya 6, pamoja na hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi.

“Ni muhimu kuhakikisha kuwa msimamo wetu unaakisi vipaumbele vya Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na mahitaji ya sekta za kilimo, maji, nishati, afya, miundombinu, misitu, mifumo ya ikolojia, bahari na uchumi wa buluu” amesema Dkt. Latifa.

Ameeleza kuwa vipaumbe hivyo vitatoa fursa kwa Tanzania kuendeleza ajenda za nishati safi, usalama wa chakula, uchumi wa buluu, uhifadhi wa mazingira, viwanda vya kijani na ushiriki wa vijana.

Ameeleza kuwa kuelekea mkutano huo ni muhimu kwa wataalamu kukamilisha mpango kazi ikihusisha maandalizi ya mikutano ya pembezoni, mikutano ya uwili na shughuli zitakazofanyika katika jengo la maonesho la Tanzania.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa amesema maelekezo yaliyotolewa katika kikao hicho yatawekewa mpango wa utekelezaji wenye majukumu yaliyo wazi, muda maalumu na utaratibu wa ufuatiliaji.

“Ni muhimu kwa Makatibu Wakuu kupitia matokeo ya majadiliano haya, kutoa maelekezo ya Serikali na kukubaliana kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kukamilisha maandalizi ya kitaifa kwa wakati” amesema Kemilembe.

Aidha amewataka washiriki wa mkutano huo ikiwemo Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wengine kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao kwa wakati ili kufanikisha malengo ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu (IUCN), Bw. Ghaamid Abdulbasat amesema Shirika hilo limeendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais katika utekelezaji wa ahadi za mikataba ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi.

Akitolea mfano amesema Shirika hilo kwa linashirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza Programu ya Urejeshaji ya kidunia (TRI) inayolenga kurejesha uoto wa asili katika ardhi iliyoharibika takribani hekta milioni 5.2 ifikapo mwaka 2030 katika mabonde ya Ruaha Mkuu na Ziwa Rukwa, katika mikoa ya Iringa, Mbeya na Rukwa.





Na Mwandishi Wetu Michuzi Tv 

SGA Cash in Transit Tanzania imetajwa kuwa Kampuni Bora ya Huduma za Courier na Uwasilishaji wa Mwaka katika Tuzo za Supply Chain, Mobility & Logistics (SML) 2026. 

Tuzo hiyo inatambua ubora, uaminifu na kiwango cha huduma katika sekta ya courier, na inaonyesha dhamira ya SGA ya kusafirisha fedha na vitu vya thamani kwa usalama, ulinzi na kwa wakati kwa wateja kote nchini Tanzania. 


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Security Tanzania, CPA Jonathan Geleta, alisema ushindi huo ni uthibitisho na pia changamoto. “Utambuzi huu unaonyesha viwango ambavyo tumejenga biashara yetu juu yake, lakini pia unainua kiwango cha matarajio. Wateja wetu wanatarajia zaidi kutoka kwetu kila mwaka, na tutaendelea kuboresha huduma zetu na kuwekeza katika watu wetu, michakato na teknolojia ili kukidhi matarajio hayo nchini kote Tanzania,” alisema. 


Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Huduma za Courier, Stella Chiwango, alisema utambuzi huo unaonyesha kujitolea kwa timu zinazohusika na kuhakikisha huduma za courier zinazotegemewa. 


“Huduma za courier ni kutimiza ahadi: kumfikishia mtu sahihi mzigo sahihi kwa wakati sahihi. Tuzo hii inatambua nidhamu na kujitolea kwa wasafirishaji wetu na timu za usambazaji, na inatutia moyo kuendelea kuboresha huduma tunazowapa wateja wetu,” alisema. 


Mkuu wa Huduma za Cash in Transit,  Rashid Kawawa, alisema utambuzi huo unasisitiza umuhimu wa nidhamu ya kiutendaji na usalama katika kutoa huduma salama za usafirishaji. 

“Nyuma ya kila uwasilishaji salama kuna timu inayopanga kwa umakini, inayofuata taratibu zilizowekwa na isiyowahi kuhatarisha usalama. Najivunia watu wetu na ninawashukuru wateja wetu kwa imani wanayotuwekea,” alisema. 

