Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nkoba Mabula, ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuboresha miundombinu ya barabara, maji, umeme na mawasiliano, pamoja na kuimarisha vitendea kazi na kutoa elimu kwa watumishi na wadau ili kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa.

Akiwa katika ukaguzi wa miundombinu ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mabula ameelekeza kasi ya maboresho iongezwe katika maeneo hatarishi, maandalizi ya mitambo na huduma za afya, pamoja na kutolewa kwa mafunzo ya vitendo kwa timu za uokoaji zinazojumuisha maafisa na askari wa uhifadhi.

“Kama El Niño itakuja, itukute tumejiandaa. Mitambo, magari ya huduma, mafuta na vipuri viwepo wakati wote ili kuhakikisha usalama wa watalii, wananchi na rasilimali za wanyamapori na malikale zilizopo,” amesema Mabula.

Ameongeza kuwa ni muhimu kuweka alama katika maeneo hatarishi ili kuongeza tahadhari kwa watumiaji wa barabara na maeneo mengine yanayoweza kuathiriwa na mvua hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Ngorongoro, SACC Gloria Bideberi, amesema mamlaka hiyo imeendelea kutoa elimu kuhusu namna ya kukabiliana na athari za mvua hizo kwa makundi mbalimbali.

Amesema hadi sasa elimu imetolewa kwa watumishi 200, viongozi wa vijiji na kata 275, wanafunzi zaidi ya 1,550 na wananchi 4,965 katika kata 10 zilizopo ndani ya hifadhi.

Aidha, amesema maeneo 80 ya huduma za malazi yamehusishwa katika maandalizi hayo, huku magari ya huduma za dharura na vifaa tiba vikiandaliwa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, Mratibu wa Shughuli za Miundombinu, Mhandisi Shaban Felician, amesema mitambo zaidi ya 11 imeandaliwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara, pamoja na uokoaji wa magari ya wageni yanayoweza kukwama kutokana na mvua.

Amesema mamlaka hiyo pia inaendelea kuhakikisha mtandao wa barabara wenye urefu wa zaidi ya kilomita 600 ndani ya hifadhi unabaki kupitika katika msimu wote wa mvua, ili kuwezesha shughuli za uhifadhi na utalii kuendelea bila kukwama.






-Aelezea jinsi shirika lilivyotumia mabilioni ya fedha kusogeza huduma karibu na wananchi

-Asema TBS ina jumla ya maabara 14 na zote zimeweza kupata ithibati za umahiri


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

KATIKA kipindi cha Serikali ya awamu ya Sita (2021-2026), chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan Shirika la Viwango Tanzania( TBS) limekuwa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mafanikio hayo yanaendana na kutimiza azma ya Shirika katika masuala mbalimbali yakiwemo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali iliwa na lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 27,2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania(TBS) Dkt. Ashura Katunzi alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi kilichohusisha Wahariri wa vyombo vya habari nchini.Kikao kazi hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ikiwa ni muendelezo wa mashirika ya umma na taasisi kutoa taarifa za mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Akifafanua zaidi Dk.Katunzi amesema TBS inaendelea na hatua za mwisho za ukamilishaji na makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa maabara na ofisi katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma, au kwa jina jingine mradi wa Viwango House – Dodoma wenye thamani ya TZS 24.7 Bilioni.

Pia Shirika linaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa ofisi na maabara katika Kanda ya Ziwa eneo la Kiseke Wilaya ya Ilemela – Mwanza unaojulikana kama Viwango House- Mwanza ambao unakadiriwa kugharimu Sh.bilioni 12.1 Bilioni huku pia likiwa hatua za awali za maandalizi za mradi wa ujenzi wa ofisi na maabara Jijini Arusha.

Pia amesema kwa upande wa Dodoma, maabara zilizojengwa zinahudumia pia mikoa ya karibu na Dodoma hususani Singida na Tabora. Aidha, maabara za Mwanza zinatarajiwa kuhudumia mikoa sita, ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.

Amefafanua hatua hiyo ya ujenzi wa ofisi na maabara itasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa majibu ya vipimo vya sampuli.

Wakati huo huo amesema Serikali kupitia TBS imetumia zaidi ya Sh.bilioni 9.8 bilioni kwa ajili ya kuimarisha ofisi tisa za kanda.

Pia amesema ili kuwezesha Biashara, Shirika lina Kamati za Kitaalam (Technical Commitees) za Uandaaji Viwango 117 katika sekta ya chakula, kemikali, uhandisi mitambo, uhandisi umeme, uhandisi ujenzi, nguo na ngozi, madini na mitambo ya uchimbaji madini, mazingira na taaluma mtambuka (general tecniques).

“Katika mchakato wa kuandaa viwango Kamati hizo zinashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu, taasisi za utafiti, wafanyabiashara, wazalishaji, vyama vya walaji, vyama na bodi za wataalam, taasisi za udhibiti na watunga sera.”

Pia amesema Shirika limefanikiwa kuandaa viwango 3901 vya sekta mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya soko ambavyo vinasaidia wafanyabiashara, wajasiriamali na watoa huduma kuzalisha bidhaa bora zenye kukidhi matakwa ya viwango, hivyo kuwawezesha kufanya biashara ndani na nje ya nchi, hatua ambayo italeta tija na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Aidha, jumla ya vyeti na leseni za ubora 3,940 vimetolewakwa wazalishaji, miongoni mwao wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,683. Serikali kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya TZS milioni 300 kila mwaka kwa madhumuni ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote.

“Leseni hizi zimesaidia wazalishaji kuzalisha bidhaa bora, ikiwa ni pamoja na bidhaa zao kuweza kuaminika sokoni na pia kufanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.

“Shirika limeendelea na huduma za usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi pamoja na maeneo ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula na vipodozi kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wa maeneo hayo ili kuendelea kulinda afya za walaji ambapo jumla ya bidhaa 9,731 zilisajiliwa na maeneo 80,836 yalisajiliwa.”

Ameongeza katika kuimarisha ukaguzi wa bidhaa zinazoingia nchini kutoka nchi za nje, TBS huhakiki ubora wa bidhaa na magari yaliyotumika kabla ya kusafirishwa kuja nchini ambapo katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita jumla ya shehena za bidhaa 183,186 zilikaguliwa kabla ya kuingia nchini kupitia mfumo wa Pre-Shipment to Conformity (PVoC).

“Shehena za bidhaa 426,842 zilikaguliwa baada ya kufika nchini kupitia mfumo wa Destination Inspection (DI).Jumla ya magari 249,386 yalikaguliwa. Bidhaa hizo zinakaguliwa kwa lengo la kuiepusha Tanzania kuwa jalala la bidhaa duni pamoja na kulinda afya, usalama na mazingira ya watumiaji.

Kuhusu kuongeza ufanisi wa maabara amesema TBS ina jumla ya maabara 14 na zote zimeweza kupata ithibati za umahiri, ambapo maabara hizo zimehakikiwa na kupatiwa vyeti vya ithibati ya umahiri wa kimataifa.

“Hatua hiyo inamaanisha kuwa majibu ya sampuli kutoka katika maabara hizo yanaaminika na kukubalika popote duniani na hivyo kurahisisha biashara ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.Katika kipindi hicho TBS imeweza kupima sampuli zaidi ya 188,952 na kufanyia ugezi vifaa 54,396ambapo suala hili litasaidia kuhakikisha katika soko kunakuwa na bidhaa zenye ubora.”

Pia, maabara hizo zina mashine za kisasa (state-of -art-equipment) zinazopelekea kupata majibu kwa wakati na sahihi, Serikali imeweza kutumia kiasi kisichopungua Sh.12.9 bilioni kuhakikisha mashine hizi zinapatikana.

“Kuna mashine za kipekee ikiwemo ya hydrostatic pressure test ya kupima mabomba ya maji na yenye uwezo wa kupima mabomba yenye kipenyo cha milimita 12 sawa na inch 0.5 hadi milimita 800 sawa na inchi 32. Mashine hiyo ina uwezo pia wa kupima sampuli 120 kwa wakati mmojana kati ya nchi 54 za Barani Afrika inapatikana katika nchi tano tu ikiwemo Tanzania.










MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt Nicas Mawazo amezindua Casino ya Kisasa inayofahamika kana CLEOPATRA iliyopo maeneo ya stendi ya zamani.