Tuzo za SML ni jukwaa la hadhi ya juu katika sekta, linaloadhimisha utendaji bora, ubunifu na matokeo chanya katika sekta za ugavi (supply chain), usafiri (mobility) na usafirishaji (logistics). Toleo la mwaka huu liliwakutanisha kampuni za usafirishaji, waendeshaji wa minyororo ya ugavi, wabunifu katika sekta ya usafiri, mitandao ya usambazaji, taasisi za fedha, kampuni za bima na watoa huduma. 

Tuzo hii inaimarisha dhamira ya SGA ya kudumisha viwango vya juu vya usalama, uaminifu na utoaji wa huduma katika shughuli zake za courier na usafirishaji wa fedha (cash in transit). 

SGA Cash in Transit (T) Limited ni kampuni iliyosajiliwa mwaka 1995 kama Group Four Cash in Transit (T) Ltd, ikawa Security Group Cash in Transit (T) Ltd mwaka 2000, kisha ikabadilisha chapa na kuwa SGA Cash in Transit (T) Ltd mwaka 2016. Kwa miongo mitatu, imejijengea sifa katika usafirishaji na utunzaji salama wa fedha na vitu vya thamani kwa taasisi kuu za fedha, ikiungwa mkono na rasilimali na uzoefu iniwa mojawapo miongoni mwa makampuni ya SGA.



WANANCHI na wafanyabiashara wa Tunduma, mkoani Songwe, wameishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Songwe kwa kutoa elimu kuhusu athari za magendo na umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu za Forodha, wakisema imewaongezea uelewa kuhusu namna ya kuendesha biashara zao kwa mujibu wa sheria.
Shukrani hizo zimetolewa wiki hii wakati wa zoezi la utoaji wa elimu ya Forodha lililofanyika katika maeneo ya Kisimani, Kilimanjaro na Soko Kuu la Black, yaliyopo mpakani mwa Tanzania na Zambia.


Elimu hiyo imetolewa na Afisa Msimamizi wa Kodi Mwandamizi, Julieth Kidemi, na Afisa Uhusiano, Salome Mwandalanga, kutoka TRA Makao Makuu, Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Afisa Forodha wa TRA Mkoa wa Songwe, Abel Ikomeja.


Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Meneja Msaidizi wa Forodha Mkoa wa Songwe, Nsajigwa Mwambegele, amewataka wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kujiepusha na vitendo vya magendo na kuzingatia sheria na taratibu za Forodha.
Aidha, Mwambegele amewasihi madereva wa magari ya usafirishaji wa mizigo kutoshusha njiani mizigo inayopaswa kufikishwa katika nchi jirani, akisisitiza kuwa kuzingatia taratibu za usafirishaji ni muhimu katika kuzuia magendo na kuhakikisha biashara halali zinafanyika kwa mujibu wa sheria.






📍Bungeni- Dodoma

Serikali imesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa mikataba ya uhawilishaji teknolojia (Technology Transfer Agreements) katika miradi ya madini, hususan madini mkakati (Critical Minerals), ili kuimarisha ujuzi, utaalamu na uwezo wa kiteknolojia wa Watanzania katika sekta ya madini.

Akijibu swali la Mbunge wa Tarime Mjini, Mhe. Esther Matiko, kuhusu Sera ya kuimarisha mikataba hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, amesema Serikali imeweka misingi ya kisheria inayowataka wawekezaji katika sekta ya madini kushirikiana na wataalamu wazawa katika uhawilishaji wa maarifa na teknolojia.

Amesema Sera ya Madini ya mwaka 2009, hususan Ibara ya 5.12, inasisitiza umuhimu wa kuimarisha ujuzi na uwezo wa kitaalamu wa Watanzania kupitia mafunzo na ushirikiano na kampuni za madini.

Aidha, Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa Kifungu cha 135 cha Sheria ya Madini, Sura ya 123, kinawataka wamiliki wa leseni za madini kuweka utaratibu wa uhawilishaji wa maarifa na teknolojia, kujenga uwezo wa wataalamu wazawa na kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa wajibu huo.

Ameongeza kuwa Kanuni za Madini za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018, hususan Kanuni za 27 hadi 29, zinaweka matakwa kwa wawekezaji kuandaa mipango ya uhawilishaji teknolojia na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa Tume ya Madini.

Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mipango hiyo ili kuhakikisha uhawilishaji wa teknolojia unaleta matokeo halisi katika kujenga uwezo wa kitaalamu na kiteknolojia kwa Watanzania.

Amesema hatua hiyo ni muhimu zaidi katika miradi ya madini mkakati, ambayo ina nafasi kubwa katika kukuza viwanda, kuongeza thamani ya madini nchini na kuimarisha manufaa ya rasilimali hizo kwa uchumi wa Taifa.

Kupitia utekelezaji madhubuti wa mikataba hiyo, Serikali inalenga kuhakikisha kuwa uwekezaji katika sekta ya madini hauishii katika uzalishaji wa madini pekee, bali pia unaacha urithi wa maarifa, ujuzi na teknolojia utakaosaidia kukuza uwezo wa wazawa na kuchochea maendeleo endelevu ya sekta hiyo.


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na taasisi za uhifadhi wa mazingira, limeadhimisha kumbukizi ya miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kupanda miti ya kumbukumbu katika taasisi za umma, ikiwemo shule.

Zoezi hilo limefanyika jana, Oktoba 27, 2026, katika Nyumba ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Magomeni, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuenzi urithi na mchango wake katika ujenzi wa taifa na uhifadhi wa mazingira.

Akiongoza zoezi hilo, mtoto wa Baba wa Taifa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere, alisema taifa litaendelea kumkumbuka Mwalimu Nyerere kwa uzalendo wake, uadilifu na moyo wa kulitumikia taifa, sambamba na misingi ya mshikamano aliyoiacha ambayo imeendelea kuwa nguzo ya umoja na amani nchini.

Makongoro aliwataka vijana wa Kitanzania kuzingatia uzalendo na kutanguliza maslahi ya taifa, huku akiwahimiza kuenzi misingi ya Mwalimu Nyerere kwa kutunza mazingira, kulinda maeneo yaliyohifadhiwa na vyanzo vya maji, pamoja na kupanda miti katika makazi yao kwa ajili ya kupata vivuli na matunda.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Emmanuel Moirana, alisema shirika hilo litaendelea kuenzi mchango wa Hayati Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa mwanzilishi wa TANAPA.

Alisema maono ya Baba wa Taifa yameendelea kuwa dira ya uhifadhi endelevu nchini, huku matokeo yake yakionekana kupitia maendeleo ya sekta ya utalii na ongezeko la watalii wanaotembelea vivutio vya Tanzania.

Moirana aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere atakumbukwa pia kwa kusisitiza umuhimu wa amani, uzalendo, mshikamano na kuwaunganisha Watanzania bila kujali tofauti zao.

Alisisitiza kuwa rasilimali za taifa zinapaswa kusimamiwa kwa manufaa ya Watanzania wote, akihimiza wananchi kuendeleza misingi hiyo kwa kulinda mazingira na kuhifadhi urithi wa taifa kwa ajili ya vizazi vijavyo.








Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amemtembelea na kumfariji Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura, kufuatia kifo cha baba yake mzazi, marehemu Deusdedit Mwita Wambura.

Mzee Deusdedit Wambura alifariki dunia Oktoba 24, 2026, jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais ametoa salamu za pole kwa familia hiyo alipoitembelea katika makazi ya IGP Camillus Wambura, yaliyopo Masaki, jijini Dar es Salaam.









NA: DK. REUBENI LUMBAGALA

Serikali ina vipaumbele vingi vya maendeleo kwa ajili ya watu wake. Miongoni mwao ni uwezeshaji wananchi kiuchumi. Hapa serikali huweka mazingira rafiki na wezeshi kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanatumia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo ili kujiongezea kipato na kuchangia maendeleo ya nchi.

Katika juhudi za maendeleo, kundi la vijana ni muhimu kuwezeshwa ili nao washiriki kikamilifu katika maendeleo. Vijana wana nguvu na maarifa ya kuweza kuzalisha na hatimaye kubadili hali zao za maisha kutoka hali duni na kuwa nzuri zaidi. Ni kundi ambalo likiwezeshwa, maendeleo yatasonga mbele kwa haraka zaidi.

Kutokana na umuhimu wa kundi la vijana katika maendeleo, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameanzisha wizara maalum ya kushughulikia masuala ya vijana - Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana chini ya uongozi wa Waziri wake, Joel Nanauka.