Akizungumza katika uzinduzi huo Dkt. Mawazo ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo, amewapongeza uongozi wa CLEOPATRA kwa kuongeza ajira kwa vijana ndani ya Manispaa ya Kibaha Mkoani Pwani.

Amesema hawa waru nimuhimu sana katika Mkoa wetu wa Pwani na nchi nzima kwa ujumla sababu wanaleta ajira za uhakika kwa vijana wetu.

Aidha Mstahiki Meya amesema kuwa akiwa meza kuu Mkurugenzi Mtendaji wa CLEOPATRA CASINO Juma Mlali amemweleza kuwa anatamani wapate eneo ili waweze kuwekeza kwa kujenga Kiwanda .

"Niseme ukweli ni kwamba nimefurahishwa na nia njema aliyonayo hivyo nawakaribisha sana ofisini ili tuweze kuelewana zaidi na hata kama hawana pesa sisi tutawakopesha na kuwapa eneo.

"Manispaa ya Kibaha tunataka wawekezaji vijana na wenye maono namna hii tunajivunia kuwa na watu wa namna hii sisi tupo na Mwekezaji yeyote anayetaka kuwekeza aje tunayo Kongami ya Viwanda ,kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo anasema karibuni Pwani ni tulivu na kuna usalama wa kutosha" amesema Dkt. Nicas.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa CLEOPATRA amesema kuwa wanajivunia kwa kutoa ajira kwa vijana wengi katika mikoa yote nchini. 

"Tuna matawi nchi nzima nantumetoa ajira 400 na kwa upande wa uwekezaji tutaanza kujenga Kiwanda cha vinywaji mbalimbali" amesema Mlali.


Na Mwandishi Wetu, Mkuranga

Warembo wanaowania taji la Miss Eastern Zone wanatarajiwa kuchuana katika fainali za shindano hilo zitakazofanyika Novemba 6, 2026, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, ambapo mshindi atajinyakulia zawadi ya gari pamoja na tiketi ya kushiriki fainali za Miss Tanzania 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 27, 2026, wilayani Mkuranga, Mkurugenzi wa Miss Eastern Zone, Yusuf Hassan, amesema maandalizi ya shindano hilo yanaendelea na washiriki wanatarajiwa kuingia kambini hivi karibuni katika Kisiwa cha Vikuruti kilichopo Mkuranga.

Amesema warembo hao watasafiri kwa usafiri wa majini kutoka Sea Cliff, Masaki, jijini Dar es Salaam, kuelekea kisiwani humo, huku washiriki wengine wakitarajiwa kupata zawadi mbalimbali.

Hassan amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Idara ya Utamaduni na Michezo, kwa juhudi za kuwezesha vijana kunufaika na mikopo ya makundi maalumu.

Pia amewashukuru Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga kwa maelekezo na ushirikiano wao katika kufanikisha maandalizi ya shindano hilo.

Amesema shindano hilo linatarajiwa kunogeshwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, akiwemo D-Voice wa lebo ya WCB, Isha Mashauzi, Yammy Tz na Dogo Parten, pamoja na wasanii wazawa kutoka Mkuranga na Mkoa wa Pwani.

Aidha, amesema mdau mkubwa wa shindano hilo ni BOSS BOSS, huku Adey na wadau wengine wakitajwa kuwa miongoni mwa wanaounga mkono maandalizi yake.

Kuhusu tiketi, Hassan amesema tayari zimeanza kuuzwa kwa bei ya Sh20,000 kwa tiketi ya kawaida, Sh50,000 kwa VIP na Sh100,000 kwa VVIP.

Amesema tiketi hizo zinapatikana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga na ofisi za utamaduni mkoani humo, pamoja na Parachichi, BOSS BOSS Vikindu na Samaki Sport, Morogoro.


WAZIRI  wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Homera, amepongeza juhudi za Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy, katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, huku akitangaza kuongezwa kwa kasi ya operesheni ya kuwasha umeme katika kila kitongoji nchini.


Waziri Homera amesema operesheni hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi katika maeneo yote nchini, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hususan katika maeneo ya vijijini.