Wizara hii hajachanganywa na sekta nyingine yeyote, imebaki kushughulikia masuala ya maendeleo ya vijana. Basi. Huu ni upekee wa aina yake kutokana na dhamira ya serikali ya kuhakikisha kundi la vijana linakamata fursa muhimu za uchumi kwa maendeleo.

Katika kuhakikisha uwezeshaji vijana kiuchumi haubaki kuwa mpango wa kwenye makaratasi tu, serikali ikaweka katika vitendo kwa kutoa shilingi bilioni 200 ili zikopeshwe kwa vijana bila riba. Fedha hizi zikawekewa utaratibu kwa vijana katika vikundi waungane na watume maombi na kwa wale watakaokidhi vigezo watakopeshwa.

Kikundi cha vijana cha Kitwima yaani Kitwima Youth Group (KYG) ni miongoni mwa wanufaika wa mkopo wa shilingi bilioni 200 zilizokopeshwa na vijana nchi nzima. Kikundi hiki ni cha vijana wasomi ambapo wamejikita katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, katika Ziwa Viktoria, mkoani Mwanza.

Ni kwamba, kikundi hiki kilipata mkopo wa shilingi milioni 106.9, mwezi Machi, 2026. Baada ya kupokea fedha hizo, walinunua vifaranga vya samaki 60,000 kwa shilingi milioni tisa, wakaongezwa vifaranga 6,000 na kufanya vifaranga vya samaki kufika 66,000.

Vilevile, walitengeneza keji kwa shilingi milioni 35, wakanunua mtumbwi, chakula cha samaki na majaketi ya kuwasaidia katika shughuli zao za uvuvi (life jackets). Ndani ya miezi saba ya shughuli hiyo (Machi - Oktoba, 2026) wameweza kuzalisha samaki tani 15 aina ya Sato ambao mauzo yake yana thamani ya shilingi milioni 127.5.

Kimsingi, kikundi hiki kimeonyesha uthubutu mkubwa na kimetoa darasa kwa vijana wenzao katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, kuchangamkia fursa za uchumi zinazoratibiwa na serikali. Kupitia mradi huu, vijana hao wamejihakikishia kipato kupitia mauzo ya samaki pindi wanapowavuna.

Pengine sana, kupitia mafanikio ya kikundi cha Kitwima, vijana waongeze ari ya kufuatilia mikopo inayotokewa na Wizara ya Vijana na Wizara nyingine ili vijana waweze kubadili maisha yao kwa kujiajiri wenyewe. Aidha, waliopewa dhamana ya kushughulikia mikopo ya vijana watende haki, waondoe urasimu ili vijana wanufaike na fursa hizo muhimu kwa maendeleo endelevu.

Maoni : 0620 800 462.


Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Mbeya, wametakiwa kutumia elimu na ujuzi walioupata chuoni kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kuzingatia utu, uadilifu na maadili ya Kitanzania, huku wakitumia ubunifu na uthubutu kutafuta suluhisho la changamoto zinazowazunguka.

Mwito huo umetolewa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, wakati wa Mahafali ya 25 ya chuo hicho yaliyofanyika katika Ndaki ya Mbeya, mkoani Mbeya.

Dkt. Shein amewasisitiza wahitimu hao kutumia maarifa na ujuzi walioupata kwa manufaa ya jamii, akieleza umuhimu wa kujitofautisha kupitia matendo yanayoonesha utu, uadilifu, kuheshimu wengine na kuzingatia maadili ya Kitanzania. Amesisitiza kuwa elimu inapaswa kuwa nyenzo ya kuboresha maisha ya watu na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Mlau wa Mahafali, Prof. Elizabeth Lulu Genda, amewataka wahitimu kukabiliana na changamoto za maisha kwa uvumilivu, ubunifu na uthubutu badala ya kulaumu Serikali, mifumo au jamii wanapokutana na vikwazo.

Prof. Genda amesema ukosefu wa ajira, mitaji, urasimu na uhaba wa fursa ni miongoni mwa changamoto ambazo wahitimu wanaweza kukutana nazo wanaporejea katika jamii, hivyo wanapaswa kutafuta mbinu sahihi za kuzivuka badala ya kukata tamaa.