Akizungumza wakati akiwasha umeme Kitongoji cha Lindi B, Wilaya ya Namtumbo, na Kitongoji cha Nakanyonyo, Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, amesema Wakuu wa Mikoa wataendelea kushiriki katika kuwasha umeme kwenye miradi iliyokamilika ili kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika na huduma hiyo kwa wakati.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza kasi ya matumizi ya miundombinu ya umeme iliyokamilika, huku Serikali ikiendelea kutekeleza miradi mipya katika vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa umeme mkoani Ruvuma, Waziri Homera amesema mkoa huo una jumla ya vitongoji 3,691, ambapo vitongoji 2,235 tayari vimefikiwa na umeme, sawa na takribani asilimia 61 ya vitongoji vyote.

Amesema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 224.7 katika miradi mbalimbali ya umeme inayotekelezwa na REA mkoani humo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua wigo wa upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Waziri Homera, vitongoji 799 vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya kuviunganishia umeme, huku vitongoji 657 vikiwa bado havijafikiwa na huduma hiyo na havipo katika miradi inayoendelea kutekelezwa.

Amefafanua kuwa kukamilika kwa miradi inayoendelea kutasaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme katika vitongoji vya Mkoa wa Ruvuma kutoka asilimia 61 ya sasa hadi takribani asilimia 82.

Amesema ongezeko hilo linatarajiwa kufungua fursa zaidi za shughuli za kiuchumi, ikiwemo biashara, uzalishaji mali na utoaji wa huduma za kijamii, hivyo kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo ya vijijini.

Aidha, Waziri Homera amewataka wananchi kuendelea kuiombea Wizara ya Nishati ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha azma ya kufikisha umeme kila kitongoji inafikiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini imeendelea kuongezeka na kwamba Wakala hautarudi nyuma katika kutimiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma ya umeme.

Mhandisi Saidy amesisitiza kuwa Wakala utaendelea kuongeza juhudi za kusogeza huduma ya umeme katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa, sambamba na kufungua fursa mpya za kiuchumi, kuongeza uzalishaji na kuboresha ustawi wa wananchi wa vijijini.



Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Mariam Ibrahim, ametoa wito kwa taasisi za dini, wazazi, walezi, waelimishaji na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kuhusu stara, kukuza maadili, kuimarisha malezi bora na kulinda ustawi wa watoto na wanawake nchini.


Mariam ametoa wito huo Oktoba 25, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za Muslim Stara Women Awards, msimu wa kwanza, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City.

Amesema stara inapoambatana na elimu, malezi bora na tabia njema, humsaidia binti kujenga kujiamini, kuheshimu utu wake na kufanya maamuzi yenye busara.

Ameongeza kuwa stara ina mchango katika kukuza maadili na mahusiano yenye heshima ndani ya familia, pamoja na kuimarisha utamaduni wa kuheshimiana, uwajibikaji na kuishi kwa amani katika jamii.
“Nitoe wito kwa taasisi ya Juby Enterprises Limited, taasisi za dini, wazazi, walezi, waelimishaji na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu ya stara, kukuza maadili, kuimarisha malezi bora na kulinda ustawi wa watoto na wanawake,” amesema Mariam.























MOSHI.


MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ameitaka Taasisi ya Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani (NAESA) kushirikiana kwa karibu na maafisa kilimo wa mkoa huo ili kuongeza tija katika sekta za kilimo na ufugaji, hususan katika utoaji wa elimu na ushauri wa kitaalamu kwa wakulima kupitia maafisa ugani.

Babu ameyasema hayo alipokutana na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo waliotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa lengo la kuitambulisha NAESA ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha usimamizi na utendaji wa huduma za ugani nchini.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha huduma za ugani na kuhakikisha kuwa wakulima na wafugaji wanatumia mbinu bora za uzalishaji, hatua itakayochangia kukuza uchumi wa wananchi na maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Akizungumza wakati wa utambulisho huo, Mkurugenzi wa Mafunzo kutoka NAESA, Felix Mrisho, ameeleza kuwa miongoni mwa majukumu ya taasisi hiyo ni kuratibu na kusimamia huduma za ugani katika sekta ya kilimo pamoja na kuanzisha na kusimamia miundombinu ya teknolojia za kilimo.

Alifafanua kuwa kitaifa NAESA itashirikiana na Ofisi za Wakuu wa mkoa, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na wadau wengine wa sekta ya kilimo katika kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini shughuli za ugani.