“Msipoteze muda na rasilimali zenu kugombana na mambo yatakayowakinga katika safari ya maisha. Chunguzeni kwa makini na kutafuta namna ya kuvuka vikwazo hivyo,” alisisitiza Prof. Genda.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amewataka wahitimu kutumia elimu yao kwa uadilifu, ubunifu na bidii ili kuanzisha shughuli za uzalishaji mali, kutengeneza fursa na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Prof. Mwegoha pia amewahimiza wahitimu kudumisha uhusiano na chuo chao kwa kushirikiana, kushauriana na kusaidia wanafunzi kupata fursa za ajira na ujasiriamali, akisisitiza kuwa mtandao wa wahitimu unaweza kuunganisha maarifa, uzoefu na fursa kwa manufaa ya wahitimu wenyewe, chuo na jamii kwa ujumla.

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 1,212, wakiwemo wanaume 587 na wanawake 625, wametunukiwa tuzo za kitaaluma katika ngazi za Shahada ya Umahiri, Shahada ya Awali, Stashahada na Astashahada.

Naye, mhitimu bora wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Ndg. Lugano Mwapongo amewataka wahitimu kutumia maarifa waliopata chuoni hapo kuleta maendeleo katika jamii. Aidha, ameeleza kuwa ni mwiko kukata tamaa hivyo wahitimu na wanafunzi waendelee kuweka juhudi zenye kuleta mafanikio.

Mahafali hayo yanaweka bayana kuwa thamani ya elimu haipo katika vyeti pekee, bali pia katika uwezo wa wahitimu kutumia maarifa yao kutatua changamoto, kufungua fursa na kuboresha maisha ya watu. Kwa wahitimu hao, hatua inayofuata ni kuyageuza maarifa waliyoyapata chuoni kuwa matokeo yanayoonekana katika jamii na maendeleo ya Taifa.







Na. Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wadau wa sekta ya afya wapewa mafunzo ya siku nne jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 26 hadi 29 Oktoba, 2026, yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu Kinga Dhidi ya Unyonyaji, Ukatili wa Kingono na Unyanyasaji (Protection from Sexual Exploitation, Abuse and Harassment – PSEAH) ili kuendelea kulinda haki, utu na usalama wa wananchi wanaonufaika na huduma za afya.

Warsha hiyo inalenga kuimarisha mifumo ya ulinzi, uwajibikaji na maadili katika utekelezaji wa programu zinazofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) na ni sehemu ya juhudi za kujenga uwezo wa taasisi kuzuia vitendo vya unyonyaji, ukatili na unyanyasaji wa kingono, kuweka mifumo madhubuti ya kuripoti matukio, na kuhakikisha manusura wanapata msaada unaozingatia mahitaji yao.

Serikali, kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia, inaendelea kuimarisha usimamizi, uratibu na uwajibikaji katika utekelezaji wa programu hizo, huku ikihakikisha zinazingatia viwango vya juu vya uadilifu na maadili.

Maeneo makuu yaliyotiliwa mkazo wakati wa warsha hiyo ni pamoja na kuimarisha uwezo wa viongozi na wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Uratibu wa Mfuko wa Dunia (TNCM) katika usimamizi, utawala unaozingatia maadili, na uwajibikaji katika utekelezaji wa PSEAH na sehemu ya pili inahusisha Wizara ya Fedha kama Mpokeaji Mkuu wa Ruzuku (Principal Recipient – PR), Wizara ya Afya kama Mpokeaji Kiongozi wa Ruzuku Ndogo (Lead Sub-Recipient - LSR), pamoja na wapokeaji wengine wa ruzuku ndogo, kwa lengo la kuimarisha mifumo ya ulinzi ndani ya taasisi zao.

Vilele, inajikita katika utekelezaji salama wa programu, hususan kutathmini na kupunguza hatari za unyonyaji, ukatili na unyanyasaji wa kingono katika ngazi ya utoaji huduma.

Miongoni mwa viongozi walioshiriki warsha hiyo ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mwenyekiti wa TNCM, Dkt. Jim Yonazi, Makamu Mwenyekiti wa TNCM, Godlisten Moshi, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Prof. Tumaini Nagu, Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI, Dkt. Adam Mrisho na Katibu Mtendaji wa TNCM, Kent Pius.