Hata hivyo ushirikiano huo unalenga kuboresha upatikanaji na kuongeza ufanisi wa huduma za ugani kwa wakulima, ili kuwawezesha kupata utaalamu na mbinu bora za kilimo zitakazochochea uzalishaji na tija katika sekta hiyo.




Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Serikali inatarajia kuzindua rasmi majengo 37 ya wizara na taasisi za Serikali pamoja na kilomita 57.1 za barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Oktoba 30, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha utendaji wa Serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Profesa Palamagamba Kabudi, amesema majengo yatakayozinduliwa yanajumuisha majengo 24 ya wizara na 13 ya taasisi za Serikali. Ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hizo za lami umegharimu Shilingi Bilioni 110.5.

Profesa Kabudi amesema kukusanywa kwa wizara na taasisi za Serikali katika eneo moja kutarahisisha uratibu wa shughuli za Serikali, kuboresha mawasiliano baina ya taasisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi. Hatua hiyo pia inalenga kupunguza changamoto zinazotokana na ofisi za Serikali kutawanyika katika maeneo mbalimbali.

Ameeleza kuwa majengo hayo ni sehemu ya awamu ya pili ya mradi wa Mji wa Serikali Mtumba, unaohusisha pia majengo mengine 35 ya taasisi mbalimbali yaliyokamilika nje ya eneo la Mji wa Serikali, yakiwemo yaliyopo Chang’ombe na Njedengwa.

Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, uwekezaji huo unaendelea kuimarisha hadhi ya Dodoma kama Makao Makuu ya nchi na kitovu cha shughuli za Serikali, huku ukifungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi na sekta binafsi.

Amewahimiza wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa jiji la Dodoma, hususan katika sekta za usafirishaji, malazi, biashara na huduma za kitaalamu. Amesema kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato kunatarajiwa kuongeza zaidi fursa hizo kadiri idadi ya watu wanaotembelea jiji hilo itakavyoongezeka.

Aidha, amewataka watumishi wa umma watakaofanya kazi katika Mji wa Serikali Mtumba kutumia miundombinu hiyo kwa ufanisi na kuzingatia misingi ya uwajibikaji, uadilifu, nidhamu na uzalendo ili kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Katika hatua nyingine, Profesa Kabudi amewaalika wananchi, hususan wakazi wa Dodoma, kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo. Amesema shamrashamra za kuelekea uzinduzi zitahusisha upigaji fataki usiku wa kuamkia Oktoba 30, 2026.

Amesisitiza kuwa mradi huo unaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendeleza miundombinu ya kisasa na kuimarisha utoaji wa huduma za umma nchini.







Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi Ajira na Mahusiano Mhe Deus Sangu, akimpongeza Mkurugenzi wa Fedha Mfuko wa PSSSF Bw. Ally Yakuti, baada ya kukabidhiwa mfano wa hundi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.07 ikiwa ni Gawio kutokana na uwekezaji wa Mfuko kwenye Mradi wa Rock City Mall ya jijini Mwanza. Hafla hiyo imefanyika jijini Dodoma Oktoba 27, 2026.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi Ajira na Mahusiano Mhe Deus Sangu, akizungumza wakati wa hafla hiyo





Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mwanza City Company Limited, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo akizungumza kwenye hafla hiyo





Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa PSSSF Bw Fortunatus Magambo (kulia) akisalimiana na viongozi wa jiji la Mwanza wakati wa hafla ya kukabidhi Gawio kwa wabia wa Rock City Mall jijini Dodoma Oktoba 27, 2026





Dodoma, Oktoba 27, 2026

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema uwekezaji uliofanywa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma PSSSF kwenye mradi wa Rock City Mall jijini mwanza ni ishara kwamba michango ya wanachama inalindwa, inakua na kurejesha faida kwa Taifa.

Mhe. Sangu ameyasema hayo jijini Dodoma Oktoba 27, 2026 wakati Kampuni ya Mwanza Rock City Ltd ambayo ndiyo inasimamia mradi huo ikitoa gawio la jumla ya Shilingi 1.18 bilioni kwa wabia wake watatu ambao ni; PSSSF ambayo imepokea Shilingi 1.07 bilioni; Halmashauri ya Jiji la Mwanza imepokea Shilingi 71.3 milioni na Manispaa ya Ilemela imepokea Shilingi 47.56 milioni. PSSSF ambayo ni taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), ndiye mwekezaji mkuu katika mradi huo.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza Mhe. Constatine Sima, Mstaiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe. Sarah Ng’wani, na Mstaiki Meya wa Halmashauri ya Ilemela, Mhe Renatus Mulunga pamoja na Waheshimiwa Madiwani.


“Ninapenda kutoa pongezi za dhati kwa Bodi na Menejimenti ya Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii, hususan PSSSF, kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuhakikisha michango ya wanachama inalindwa, inakua na kurejesha faida kwa Taifa. Leo hatupokei gawio tu, tunapokea uthibitisho kuwa mfumo wetu wa hifadhi ya jamii uko imara, unakua na unalipa.” Alisema Mhe. Sangu.


Mhe. Waziri Sangu alisema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaogozwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. Dira hiyo inatuambia kuwa Tanzania tunayoitaka ni ya uchumi imara, wa viwanda, usio na umaskini, na wenye ajira zenye staha kwa kila Mtanzania.


“ Hivyo, jitihada hizi zinaonekana kwa wabia wote wa mradi huu wa Rock City Mall ambao ni PSSSF, Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Ilemela kwa usimamizi mzuri wa mradi ambao pia umezalisha ajira. Bila usimamizi wenu pengine leo tusingekuwa hapa kushuhudia tukio hili kubwa kwa wabia hawa. Hongereni sana….!” Alisema.


Nawapongeza PSSSF kwa uwekezaji huu wenye tija kwa taifa letu, kwani nimeelezwa mpaka sasa asilimia 98 ya jengo lina wapangaji. Pamoja na kupendezesha jiji letu la Mwanza, mradi huu unanufaisha watu zaidi ya 1000 kupitia ajira za kudumu na za muda, kwa kufanya hivyo mnaunga mkono juhudi za Serikali kwa kuzalisha ajira kwa vijana wetu, alisema Mhe. Sangu.


Aidha Mhe. Sangu ametoa wito kwa PSSSF na taasisi nyingine zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) kuhakikisha wanafuata miongozo ya uwekezaji inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania pamoja na sera za uwekezaji za taasisi husika ili kuweza kufanya uwekezaji wenye tija kama huu ambao leo tunashuhudia ukitoa gawio kwa wabia wake.


“Lengo la kuwekeza ni kulinda thamani ya michango ya Wanachama ili wanapokuja kustaafu waweze kulipwa mafao ambayo ni zaidi ya michango yao waliyokuwa wanachangia katika Mfuko, hivyo, kutokana na mafanikio ya mradi huu tunaamini sehemu hii ya gawiwo itachangia katika kuwafanya wanachama wa PSSSF KULIPWA JANA.” Alisisitiza.






Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa PSSSF, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mwanza Rock City Company Limited, Bw. Fortunatus Magambo, amelinganisha tukio hilo na siku ya mavuno.

“Hakika ile mbegu tuliyopanda, ilimea vyema na hatimaye leo tunavuna tulichopanda, hakika leo ni siku muhimu sana.” Alisema Bw. Magambo.



Bw. Magambo alisema, Rock City Mall ina mchango kwa jamii na maendeleo ya Jiji la Mwanza kwa kuwa kituo cha huduma mbalimbali, ambapo faida zake ni pamoja na; Kurahisisha upatikanaji wa huduma, inakusanya huduma mbalimbali katika eneo moja, zikiwemo maduka, huduma za benki na migahawa mbalimbali.



“Hii huwasaidia wananchi kuokoa muda na kurahisisha shughuli zao, Rock City Mall inatoa nafasi za biashara na ajira, inatoa maeneo ya kufanyia biashara na kuchangia fursa za ajira kupitia maduka, migahawa na huduma nyingine zinazopatikana hapo.



Aidha, Bw. Magambo alisema, PSSSF inawekeza ili kulinda thamani ya michango ya Wanachama ili wanapokuja kustaafu waweze kupata mafao zaidi ya michango yao waliyokuwa wanachangia katika Mfuko.



“ Uwekezaji wa Mfuko unaongozwa na Mwongozo wa Uwekezaji kutoka Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Sera ya Uwekezaji ya Mfuko. Sehemu kubwa ya uwekezaji upo katika dhamana za serikali, hisa za kampuni na amana za mabenki na si kwenye majengo kama wengi wanavyodhani.” Alisisitiza.